Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania yaanza kuelekea mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo

Muktasari:

  • Bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2026/27 imepungua kidogo ikilinganishwa na mwaka uliopita, huku utekelezaji wa mageuzi ya elimu, upanuzi wa elimu ya ufundi na stadi, mabadiliko ya kidijitali, utafiti na mtaala mpya unaozingatia umahiri ukihitaji uwekezaji mkubwa Zaidi.

Dar es Salaam. Sekta ya elimu ya juu nchini iko katika hatua muhimu ya kubadili mfumo wa ufadhili, huku Serikali ikianza kutafuta njia mbadala za kugharamia mahitaji yanayoongezeka ya vyuo vikuu na wanafunzi.

Kadri vyuo vikuu vinavyozidi kupanuka, idadi ya wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu kuongezeka na malengo ya Taifa kupitia Dira ya Maendeleo 2050 kutegemea nguvu kazi yenye ujuzi mkubwa, shinikizo kwenye fedha za umma limezidi kuonekana.

Hali hiyo imejitokeza wiki hii baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo kusema Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeanza kuchunguza mifumo mbadala ya ufadhili kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya mikopo.

Akizungumza wakati akifungua kikao cha wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kujadili vipaumbele vya utekelezaji wa mwaka wa fedha 2026/27, Julai 13, 2026, Profesa Nombo amesema fedha za Serikali pekee hazitaweza kuendelea kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya sekta hiyo.

“Serikali imeendelea kuongeza fedha za mikopo ya wanafunzi na mwaka huu tumefikia takribani Sh1 trilioni, lakini Watanzania wanaendelea kuthamini elimu ya juu na mahitaji yanaendelea kuongezeka, hivyo ni muhimu kutambua mifumo mbadala ya ufadhili,” amesema.

Alipongeza hatua ya HESLB kuanza majadiliano kuhusu mifumo mipya ya fedha, akisema sekta nzima ya elimu inapaswa kuanza kuangalia zaidi ya utegemezi wa kawaida wa Hazina.

“Ni muhimu kupunguza mzigo mkubwa unaobebwa na Serikali na kutafuta vyanzo vingine vya fedha. Taasisi nazo zinapaswa kuongeza shughuli za kuzalisha mapato kupitia mipango yao wenyewe,” amesema.

Kauli hiyo imekuja wakati wizara hiyo ikikabiliwa na changamoto ya nafasi finyu ya kifedha.

Ingawa elimu bado ni miongoni mwa sekta zinazopata kipaumbele cha Serikali, bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2026/27 imepungua kidogo ikilinganishwa na mwaka uliopita, huku utekelezaji wa mageuzi ya elimu, upanuzi wa elimu ya ufundi na stadi, mabadiliko ya kidijitali, utafiti na mtaala mpya unaozingatia umahiri ukihitaji uwekezaji mkubwa zaidi.


Mahitaji ya mikopo yaongezeka

Shinikizo la ufadhili linaongezeka kutokana na kasi ya upanuzi wa elimu ya juu nchini mbapo mwaka huu pekee, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imetangaza kuwa vyuo vikuu vina nafasi zaidi ya 170,000 za udahili kutokana na mwaka mwingine wa matokeo mazuri ya mtihani wa kidato cha sita.

Kadri idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu inavyoongezeka, mahitaji ya mikopo nayo yanatarajiwa kupanda zaidi na kuongeza mzigo kwa HESLB.

Kwa miaka mingi, Serikali imekuwa mfadhili mkuu wa elimu ya juu kupitia HESLB ingawa mgao wa fedha umeendelea kuongezeka kila mwaka, wataalamu wanasema ufadhili wa umma pekee hauwezi kukidhi mahitaji ya baadaye, bila ushiriki mkubwa wa sekta binafsi.

Dalili zipo

Benki za NMB na CRDB zimeanzisha bidhaa za ufadhili wa elimu zinazowawezesha wanafunzi na wazazi wanaokidhi vigezo kupata mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya ada na gharama nyingine za masomo.

Ingawa bidhaa hizo kwa sasa zinaongeza nguvu kwenye mikopo ya Serikali badala ya kuchukua nafasi yake, wachambuzi wa elimu wanasema zinaonyesha namna fedha za kibiashara zinavyoweza kusaidia kuziba pengo la ufadhili, hasa kwa wanafunzi wasiopata mikopo ya HESLB na hivyo kushindwa kumudu gharama za elimu ya juu.


Sekta binafsi kushirikishwa

Profesa Nombo amesema mfumo huo wa ushirikiano unapaswa kuenea zaidi katika sekta binafsi.

Aliwataka viongozi wa taasisi zilizo chini ya wizara kuacha kutegemea ruzuku za Serikali pekee na kuanzisha ushirikiano na kampuni kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), akisema karibu asilimia 70 ya fursa za ajira zinatokana na sekta binafsi.

“Tayari tuna mfumo wa PPP. Tusiziache nyaraka hizi kwenye makabati. Kila taasisi ibaini mfumo unaoifaa na kushirikisha sekta binafsi kusaidia elimu,” amesema.

Wito huo hauishii kwenye ufadhili wa wanafunzi pekee, bali unahusisha pia uwekezaji katika miundombinu ya vyuo vikuu, utafiti, ubunifu, mabweni ya wanafunzi, maabara maalumu na miradi ya kibiashara inayoweza kuzalisha mapato endelevu kwa taasisi.

Wataka mfumo mpana

Mtaalamu wa sera za elimu, Dk Thomas Jabir amesema Tanzania inapaswa kubadili mfumo kutoka utegemezi wa Serikali pekee kwenda kwenye mfumo mpana unaohusisha wadau mbalimbali.

“Elimu ya juu inapaswa kuonekana kama uwekezaji wa pamoja wa taifa. Serikali itaendelea kuwa mhimili mkuu, lakini waajiri, taasisi za fedha, viwanda, washirika wa maendeleo, wafadhili na wahitimu wa zamani wote wana nafasi katika kugharamia wahitimu wa baadaye,” amesema.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa elimu, Dk Ibrahimu Mkora amesema maboresho ya mfumo wa ufadhili yanapaswa kuangalia pia suala la ajira kwa wahitimu.

“Waajiri wanaposhiriki kugharamia elimu, wanakuwa sehemu ya uundaji wa mitalaa, mafunzo kwa vitendo na programu za kujenga ujuzi. Hatimaye tunapata wahitimu wenye uwezo unaoendana na mahitaji ya soko la ajira,” amesema.