Kenya kuzalisha umeme wa nyukilia
Muktasari:
Imepanga kutumia dola za Marekani bilioni tano ambako ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha nishati hiyo utaanza rasmi mwaka 2024.
Nairobi, Kenya. Serikali ya Kenya imesema itaendelea na mpango wake wa kuhakikisha kwamba ina kiwanda cha kuzaliwa umeme kwa kutumia nguvu za nyuklia ifikapo mwaka 2027.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Umeme wa Nyuklia nchini Kenya, Collins Juma ameuambia mkutano wa wadau kuhusu mpango huo unaoendelea jijini Nairobi leo Alhamisi Septemba 19 kuwa ujezi wa kiwanda cha kuzalisha nishati hiyo unatarajiwa kuanza rasmi mwaka 2024.
Kwa mujibu wa Shirika la habari la BBC, bodi hiyo ilisema kuwa nishati hiyo itatumiwa kuongeza uzalishaji wa umeme nchini humo na si kuchukua nafasi ambayo imekuwa ikitekelezwa na vyanzo vingine.
Inaelezwa kuwa kufikia mwaka 2030, Kenya inatazamiwa kuwa Taifa lenye viwanda na kuwa na pato la wastani hivyo kuhitaji megawati 17,000.
Kwa sasa nchi hiyo inatumia nishati mbadala ikiwamo umeme na maji ambako hutumiwa kuzaliwa megawati 2,400 za umeme.
Kaimu Afisa mkuu mtendaji wa kukinga miali nururishi nchini Kenya, Joseph Maina alisema Wakenya hawafai kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa nishati ya nyuklia.
"Kumekuwa na ajali tatu pekee kubwa za nyuklia katika historia. Kisiwa cha Three Mile Marekani, 1978; Chenorbyl nchini Ukraine, 1986 na Fukushima, Japan mwaka 2011. Usalama umeimarishwa kutokana na mafunzo kutoka kwa mikasa hiyo,” alisisitiza.
Kenya imekuwa na mpango wa kuzalisha nishati ya umeme kwa kutumia nyuklia kwa muda mrefu kama ilivyo nchi ya Uganda. Machi mwaka huu, Waziri wa Nishati na mafuta wa nchi hiyo Charles Keter alisema nchi hiyo itatimiza vigezo vilivyowekwa na Shirika la kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) kabla ya kutekeleza mpango huo.
Afisa huyo alisema tayari upembuzi yakinifu wa mradi huo umeshafanywa na kwamba inakadiriwa nchi hiyo itatumia dola za Kimarekeni bilioni tano kujenga kiwanda cha kuzalisha nishati hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya IAEA ya mwaka 2015, zaidi ya nchi 30 duniani, theluthi moja zikitoka Afrika zinajiandaa kuanzisha mipango ya nyuklia kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa usaidizi wa wataalamu kutoka shirika hilo.
Nishati ya nyuklia ni matumizi ya nishati inayopatikana ndani ya kiini cha atomi. Atomi ni kitu kinachotunza nishati kubwa, wakati muundo wa kiini cha atomi unabadilishwa, sehemu ya nishati hii inapatikana.
Nishati inayotokea hapo inaweza kutumiwa katika mitambo. Inapatikana hasa kwa njia ya joto ambalo kwa kawaida linatumiwa kuchemsha maji yanayozungusha rafadha za kutengenezea umeme.