Mtanzania ateuliwa katika jopo la vijana wa nyuklia duniani
Mtanzania aliyeteuliwa katika jopo la vijana wa nyuklia duniani, Aloyce Kinemo.
Muktasari:
- Impact Team 2050 ilianzishwa mwaka 2021 kama chombo cha ushauri cha vijana chini ya Rosatom kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia na kuongeza ushiriki wa vijana katika maendeleo ya sayansi, elimu na ushirikiano wa kimataifa.
Dar es Salaam. Mtanzania, Aloyce Kinemo amejiunga na jopo jipya la kimataifa la Impact Team 2050, chombo kinachowakutanisha vijana viongozi kutoka nchi mbalimbali ili kuendeleza matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia.
Kinemo ambaye ni mtafiti katika Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), ni mmoja wa vijana 13 waliochaguliwa kutoka mataifa 13 baada ya mchujo ulioshirikisha waombaji 207 kutoka nchi 58 duniani.
Jopo hilo lilianza rasmi kazi zake wakati wa kongamano la kimataifa la vijana kuhusu Nishati ya Nyuklia nchini Urusi, wajumbe wa awamu ya kwanza wamekabidhi rasmi majukumu kwa viongozi wapya.
Akizungumza leo Jumanne, Julai 14, 2026 na wajumbe hao, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nishati ya Nyuklia la Urusi (Rosatom), Alexey Likhachev amewataka kutumia nafasi hiyo kuimarisha ushirikiano wa kimataifa wa vijana na kuongoza mjadala kuhusu mchango wa teknolojia ya nyuklia katika maendeleo endelevu.
"Kila mmoja wenu ameonyesha uwezo wa kuunganisha vijana, kusimamia miradi yenye matokeo na kuleta mabadiliko katika nchi zake. Tunatarajia mtatumia uzoefu huo kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sayansi, elimu na ubunifu," amesema Likhachev.
Kwa mujibu wa Rosatom, katika miezi ijayo wajumbe hao wataandaa mijadala katika nchi zao ili kutathmini sababu zinazowafanya vijana wengi kuchagua taaluma nyingine badala ya sekta ya nishati ya nyuklia, licha ya nafasi yake katika maendeleo ya teknolojia na nishati safi.
Matokeo ya mijadala hiyo yatawasilishwa katika Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP-31), utakaofanyika Antalya, Uturuki.
Wajumbe hao pia watashiriki kuandaa programu ya vijana katika Siku ya Nishati ya Nyuklia na kutembelea Kituo cha Kuzalisha Umeme wa Nyuklia cha Akkuyu.
Mbali na Tanzania, nchi nyingine zilizopata uwakilishi katika jopo hilo ni Bangladesh, Brazil, China, Misri, Ethiopia, Hungary, Indonesia, Kyrgyzstan, Rwanda, Serbia, Afrika Kusini na Uzbekistan.
Impact Team 2050 ilianzishwa mwaka 2021 kama chombo cha ushauri cha vijana chini ya Rosatom kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya amani ya teknolojia ya nyuklia na kuongeza ushiriki wa vijana katika maendeleo ya sayansi, elimu na ushirikiano wa kimataifa. Jopo jipya limeongeza idadi ya nchi zinazowakilishwa kutoka nane hadi 13, hatua inayolenga kupanua ushiriki wa vijana kutoka Afrika, Asia na Ulaya katika ajenda ya kimataifa ya nishati ya nyuklia.