Mtandao mpya wa Threads waporomoka

Muktasari:
- Kwa mujibu wa jarida la Forbes linaloangazia masuala ya masoko, teknolojia na mawasiliano, limesema mtandao mpya wa threads umepungua matumizi ya watumiaji wake (Engagement) kwa karibu asilimia 70.
Dar es Salaam. Mtandao mpya wa threads umepungua matumizi ya watumiaji wake (Engagement) kwa karibu asilimia 70, jarida la Forbes limebainisha.
Jarida hilo linaloangazia masuala ya masoko, teknolojia na mawasiliano, limesema
mtandao huo uliozinduliwa Julai 5 mwaka huu ulipata watumiaji milioni 100 ndani ya wiki moja na kuvunja rekodi ya kuwa mtandao uliopata wafuasi wengi zaidi kwa kipindi cha muda mchache.
Lakini hivi sasa mambo si mambo kwenye mtandao huo, ambao awali ulionekana ndio mpinzani wa mtandao wa Twitter unaomilikiwa na tajiri Elon Musk.
Inaelezwa kwa sasa watumiaji wa kila siku wa Threads ni takriban milioni 13 kutoka watumiaji milioni 44 mnamo Julai 7.
Katika watumiaji hao wanatumia wastani wa dakika nne ambapo zimekupungua kutoka dakika 19 katika siku za kuzinduliwa kwa mtandao huo. Hii ni kwa mujibu wa kampuni ya utafiti wa masoko ya Sensor Tower ya nchini Marekani.
Sensor Tower imeeleza kuwa Twitter ina takriban watumiaji milioni 200 kila siku na wastani wa muda unaotumika kila siku ni dakika 30.
Matarajio ya Threads ambao unatajwa kama mpinzani wa Twitter ni kuingiza mapato hadi dola bilioni 8 katika miaka miwili ijayo.
Kampuni ya Meta ambayo inamilikiwa na tajiri Marc Zuckerberg iliweka malengo ya kuwa na watumiaji milioni 200 wanaotumia kila siku, (engagement).
Akinukuliwa na tovuti ya Digital Information World, Zuckerberg ameonekana akizungumzia jinsi mbinu yake ya kufanya Threads ifanye kazi sawa na programu zingine.
Lengo lake ni kufikia idadi ya bilioni moja kwa watumiaji na baada ya hapo, lengo lao ni kubaini namna ya kupata mapato.
Wadau
Watumiaji wa mtandao huu mpya wanasema hakuna jambo jipya ila kilichowapeleka ni kutopitwa na wakati pamoja na aina ya mabadiliko yaliyoletwa na mmiliki wa Twitter.
Amina Rajabu kutoka Temeke Dar es Salaam anasema alijiunga Threads ila alichokigundua ni kuwa hakuna ubunifu kwa maana mambo yaliyopo mitandao mingine ndiyo yaliyopo Threads.
“Nilijiunga baada ya kuona kila mtu anakimbilia huko lakini baadaye nikaamua kuacha baada ya kugundua hakuna mapya,” amesema Amina
Kwa upande wake Krantz Mwantepele Mkurungezi Mtendaji wa Koncept Group, anasema kwa upande wake anaona mtandao huo unaweza kukabiliwa na changamoto za kuvutia watumiaji na kujenga msingi mkubwa wa wafuatiliaji. Kwa kuwa umri wa mtandao unazingatiwa, inaweza kuchukua muda kwa watu kugundua na kuanza kushiriki kikamilifu.
Pia anasema hata uzoefu wa watumiaji ni jambo muhimu ili kuvutia na kudumisha watumiaji anasema kama mtandao huo una matatizo ya kiutendaji, au kutokuwa na kazi vizuri kwenye majukwaa mbalimbali, basi watumiaji wanaweza kuvunjika moyo na kutoendelea kutumia mtandao huo.
“Ubora wa yaliyomo kwenye mtandao wa Threads ni jambo lingine la kuzingatia. Ikiwa yaliyomo hayavutii au hayalingani na mahitaji ya watumiaji, basi engagement inaweza kupungua. Ni muhimu kutoa yaliyomo ya kuvutia na yenye thamani kwa watumiaji ili kuwafanya warudi mara kwa mara.
“Soko la mitandao ya kijamii limejaa ushindani mkubwa. Threads inakabiliwa na ushindani kutoka kwa majukwaa mengine yanayojulikana na yaliyokita mizizi. Kukabiliana na ushindani huu unahitaji mkakati thabiti na kujitahidi kutofautisha na kuonyesha faida za kipekee za kutumia Threads,” anafafanua Mwantepele.
Anamalizia kwa kukumbuka kuwa hali ya engagement inaweza kubadilika na kuboreshwa kwa muda.
Anasema ni muhimu kufanya utafiti na tathmini mara kwa mara ili kugundua changamoto na fursa za kuboresha mtandao na kurejesha au kuongeza engagement.