Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mtanzania aliyeishi Afrika Kusini miaka 22 arejea akisimulia mateso

Ndugu waliofika kumpokea Mtanzania aliyekuwa akiishi Afrika Kusini.

Muktasari:

  • Baada ya miaka 22 Afrika Kusini, Denis Raphael amerejea Tanzania akieleza mateso, mashambulizi dhidi ya wageni na changamoto za kupata haki, huku wahamiaji wengi wakiondoka nchini humo.

Dar es Salaam. Baada ya kuishi Afrika Kusini kwa miaka 22, Denis Raphael, Mtanzania aliyerejea nchini kupitia mpango wa kurejeshwa kwa hiari, amesema mazingira ya sasa kwa wageni nchini humo yamekuwa magumu kutokana na kuongezeka kwa chuki dhidi ya wahamiaji.

Raphael anasema alienda Afrika Kusini kutafuta fursa za maisha, lakini badala ya kupata ustawi aliishia kukumbana na changamoto za usalama, ubaguzi na ugumu wa kupata haki.

Anasema aliingia nchini humo akiwa na kibali cha kuishi Msumbiji na kuanza kujitafutia kipato kupitia vibarua pamoja na biashara ndogo ndogo za kuuza bidhaa mbalimbali.

Hata hivyo, anasema hali ilianza kubadilika mwaka 2021 wakati wa janga la Uviko-19, baada ya baadhi ya wanasiasa kuanza kutoa kauli zilizowahusisha wageni na tatizo la ajira nchini humo.

“Kuanzia hapo mambo yalibadilika. Wageni walianza kushambuliwa, kuporwa na wengine kuuawa. Yalikuwa maisha ya mateso makubwa,” anasema Raphael.

Anasema katika kipindi alichoishi Afrika Kusini alikumbana na mashambulizi mara kadhaa, huku akidai kuwa hata alipojaribu kutafuta msaada kutoka kwa vyombo vya dola hakupata haki aliyotarajia.

Anadai kuwa aliwahi kuvamiwa na askari nyumbani kwake na kuporwa mali zake, lakini kesi aliyofungua baadaye iliondolewa bila kufanyika uchunguzi wa kina.

“Nilifungua kesi baada ya kuvamiwa, lakini baadaye nikaambiwa jalada limeondolewa. Ukiwa mgeni, wakati mwingine unajikuta huna nguvu ya kupata haki,” anasema.

Raphael anasema licha ya kuishi nchini humo kwa zaidi ya miongo miwili, hakuwahi kupata kibali cha kudumu cha makazi na aliendelea kutegemea vibali vya muda.

Anasema licha ya kujenga maisha nchini humo, ikiwa ni pamoja na kuwa na nyumba na kuoa raia wa Afrika Kusini, amelazimika kuacha mali zake zote na kurejea Tanzania mikono mitupu.

“Nimeshindwa kuuza mali zangu. Hakuna chochote nilichoambulia. Nimerejea nyumbani kuanza upya. Nilimwacha mke wangu Afrika Kusini, na hatukubahatika kupata mtoto.

“Ilifika wakati hata wananchi walipotaka kukusaidia, polisi nao walikuwa wanakushambulia. Huwezi kuwa na fikra za kutafuta wateja au kufanya biashara katika mazingira hayo,” anasema.

Anawashauri vijana wanaotamani kwenda Afrika Kusini kutafuta maisha kuwa makini na kutambua changamoto zinazowakabili wageni nchini humo.

“Maisha ya Afrika Kusini si rahisi kama wengi wanavyofikiria. Chuki dhidi ya wageni imekuwa tatizo kubwa na baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakilitumia kama mtaji wa kisiasa,” anasema.

Julai 25, 2026, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana, aliiambia Mwananchi kuwa jumla ya Watanzania 85 wamerejea nchini kwa hiari kupitia mpango ulioratibiwa na ubalozi kwa kushirikiana na mamlaka za Afrika Kusini.

Anasema viongozi wa Watanzania wanaoishi Afrika Kusini walikuwa mstari wa mbele kuwahamasisha na kuwasaidia waliokuwa katika mazingira magumu kurejea nchini.

Kwa upande wake, Rajabu Kiwitu, Mtanzania mwingine aliyerejea nchini, ameishukuru Serikali kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini kwa kusaidia Watanzania waliokuwa katika mazingira magumu kurudi nyumbani.