Prime
Binti wa miaka 14 afika kilele Mlima Kilimanjaro

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kivukoni, Rebecca Damian (14) akipokea cheti kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama
Moshi. Rebecca Damian (14), mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kivukoni, ameweka historia kwa kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro tangu kuanza kwa kampeni ya ‘GGM Kili Challenge’ miaka 20 iliyopita.
Mwenzake, Abel Musa (14), mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbugani, aliishia njiani baada ya kuugua malaria akiwa mlimani.
Wanafunzi hao wanatoka mkoani Geita katika kituo cha Moyo wa Huruma kinachofadhiliwa na Kampuni ya GGML inayojihusisha na uchimbaji wa dhahabu.
Kampeni hiyo inalenga kuchangisha fedha kusaidia mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini.
Jana, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Terry Strong amesema binti huyo ameweka historia kwa mara ya kwanza kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro tangu kampeni hiyo ianzishwe mwaka 2002.
"Tuna furaha kwa mafanikio ya watoto hawa, tunaahidi kuendelea kuwasaidia," amesema.
Kutokana na hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama aliagiza naibu katibu mkuu wa wizara hiyo kuhakikisha wanafunzi hao waliopanda mlima kwa siku saba wanaingizwa kwenye orodha ya watu watakaohudhuria Sikukuu ya Mashujaa Julai 25, mwaka huu.
Wawili hao ni miongoni mwa wapanda mlima 61, kati yao 35 ni wapanda mlima na 26 ni waendesha baiskeli. Walishuka mlimani jana kupitia geti la Mweka wilayani Moshi.
Akizungumza baada ya kuwapokea wapanda mlima hao, Waziri Mhagama amesema watoto hao wameonyesha uzalendo kwa Taifa kwa kujitosa kuungana na Watanzania wengine kuchochea nguvu ya mapambano dhidi ya VVU, hivyo wanapaswa kutambuliwa kama mashujaa.
"Naomba niwaalike watoto hawa kama sehemu ya mashujaa kwa namna walivyoonyesha uzalendo wa kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU nchini," amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alisema kampeni hiyo imekuwa chachu ya mafanikio katika mapambano dhidi ya VVU.
Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Strong aliishukuru Serikali jinsi inavyowaunga mkono katika mapambano hayo na kuhakikisha zinapatikana fedha kutokomeza ugonjwa huo.