Prime
Msimamo mkataba wa uwekezaji wa bandari

Dar es Salaam. Hakuna unachoweza kusema zaidi ya kueleza kuwa suala la bandari limeendelea kuwa na mitazamo na misimamo tofauti.
Wakati jana Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ikiweka bayana msimamo wake kwa umma wa kupinga mkataba wa ushirikiano wa uwekezaji na uendelezaji wa bandari nchini kati ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai, jana hiyohiyo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa aliongoza timu ya wataalamu walioshughulikia mkataba huo kutoa elimu kwa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), akitetea uwekezaji huo, sambamba na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro ambaye naye alilizungumzia.
Mbali na wote hao, Rais Samia Suluhu Hassan alitumia sehemu ya hotuba yake fupi Ikulu ya Dar es Salaam, wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni, kuelezea umuhimu wa kuchangamkia fursa ikiwemo hiyo ya uwekezaji bandarini na kuzilinda.
Katika maelezo yake, Rais Samia alisema: “…hili la fursa, nataka niseme vizuri, wakati sisi tunalumbana, bandari apewe nani, iende, isiende, ikae, wenzetu kwa kuona malumbano yetu, wameruka, wamekwenda kulekule na lilelile jumba lililowekwa bendera ya Tanzania limeweka bendera ya jirani, sasa Tanzania tumeuza wale jirani wamekimbilia kule wemekwenda kufanya nini?”
Rais aliongeza: ‘‘ Siku ileile Bunge linaridhia azimio la kukubali ushirikiano, siku ya pili wakasema ninyi bandari moja, sisi zote na wakakimbia kuwahi nafasi, sasa muone jinsi fursa zinavyokuja na kukimbia harakaharaka.”
Licha ya Rais Samia kutobainisha jina la jirani wala hilo jumba, lakini alikuwa akimaanisha ni nchi ya Kenya ambayo rangi ya bendera yake ilipambwa kwenye mnara wa Burj Khalifa uliopo Dubai, kama ilivyokuwa kwa rangi ya bendera ya Tanzania iliyowahi kupambwa kwenye mnara huo.
Si kauli ya kwanza kwa Rais Samia kuhusu suala hilo kwani Juni 13 mwaka huu, mara tu baada ya kuwasili jijini Mwanza kuanza ziara aligusia akisema atafanya kila analoweza kufanya Tanzania iendelee.
“Tanzania ni moja, haigawanyiki wala haiuziki. Kwa hiyo ndugu zangu mama ni Mtanzania, maendeleo yetu ndiyo muhimu, kila linalofanyika ni kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania,” alisema.
Mbarawa na wahariri
Waziri Mbarawa aliongoza timu ya wataalamu mbalimbali wa wizara yake ya ujenzi na uchukuzi akiwemo Hamza Johari, aliyeongoza timu ya majadiliano ya mkataba huo wa uwekezaji kuzungumza na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
Katika mkutano huo ulioanza saa 4 asubuhi na kumalizika saa 8 mchana huku ukirushwa moja kwa moja na vyombo vya habari ambapo wahariri walipata fursa ya kuwasikiliza wataalamu pamoja na kuuliza maswali.
Johari alisema uwekezaji utakaofanywa na kampuni ya DP World, ni asilimia nane pekee ya shughuli zote zinazofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TPA).
Hamza ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) alisema kutokana na ufinyu huo wa uwekezaji, ndio maana Zanzibar na bandari zingine ikiwemo ya Mtwara haikutajwa kwenye mkataba huo.
Alisema DP World haitakuwa na haki ya kumiliki ardhi ya Tanzania kama inavyosemwa, bali maeneo yote itakayofanyia kazi itakodishiwa na si kumilikishwa.
Hamza ambaye ni kitaluma ni mwanasheria wa sheria za kimataifa, alisema kampuni hiyo itakapokuja kuwekeza nchini lazima isajiliwe Tanzania na asilimia 35 ya wafanyakazi wake watakuwa ni Watanzania.
“Ni kama ilivyokuwa Ticts (Kampuni binafsi ya kimataifa ya kuhudumia makontena Tanzania), atatoa hisa kwa Watanzania, pia atalipa kodi na asilimia 35 ya wafanyakazi ni wazawa, kwa hiyo DP World hawawezi kuja nchini mzima mzima,” alisema na kuongeza: “Mkataba huu wa ushirikiano hauna shida yoyote na ninaposikia watu wanazungumza nasikitika sana.”
