Siri wengi kukimbilia shahada za heshima

Kwa mujibu wa wadau wa elimu, shahada za heshima haziombwi wala kununuliwa, bali hutolewa kwa watu kutokana na mchango wa maendeleo walioutoa na athari chanya waliyoiacha katika jamii. Picha na Maktaba


Mjadala wa utitiri wa watu hasa wanasiasa kutunukiwa shahada za heshima umeibuka tena. Safari hii mjadala huo ulianzia bungeni hali iliyomlazimu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kutoa ufafanuzi.

Ufafanuzi wa waziri huyo, ulitokana na swali la mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi aliyetaka kufahamu ni kwa kiasi gani vyuo vinavyotoa shahada hizo vinatambulika katika mamlaka zinazosimamia elimu nchini.

Pia, alitaka kujua vigezo vinavyotumika kutoa shahada hizo kama Serikali inavitambua.

Mbunge huyo aliibua hoja hiyo zikiwa zimepita siku chache tangu mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale maarufu “Babu Tale” alipotunukiwa shahada ya udaktari wa heshima na chuo kikuu kimoja cha Marekani.

Wabunge wengine waliowahi kutunukiwa shahada ya heshima ni mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku, mbunge wa Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood na mbunge wa viti maalumu (CCM), Ritha Kabati.

Kwa Tanzania japo wanasiasa wanaongoza kwa kutunukiwa shahada hizo ambazo wengi huelezwa kuwa wanazinunua, watu wengine wanaopata ‘bahati’ ya kuzitia kibindoni shahada hizo ni viongozi wa dini.

Uchunguzi wa Mwananchi unaonyesha, wakati baadhi ya watu wakisota kwa miaka kadhaa kabla ya kuhitimu, huku wengine wakilazimika kunyoosha mikono kwa sababu mbalimbali ikiwamo ya kutokidhi vigezo, Shahada ya Udaktari (PhD), inaonekana kuwavutia baadhi ya watu wanaopenda wajulikane kama wasomi, hata kama hawajakaa darasani au kufanya utafiti.


Undani wa PhD

Uzamivu au udaktari wa falsafa (PhD), ni ngazi ya juu katika mifumo ya kitaaluma kwa vyuo vikuu nyuma ya uprofesa.

Msomi wa fani za lugha na elimu. Sheikh Khamis Mataka anasema ngazi hiyo ni uthibitisho kuwa mhusika amebobea au kuzama katika fani husika.

‘’Udaktari ni uthibitisho wa wewe kuwa mwanazuoni uliyezama kielimu na kitaaluma katika eneo fulani na ndiyo maana inaitwa Shahada ya Uzamivu yaani uthibitisho wa Uzamivu na kwamba wewe ni mwalimu wa kuwafundisha wanafunzi wa vyuo vikuu,’’ anasema.

Duniani kote shahada ya udaktari wa falsafa hutolewa katika sura tatu, ya kwanza ikiwa ni ile ya mwanafunzi kufanya utafiti chini ya uangalizi wa wasimamizi maalumu wa ndani na nje ya chuo. Baada ya utafiti mhusika hulazimika kuandaa tasnifu au tazmili (dissertation/ thesis).

Aina ya pili inajumuisha tamrini (mazoezi ya darasani), kufanya utafiti na kisha kuandaa tasnifu (course work and dissertation).

Hapa mwanafunzi anatahiniwa darasani kwa alama maalumu na kisha kufanya utafiti ambao pia huwa na alama maalumu. Mchakato wote huhusisha pia wasimamizi/watahini wa ndani na nje ya chuo.

“Ukipata hiyo (shahada ya PhD kwa utaratibu huo), tuna uwezo wa kufuatilia, tunaweza kuhakiki chuo hicho kwa sababu vyuo vyote duniani popote vilipo vinasajiliwa na mamlaka inayohusika katika nchi husika,” alisema Profesa Mkenda bungeni jijini Dodoma.

