Mtifuano katazo la watoto shule za bweni

Dar es Salaam. Waraka wa kusitisha huduma ya bweni kwa wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la nne, umeibua mvutano na mgawanyiko kati ya Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco), Serikali na wazazi.

Pande hizo tatu kila moja ina msimamo wake juu ya waraka huo uliotolewa Machi 6 mwaka huu na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Kamishna wa Elimu wa wizara hiyo, Dk Lyabwene Mtahabwa, alibainisha utekelezaji wa waraka huo unatakiwa kuanza Machi Mosi mwaka huu.

Waraka huo ulieleza, shule itakayobainika kukiuka maelekezo itachukuliwa hatua za kinidhamu, kisheria au kufutiwa usajili huku watakaoruhusiwa kutoa huduma za bweni kwa wanafunzi wa awali hadi darasa la nne ni kwa shule zitakazokuwa na kibali maalum.

Agizo hilo lilizitaka shule hizo ziwe zimetekeleza uamuzi huo ifikapo mwisho wa muhula wa kwanza mwaka 2023, hata hivyo wadau walipinga kwa madai ya kutoshirikishwa na wameshafanya uwekezaji mkubwa kwenye shule zao.


Mvutano

Baada ya Waraka kutoka baadhi ya viongozi wa Tamongsco na wadau wengine wa elimu, walifanya kikao na Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda na viongozi wengine waandamizi wa wizara hiyo kujadili suala hilo.

Katika kikao hicho, viongozi wa Tamongsco walisema wanaunga mkono waraka, lakini kuna na sababu kadhaa zinazofanya nyumbani kuonekana ni mahali pasipofaa kulinganisha na shuleni.

Walisema baadhi ya wazazi pia hupata fursa za kusoma nje ya nchi, hivyo huhamishia watoto wao bweni.

“Inatokea mzazi anahamishwa mbali na nyumbani bila kujua anamaliza lini uteuzi wake, ndio maana huacha watoto bweni,” alisema Benjamin Nkonya, mwenyekiti wa jukwaa la sera la Tamongsco.

Baada ya kikao hicho na waziri, viongozi wengine wa Tamongsco wakiongozwa na aliyejitambulisha kama mwenyekiti, Alfred Luvanda walikutana Dar es Salaam, kujadili waraka huo, huku wakiilaumu Serikali kutowashirikisha.

“Leo mtu anaposema funga bweni, hivi unajua kuna fedha imewekezwa? Tutapata hasara ya jumla. Lakini kuna walezi wanaotoa huduma katika mabweni, sasa kwa tangazo la Serikali maana yake hawana kazi.

“Tunakusudia kumwandikia barua Rais Samia ili ajue na atusaidie kwa sababu kufungia mabweni ni ukatili dhidi ya sekta binafsi. Rais Samia aangalie namna kushawishi Bunge na mamlaka za kisheria kuondoa waraka zote kandamizi,” alisema Luvanda katika kikao hicho.

Kwa upande mwingine, Nkonya alisema Serikali imesikiliza hoja na mapendekezo yao huku akisema waraka huo hautafutwa bali kutakuwa na maboresho kupitia kamati itakayoundwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Alisema wamekubaliana na Serikali kuheshimiwa kwa Sheria ya Elimu, ambayo katika kifungu cha sita na saba inaelezea uwepo na Baraza la Taifa la Ushauri wa Elimu na waraka wowote lazima utokane na baraza hilo.

“Tumekubaliana na waziri (Profesa Mkenda), kuundwa kwa kamati itakayomshauri kabla ya kutoa nyaraka. Waraka wowote unaotolewa ushirikishe wadau wa elimu,”alisema Nkonya.


Waitwa Aprili Mosi

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo, amewaandika barua ya mwaliko wadau mbalimbali wa elimu, huku akiitaka kila taasisi kutoa mwakilishi mmoja kwa ajili kushiriki katika kamati ya kuandaa mwongozo itakayoanza utekelezaji wa majukumu Aprili Mosi.

Miongoni mwa walioandikiwa barua hiyo ni Tamongsco, Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata), Baraza la Sunna Tanzania (Basuta), Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet) na Umoja wa Wawekezaji Binafsi katika Elimu (Tapie).

Akizungumza na Mwananchi jana, Philipo Mulugo mdau wa elimu alisema: “Tunataka kupitia kuona namna ya kuurekebisha, kwa jinsi ulivyokaa (waraka) umeegemea upande mmoja na Aprili Mosi tutakutana kuona utekelezaji wa waraka unakuaje kwa sababu kuna upungufu,’’ alisema.

Mmoja wa wazazi, Catherine Msafiri, alisema: “Huu waraka unatuchanganya, mimi nimempeleka mtoto shule kwa sababu ya mazingira, sasa wanaposema tuwachukue inatuvuruga.Unahitajika ushirikishwaji wa kutosha. Serikali inaweza kuwa na nia njema lakini kutoshirikisha wadau ambao ni sisi na wamiliki wa shule, kuna madhara makubwa,’’ alisema.