Kuhusu maoni yaliyotolewa na Mwanazuoni nguli, Profesa Issa Shivji, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na wadau mbalimbali kuhusu mkataba huo, Serikali ilisema itafanyia kazi kwenye mikataba ya kibiashara itakayosainiwa baina ya TPA na DP World.
Mwanasheria wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mohamed Salum alisema asilimia 80 hadi 90 ya maoni yaliyotolewa kuhusu mkataba huo, yamegusa mikataba midogomidogo ambayo maoni hayo yatazingatiwa kabla ya kusainiwa.
“Kama Serikali tutachambua maoni ya TLS tukiona kuna vipengele vitaathiri utekelezaji wa huo mkataba wa biashara, tutakwenda kwenye mabadiliko kwa mujibu wa ibara ya 22,” alisema
Kuhusu maoni Profesa Shivji, Salim alisema mwanazuoni huyo alichambua vyema mkataba huo hasa akigusia kuwa mkataba huo ni wa upande mmoja.
Alisema ipo tofauti kubwa kati ya
mkataba wa BIT na IGA akifafanua kwamba BIT ni mkataba wa jumla baina ya nchi na nchi kuvutia wawekezaji baina ya nchi nan chi,
Salim alisema IGA inagusa mkataba mahususi kwenye mradi, hivyo kwa kuwa eneo la bandari ya Tanzania ndio uwekezaji unafanyika lazima haki itolewe kwa DP World na Tanzania iwe na wajibu.
“Mkataba huu hautoi haki kwamba Tanzania ikawekeze Dubai, ingekuwa BIT ingekuwa na taswira ya jumla tunazungumza haki na wajibu wa Tanzania, haki na wajibu alizozungumza Profesa Shivji yupo sahihi lakini kwa sababu hii IGA, inatoa hakikisho kwa Serikali ya Dubai kwa uwekezaji utakaofanya Tanzania,” alisema
Kwa upande wake, Waziri Mbarawa alisema kwa sasa bandari ya Dar es Salaam inachangia asilimia 37 kwenye pato la Taifa na endapo uwekezaji huo utafanikiwa utachangia asilimia 67.
"Tuna jukumu kubwa kwas ababu nyote mnajua Serikali inajenga miradi mikubwa na hatutaendelea kila siku kupeleka bakuli kuomba omba wakati tuna rasilimali ambayo tukiitumia vizuri na kuendesha vizuri, tutaweza kubadilisha uchumi wa Tanzania," alisema.
Msimamo wa Chadema
Jana hiyohiyo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alikutana na waandishi wa habari kutoa maazimio ya kamati kuu ya chama hicho iliyokutana Julai 8 mwaka huu kuhusu suala hilo pekee na mengine akisema yatatolewa wakati mwingine.
Kutokana na maazimio hayo, operesheni ya chama hicho ya '+255 Katiba Mpya' kwa sasa itajulikana kama '+255 Katiba Mpya, Okoa Bandari Zetu.”
Operesheni +255 Katiba Mpya ilizinduliwa Mei 17, mwaka huu mkoani Kigoma ikilenga kikuhuisha chama hicho kuanzia ngazi ya chini na kuhamasisha umma juu ya kuidai Katiba Mpya. Awamu ya pili ya operesheni hiyo itazinduliwa Julai 28, mwaka huu.
Mabadiliko ya operesheni hiyo ni miongoni mwa maazimio ya Kamati Kuu hya Chadema na kwamba wataizindua mkoani Kagera na kuendelea katika mikoa ya Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara.
"Tunakusudia kuifanya nchi nzima na itazinduliwa kwa kwenda kutangaza namna CCM na Serikali yake inavyoharibu nchi kwa mikataba isiyo na tija kwa kizazi cha leo, kesho na keshokutwa.
“Tumesema tunakwenda kuonana na wananchi, itoshe kusema mwambao wote wa Pwani tutaugusa tutakutana taifa zima," alisema Mbowe.
Azimio lingine la Kamati Kuu kwa mujibu wa Mbowe ni kufutwa kwa mkataba huo na alisisitiza, chama hicho kitafanya kila namna kuhakikisha Serikali inalitekeleza hilo.
"Msimamo wa Chadema ni kwamba mkataba huu ufutwe wote, aidha tutatumia njia mbalimbali ndani na nje ya nchi kuhakikisha mkataba unafutwa na maslahi ya nchi yanalindwa," alisema.
