Mtanzania kusaka rekodi kisiwa cha Greenland

Wilfredy Moshi, akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu (kulia) alipokwenda kumuaga.

Muktasari:

Wilfredy Moshi, mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro anakwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Denmark kwa kushiriki mashindao ya kutembea na kuteleza kwenye barafu katika kisiwa cha Greenland.

Moshi. Kijana mmoja mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, Wilfredy Moshi anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Denmark kwenye mashindao ya kutembea na kuteleza kwenye barafu katika kisiwa cha Greenland, huenda akawa Mtanzania na Mwafrika wa kwanza kufika katika kisiwa hicho.

Asilimia 80 ya kisiwa cha Greenland ambacho ni kikubwa zaidi duniani na chenye watu 56,000, imefunikwa na barafu na kimekuwa ni kivutio kikubwa cha utalii katika nchi hiyo na maeneo mbalimbali duniani.

Mwaka 2012, Moshi ambaye pia ni mdau wa utalii, aliweka rekodi ya kuwa Mtanzania wa kwanza kupanda Mlima Everest, mlima mrefu kuliko yote duniani wenye urefu wa mita 8,848 (futi 29, 029).

Akimuaga Mtanzania huyo leo Aprili 28, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema Serikali inamuunga mkono kwenda kuiwakilisha Tanzania na Mkoa wa Kilimanjaro huko Denmark, huku akimtaka kwenda kuipeperusha vema bendera ya Tanzania na kuleta ushindi mkubwa nyumbani.

“Ujue kwamba unakwenda kuiwakilisha nchi…sisi viongozi wa serikali ya mkoa, tunakutakia kila lenye kheri katika safari yako.Tumefurahi kwamba wewe ni Mtanzania lakini umeamua kuja hapa na haukukurupuka kama wengine wanavyofanya. Tunakutakia heri maana tunajua unakwenda kushindana, tunategemea ulete ushindi mkubwa hapa nyumbani na utakaporudi tukupokee vizuri kwa sababu mwenzetu umetuwakilisha vizuri,” amesema Babu.

Akizungumzia safari hiyo, Moshi amesema itachukua siku 25 hadi 30 kufika katika kisiwa hicho na kwamba anakwenda kushindana na timu za kimataifa na anaamini atashinda na kuleta ushindi nyumbani na kuionyesha dunia kwamba hata Watanzania wana uwezo wa kufika katika kisiwa hicho.

“Nategemea kuondoka kwenda Denmark kujiunga na timu ya kimataifa kwenda kuteleza juu ya barafu kwenye kisiwa cha Greenland ambapo safari hii itachukua siku 25 mpaka 30.

“Ni tukio la kipekee na sio watu wengi wameshafanya, najisikia furaha na fahari kwa kuiwakilisha nchi yangu Tanzania na nitafanya kitu cha kipekee kwa sababu sio watu wengi na sidhani kama kuna watu wa Afrika wameshafanya, kwa hiyo ni tukio la kipekee,” amesema.

Moshi amesema hajawahi kuteleza juu ya barafu na kwamba ni mara yake ya kwanza kwenda katika visiwa hivyo, lakini anaamini ushindi ni wake kwa kuwa amefanya mafunzo nchini Marekani kipindi kilichopita.

“Ninakwenda kuionyesha dunia kwamba hata sisi Watanzania tunaweza kufanya hivyo, nimekuja hapa kwa mkuu wa mkoa kupata baraka zote kwa kuwa yeye ni mwakilishi wa Rais,” amesema Moshi.

Pamoja na mambo mengine, amesema katika shughuli zake za utalii katika Mlima Kilimanjaro, ameweka rekodi ya kupanda mlima huo mara 23, hivyo anaamini huko anakokwenda atafanya vizuri kutokana na uzoefu alionao.