Msongo wa mawazo, magonjwa yasiyoambukiza vyawatesa Mbeya
Mkurugenzi wa Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH) Dk, Godlove Mbwanji akizungumza kwenye bonanza la familia 2023 lililoandaliwa na watumishi wa Hosptali hiyo. Picha na Hawa Mathias
Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema moja ya changamoto inayosababisha vifo kwa wananchi wa mkoa huo ni msongo wa mawazo, ukosefu wa furaha na magonjwa yasiyo ambukizwa ambayo usababisha gharama kubwa za matibabu.
Homera amesema hayo leo Jumapili Novemba 5, 2023 aliposhiriki bonanza la familia 2023 lililoandaliwa na Watumishi wa Hosptali ya Rufaa Kanda (MZRH) na kufanyika katika viwanja vya Chuo cha Uhasibu (TIA).
Homera amesema kufuatia changamoto hizo ni wakati sasa jamii kuwa na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara sambamba na kufanya mazoezi ili kukabiliana na hali hiyo.
“Niwasihi ndugu zangu kumbukeni kufanya mazoezi kwa afya, kuimarisha kinga za mwili na kuwa na utaratibu wa kupima afya mara kwa mara sambamba na kupunguza msongo wa mawazo kwa kuitafuta furaha wakati wote,”amesema.
Homera amesema inasikitishati watu kupoteza maisha kwa magonjwa yanayozuilika wakati Serikali imefanya mapinduzi katika hosptali ya Rufaa Kanda kwa kuleta mashine ya kisasa ya MRI jambo ambalo litaondoa changamoto kwa wagonjwa kusafirishwa kwenda Jijini Dar es Salaam au Dodoma kupata vipimo.
“ Niwaombe watanzania kuepuka magonjwa yasiyoambukizwa kwa kuwa na utaratibu wa kupima afya na kutumia muda mwingi kufanya mazoezi na elimu ya wataalamu wa afya pindi inapobainika kuwa na matatizo,”amesema Homera.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk Godlove Mbwanji amesema kuwa wamekuwa na utaratibu wa kuhamasisha jamii kubadili milo ya vyakula ili kuepuka magonjwa yasiyo ambukizwa.
“Idadi kubwa ya wagonjwa wanaopokelewa wanasumbuliwa na magonjwa sugu yasiyoambukizwa ambayo yanatibika kwa gharama kubwa jambo ambalo baadhi ya jamii upoteza maisha kwa hofu inayopelekea msongo wa mawazo,”amesema
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi na Mkurugenzi wa Tiba Hospitali ya Rufaa Kanda, Dk Uwesu Mchepange amesema lengo la bonanza la tisa la siku ya familia 2023 ni kuikumbusha jamii umuhimu wa kufanya mazoezi ili kulinda afya.
“Hii ni mipango yetu kwa kila mwaka kuandaa kwa watumishi kushirikiana na wanafamilia, sambamba na jamii yenyewe hivyo ni wakati sasa kuinuka na kuona umuhimu ya kulinda afya kutoathirika na magonjwa ya kuambukizwa”amesema.