Msukuma amshukia Mwambe wa Uwekezaji

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku (Msukuma)

Muktasari:

  • Mbunge wa Geita Vijijini (CCM) Joseph Kasheku (Msukuma) amemshukia Waziri wa zamani wa uwekezaji Geoffrey Mwambe kuwa ni miongoni mwa wenye mawazo potofu.

Dodoma. Mbunge wa Geita Vijijini (CCM) Joseph Kasheku (Msukuma) amemshukia Waziri wa zamani wa uwekezaji Geoffrey Mwambe kuwa ni miongoni mwa wenye mawazo potofu.

Msukuma ametoa kauli hiyo leo Mei 23, 2023 wakati akichangia hotuba ya makadilio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2023/24.

Mwambe alikuwa Waziri wa Uwekezaji nafasi ambayo alidumu kwa muda mfupi kabla ya kutenguliwa, na wakati akitajwa leo, alikuwepo Bungeni.

"Taifa hili ni la wote, wasomi na wasiokuwa wasomi, hatuhitaji mawazo potofu kama huyu Mwambe, kwanza mimi mwenyewe ulinifelisha," amesema Msukuma.

Mbunge huyo amesema Katika suala zima la uwekezaji watu wenye digrii (shahada) wamekuwa ni kikwazo kutokana na alichokiita mchakato na assessment (tathmini).

"Wengine wanaoinga humu lakini walikuwa Mawaziri, mimi huwezi kunipiga swaga maana tulikupa nafasi ukatufelisha, tuachane na mawazo potofu kama huyu Mwambe tuachane nayo," amesema.

Bila kuthibitisha, lakini amesema kuna watu wanatembea ndani Bunge wakishawishi wabunge ili wakatae uwekezaji wa bandari.

Katika hatua nyingine Msukuma amesema licha ya yeye kuwa darasa la saba lakini ni mwaminifu na ana uwezo mkubwa ndiyo maana alitunukiwa shahada ya udaktari wa heshima (PhD) akaomba ashindanishwe na msomi yeyote kwenye luninga.

Kwa mujibu wa Msukuma, huu ni wakati wa kutoa bandari kwa mwekezaji ili biashara ziweze kwenda vizuri kuliko kunajenga reli ya kisasa wakati mabehewa yanacheleweshwa.