Aina ya tatu mhusika hakai darasani, hafanyi utafiti wala hajiandikishi kama mwanafunzi. Shahada hii ya heshima, hupewa mtu kutokana na mapendekezo ya mkuu wa chuo na baraza la taaluma maarufu kama ‘senate’.

“Hutolewa kutambua, kuheshimu, kuthamini na kuenzi mchango wa mhusika katika maendeleo na ustawi wa jamii,” anafafanua Dk Mohamed Maguo wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, alipohojiwa na Mwananchi siku za nyuma.

Naye Profesa Mwandosya anasema kuwa shahada ya heshima ya udaktari hutolewa na vyuo vikuu vyenye ithibati kutambua mchango wa mtu katika maendeleo ya taaluma au ya jamii.

“Kawaida, popote pale unapotunukiwa shahada hiyo, huitwi daktari fulani,’’ aliandika Profesa Mwandosya katika ukurasa wake wa twitter Mei 29, 2021.


Utambulisho wa shahada ya heshima

Tofauti na walio wengi wanaotanguliza neno Dk kabla ya majina yao, Profesa Joseph Kironde anaeleza kuwa mtu yeyote aliyetunukiwa shahada ya heshima hapaswi kutanguliza neno Dk kabla ya jina lake kwa kigezo tu cha kutunukiwa.

‘‘ Kwa mfano, mtunukiwa anaweza kuitwa Bw Juma John (Phd Hon Causa), anaeleza Profesa Kironde katika makala aliyoitoa katika jarida la TCU mwaka 2020.

Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, chuo kinachotambulika kinaweza kumpa heshima hiyo yule ambaye chuo kimemchagua kwa utaratibu unaohusika.

Alisema Serikali kupitia Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) huwa inafuatilia uhalali wa chuo kilichomtunuku mtu shahada ya heshima ya udaktari kama imepokea maombi maalumu ya kikazi.

“Kwa watu ambao wanatunukiwa, mahitaji yanapotokea, Serikali kupitia TCU ifanye uhakiki, tuko tayari kufanya uhakiki na kutambua kwamba nani amepata lakini yasipokuja sisi huwa hatuingilii,” alisema.


Utata Phd za heshima

Aina hii ya tatu hata hivyo, imekuwa na utata, hasa kutokana na kutamalaki kwa vyuo visivyo na ithibati ndani ya nchi na hata kimataifa, vinavyotoa shahada za heshima hata kwa watu ambao kwa jicho la kawaida hawana sifa stahiki.

Kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), shahada hii ya heshima inapaswa kutolewa na vyuo vyenye ithibati kutoka tume na kutambuliwa na sheria ya vyuo vikuu.

Kwa vyuo vikuu vya nje, mwongozo ambao mara kwa mara hutolewa na TCU unaeleza kuwa, lazima viwe vinatambulika na kusajiliwa na mamlaka katika nchi husika.

Watu mbalimbali, akiwamo Mwalimu Julius Nyerere wanasifika kwa kuwa na shahada lukuki za PhD za heshima kutoka vyuo vinavyotambulika kimataifa.

Aghalabu hawakuwa wakijita madaktari kama ilivyo ada hivi sasa kwa baadhi ya watu, hususan wanasiasa na viongozi wa dini, wanaosukumwa kufanya hivyo kwa sababu ya kutaka umaarufu na hadhi.

Kwa mujibu wa Sheikh Mataka, ni ujinga uliotopea wa mtu kujipa hadhi asiyokuwa nayo. Anasema: “Maadili ya kitaalamu yameingiliwa na usomi umekuwa ni majigambo zaidi badala ya kazi za kitaalamu na kitaaluma. Ni uzumbukuku.’’

Ni dhahiri kutokana na mjadala uliopo kuhusu yanayoendelea sasa katika vyuo mbalimbali, TCU inapaswa kuvaa kibwebwe katika kudhibiti mifumo, taratibu na vigezo vya utoaji wa shahada za juu nchini, ili kusiwepo na mianya inayoweza kutumiwa na watu wasio na uwezo kusomea ngazi hiyo nyeti katika mfumo wa elimu nchini.

