Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtama yapoteza mapato wakulima wakikimbilia Tandahimba

Madiwani wa Halmshauri ya Mtama wakiwa kwenye kikao cha baraza cha robo ya nne ambapo wamesikitishwa na kitendo cha wakulima wa zao la ufuta kupeleka zao hilo Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara na kusababisha mapato ya Halmshauri ya Mtama kushuka kwa asilimia 50.

Muktasari:

  • Ushuru wa ufuta katika Halmashauri ya Mtama  umeshuka kutoka Sh800 milioni hadi Sh400 milioni kutokana na wakulima kupeleka mazao yao halmashauri ya Tandahimba mkoani Mtwara.

Mtama. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama wameiomba Serikali kuruhusu kuanzishwa kwa vyama vipya vya msingi vya ushirika (AMCOS) katika vijiji mbalimbali ili kudhibiti upotevu wa mapato ya halmashauri unaotokana na wakulima kuuza mazao yao nje ya eneo hilo.

Wamesema baadhi ya wakulima wamekuwa wakipeleka mazao yao, hususan ufuta, katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara kutokana na kutokuwa na imani na baadhi ya vyama vya ushirika vilivyopo Mtama.

Madiwani hao wameeleza kuwa hali hiyo imeanza kuathiri mapato ya halmashauri yanayotokana na mazao ya biashara. Wamesema, pamoja na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kupungua kwa uzalishaji, hatua ya baadhi ya wakulima kuuza mazao nje ya halmashauri imechangia kushuka kwa mapato.

Hoja hizo zilitolewa jana Jumatano, Julai 15, 2026 wakati wa kikao cha robo ya nne cha Baraza la Madiwani kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Diwani wa Kata ya Nahukahuka, Hamza Nguachi amesema wakulima wengi wanapeleka ufuta wao Wilaya ya Tandahimba kutokana na ugumu wa kuanzisha vyama vya msingi vya ushirika katika maeneo yao.

“Hali hii imesababisha Halmashauri yetu kukosa mapato mengi ambayo tungepata kama wakulima wangeuza zao hili hapa Mtama,” amesema Nguachi.

Naye Diwani wa Viti Maalumu kutoka Kata ya Nyangamara, Hadija Seif ameitaka Serikali kutoa elimu kwa wakulima mapema ili hali hiyo isijitokeze pia katika msimu wa mauzo ya zao la korosho.

“Niwaombe wahusika waende mapema kutoa elimu kwa wakulima ili hali hii isijitokeze kwenye zao la korosho, kwa sababu halmashauri yetu inategemea kwa kiasi kikubwa mapato yatokanayo na mazao ya biashara, ikiwemo ufuta na korosho,” amesema Seif.

Taarifa ya utekelezaji wa bajeti inaonyesha kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri ya Mtama ilikadiria kukusanya Sh800 milioni kutokana na ushuru wa zao la ufuta.

Hata hivyo, hadi mwisho wa mwaka wa fedha imekusanya Sh400 milioni pekee, sawa na asilimia 50 ya lengo.

Akijibu hoja za madiwani, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, Anderson Msumba amesema uongozi umepokea maoni kuhusu haja ya kuimarisha usimamizi wa maadili ya watumishi wa vyama vya ushirika.

Amesema pia kuna umuhimu kwa Mrajisi wa Vyama vya Ushirika kutoa elimu kwa madiwani kuhusu vigezo na taratibu za kuanzisha AMCOS, ili wawe mabalozi wa kuelimisha wananchi katika maeneo yao.

“Vyama vya msingi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya mkulima. Ni vyema madiwani wakawa mstari wa mbele kuwaelimisha wakulima kuhusu umuhimu wa kujiunga na vyama hivyo ili wanufaike na soko la uhakika,” amesema Msumba.

Hata hivyo, leo Alhamisi, Julai 16, 2026, Mwananchi imemtafuta Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Lindi kwa simu, Kenneth Shemdoe ili afafanue kuhusu hoja za madiwani hao, lakini hakupatikana baada ya simu yake kuita mara kadhaa bila kupokewa.