Mbali na kufutwa mkataba, Mbowe alisema kamati kuu hiyo iliazimia Bunge lifute azimio lake la kuridhia mkataba huo kwa kuwa hauna maslahi kwa nchi.
Alieleza kamati kuu iliazimia Serikali iwachukulie hatua kwa mujibu wa sheria, watu wote walioshiriki kuingiza nchi katika mkataba huo usiorekebishika na unaolidhalilisha Taifa.
"Kamati Kuu inaunga mkono jitihada mbalimbali za wananchi kupinga mkataba huo, ikiwemo walioamua kufungua kesi katika mahakama," alisema Mbowe.
Maazimio mengine ni kushirikiana na wananchi bila kujali itikadi zao katika kupinga mkataba huo na kuwahimiza kuona haja ya kudai Katiba Mpya.
"Ikiwa Bunge na Serikali hazitachukua hatua, Chadema itaanzisha na kuhamasisha umma kuchukua hatua kali dhidi ya Serikali hadi itakapochukua hatua," alisema.
Alieleza kamati kuu hiyo imeridhika kuwa mkataba huo unakwenda kinyume cha Katiba na sheria za nchi na kimataifa na umesababisha Serikali kuwasilisha bungeni muswada wa mabadiliko ya sheria ya kumiliki maliasili za nchi.
"Kamati Kuu imejiridhisha kuwa hakuna utafiti wa kisayansi na uliochapishwa kwa umma kuthibitisha ufanisi duni wa bandari zetu na ubora wa DP World, bali kila kitu kilifanywa kwa siri," alisema.
Uamuzi wa CCM
Julai 9 mwaka huu, Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) ilipokea na kujadili kwa kina taarifa ya makubaliano hayo na kutoka na maazimio kuwa uwekezaji na uendeshaji wa bandari ni kwa manufaa ya uchumi wa nchi. Taarifa ya CCM iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Sophia Mjema ilieleza kikao cha NEC chini ya uenyekiti wa Rais Samia kilikubaliana, Serikali iendelee kutoa elimu kwa wananchi katika jambo hilo.
"Serikali iongeze kasi ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo katika makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji huo wa bandari," alisema Mjema na kuongeza: “Serikali ihakikishe maoni chanya yenye tija, ya wananchi yanasikilizwa.”
…ni mjadala wenye afya
Jana, akizungumzia suala hilo kwenye warsha ya kuwajengea uwezo waandishi na wahariri juu ya masuala ya ukatili wa kijinsia jijini Dar es Salaam, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaru alisema mjadala unaoendelea nchi hivi sasa ni afya kwa Taifa.
Lakini ameonya watu wasiitumie vibaya Ibara ya 18 ya Katiba inayozungumzia uhuru wa kujieleza na kutoa maoni.
"Huu utashi alionao Rais (Samia) wa kutamani kuona watu wakizungumza, wakitoa maoni, usigeuzwe kuwa mapambano ya watu kutukanana na kutweza wengine," alisema Dk Ndumbaro ambaye kitalamu ni mwanasheria
Hata hivyo, alishangaa kuona suala la bandari likijadiliwa kwa jazba na nguvu kama ndiyo mkataba wa kwanza wa aina hiyo kwa nchi kusaini.
"Mbona tumesaini mkataba kama huo kwenye mradi wa bomba la mafuta kutoka Tanga hadi Hoima Uganda na ardhi imetwaliwa kwa ajili ya mradi huo, mbona hatusemi nchi imeuzwa na watu wamelipwa fidia!
"Nadhani kuna haja ya kulijadili hili kwa hekima ili tufikie malengo ya mafanikio tunayoyatamani badala ya kuendelea kutoleana maneno ya kashfa," alisema
Alisema ukisikiliza mjadala mzima, hakuna mtu anayepinga uwekezaji bandari, ila wanalalamikia baadhi ya vifungu wakitaka virekebishwe jambo ambalo Serikali imekubali kuyapokea maoni hayo na itakwenda kufanyia kazi.
Alisema dhamira ya Serikali ya kutaka uwekezaji bandarini ni njema na watu waondoe dhana ya kuwa Rais ameamua kuiuza nchi.
Alisema cha msingi kinachopaswa kufanywa ni kujadili na kuonyesha vifungu vyenye upungufu vifanyiwe kazi na mambo mengine yaendelee.