Mbunge wa viti maalumu, Sophia Mwakagenda alisema hakuna anayekataa kwa watu kupata udaktari wa heshima lakini hivi sasa wanashangaa kuibuka kwa vyuo vinavyomilikiwa na watu mbalimbali.

“Tunafahamu hadi kuipata kuna watu wanafika hadi miaka 10, kama pale Chuo Kikuu Huria (OUT). Lakini leo hii anakuja mtu anachukua shahada kwa Dola 2,000 hadi 6,000 (za Marekani) wanatangaza na wanakuja kutuomba. Mheshimiwa Mwakagenda unataka kupata PhD (udaktari) hebu lete Dola 6,000,” alisema.


Sababu wengi kukimbilia PhD ya heshima

Mdau wa elimu, Dk Avemaria Sekamakafu anaeleza kuwa tabia ya kupenda vitu kwa njia ya mkato, ndiyo inayowafanya watu wawe tayari kutoa gharama yoyote ili wapate shahada za heshima.

“Hivi tujiulize kwa nini shahada hizi zinatolewa zaidi kwa wabunge? jibu ni kwamba kwa sababu wana fedha hivyo wanaweza kununua, lakini si kweli kwamba kuna mambo makubwa ambayo wamefanya kwenye jamii kiasi cha kustahili kupata heshima hiyo wanayoitafuta. Ukifuatilia shahada hizi zinatolewa na taasisi zilizo nje ya nchi; hivi kweli kama kuna waliyofanya kwa nini wasipewe na vyuo vya hapa nchini? anahoji.

Anaongeza: “Nitolee mfano Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alipata shahada baada ya kubeba ajenda ya malaria na baadaye tafiti za kisayansi zilivyofanyika ikaonekana namna mchango wake ulivyosaidia kupunguza makali ya ugonjwa huo. Shahada hii ilitolewa na Muhas. Hayati John Magufuli naye alitunukiwa shahada hii kwa namna alivyorudisha rasilimali kama ambavyo UDSM walikaa na kuona Rais Samia Suluhu Hassan anastahili kutokana na mchango wake katila kuliunganisha Taifa na ajenda ya maridhiano. Hawa walistahili kupewa shahada ya heshima na kazi walizofanya zimeonekana wazi na zimechambuliwa na wanataaluma wa vyuo husika.’’

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Faraja Kristomus, anaeleza kuwa kinachosababisha shahada za heshima kutafutwa kwa hali na mali, kunatokana na ugonjwa wa watu kupenda kutanguliza vyeo kwenye majina.

“Tunaona taaluma mbalimbali zimekuwa na hii kitu mfano wahandisi, wahasibu, mawaliki hivyo wengi wanatamani kutanguliza cheo. Mtu akiwa maarufu halafu hana cheo, anahisi kuna kitu amekosa ndio haya tunashuhudia watu wanatafuta title (vyeo).

Bahati mbaya ni kwamba title rahisi kupata na inayonunulika ni PhD ya heshima, huko ndiko wanakokimbilia wengi bila kufahamu kwamba ile title inapaswa kutangulia kwa yule aliyesoma pekee. Mwenye PhD ya heshima hatakiwi kuitanguliza mbele kabla ya jina lake inatakiwa kuwa mwisho,” anasema Dk Kristomus

Akizungumzia hilo mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John, Shadidu Ndossa anasema ongezeko la shahada za heshima inashtusha hasa baada ya kuonekana kuwa kivutio zaidi kwa wanasiasa.

“Shahada ya heshima inatakiwa kutolewa kwa mtu ambaye amefanya kitu kikubwa kwenye jamii na inapaswa kutolewa na chuo kikuu kinachotambulika, lakini hizi shahada za heshima tunazosikia wamepata hawa waheshimiwa hatuna uhakika kama zinatolewa na taasisi zenye sifa.