Prime
Mtifuano wa CCM, Balozi Ali Karume

Unguja. Mambo si shwari ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kutokana na mvutano ulio hadharani kati ya chama hicho na kada wake, Balozi Ali Abeid Karume.
Tayari CCM imetangaza kumfukuza uanachama na kumtaka arejeshe kadi za chama hicho, huku mwenyewe akijinadi kuwa bado ni mwanachama halali.
Kwa miezi kadhaa sasa, Balozi Karume amekuwa kwenye mvutano na chama chake, kutokana na kutoa kauli ambazo zinaonekana kutowafurahisha baadhi ya viongozi ndani ya chama hicho kikongwe nchini.
Hata hivyo, mara kadhaa amekuwa akiweka wazi kuwa kauli zake hazilengi kumdhalilisha mtu wala chama, bali anachotaka kuona ni kuwapo kwa demokrasia ambayo anadai kwa sasa haipo.
Mtifuano mpya
Jana zilisambaa taarifa za chama hicho kumfukuza uanachama kwa sababu za utovu wa maadili, lakini mwenyewe ameweka msimamo akisisitiza yeye bado ni mwanachama halisi wa chama hicho. Pia, alikosoa utaratibu mzima uliotumika kumuondoa akisema ni batili.
Kada huyo ambaye ni mtoto wa mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Aman Karume, amefukuzwa uanachama ikiwa ni takribani siku 23 tu tangu apewe onyo na kuwekwa kwenye kipindi cha uangalizi wa miezi mitatu akitakiwa asifanye kosa.
Balozi Karume alipewa onyo baada ya kutiwa hatiani kwa kutuhumiwa kukidhalilisha chama hicho hadharani na kuukosoa uongozi wa Rais Hussein Mwinyi. Kabla ya kupewa onyo hilo, Balozi Karume aliitwa na kuhojiwa kwenye vikao vya chama kumjadili na kumpa onyo hilo.
Juni 15, mwaka huu kamati ya siasa ya Jimbo la Tunguu ilimuita na kumpa onyo hilo, lakini juzi akizungumza kwenye video alisema chama hicho hakijamuelewa, huku akisisitiza kuwa hakuna demokrasia ndani ya CCM na kudai imeingia madarakani kwa udanganyifu.
Akizungumza na gazeti hili jana baada ya uamuzi huo kutolewa, licha ya mwanadiplomasia huyo kukiri kuitwa na kamati ya siasa ya tawi la Mwera, kamati ya siasa jimbo la Tunguu na kamati ya siasa Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini, alisema hajaitwa kwenye kamati ya mkoa iliyofanya uamuzi huo wa kumfukuza.
“Nasikia tu kikao kimekaa huko kinamjadili mwanachama mpaka kinapitisha uamuzi bila mwenyewe kuitwa. Hilo halikufanyika,” alisema na kuongeza:
“Mimi ni mwanachama mwanzilishi wa CCM Taifa na mpaka leo ni mwanachama wala sina nia ya kutoka CCM, hivyo nasubiri barua inasema nini.
“Sijapokea barua yoyote kunifukuza uanachama, nimeona tu kwenye mitandao na nitazungumza zaidi baada ya kupokea barua hiyo.”
Akisisitiza kuendelea kuwa mwanachama halali, Balozi Karume alisema: “Ikumbukwe sikuwahi kuwa mwanachama wa CCM Mkoa wa Kusini, sio mwanachama wa CCM Zanzibar, mimi ni mwanachama wa CCM Taifa.
“Vile vikao vya jimbo na wilaya sawa, haya ya mkoa sijapata kuyasikia wala sijaandikiwa barua kuitwa huko na utaratibu ninaoujua mwanachama akiwa anajadiliwa kuhusu masuala ya maadili huwa anaitwa. Mifano yake ndio hiyo nimeitwa kwenye jimbo na wilaya na tawi.’’
Alisema licha ya viongozi wa chama hicho kumtuhumu kwamba anakiuka maadili, kutomuita na kumhoji katika ngazi ya mkoa, ni ukiukwaji wa maadili wa chama hicho.
“Hivyo mkoa walikuwa na wao waniite kwa kufuata utaratibu huo huo wa kuniandikia barua ya kunijadili, lakini sijapokea barua, huo peke yake ni ukiukaji wa maadili,” alisema.
Taratibu CCM
Kwa taratibu na kanuni za CCM, ikitokea mwanachama amefukuzwa na hajaridhika na uamuzi huo, anaweza kukata rufani kwenye Kamati Kuu ya chama hicho itakayoketi chini ya Mwenyekiti wake na makamu wake kwa upande wa bara na visiwani.
Kwa sasa, Mwenyekiti ni Rais Samia Suluhu Hassan na makamu wake kwa visiwani na bara ni Rais Hussein Mwinyi na Abdulrahman Kinana mtawalia.
Leo Kamati Kuu ya CCM inatarajiwa kuketi jijini Dodoma, ikiwa ni vikao vya kawaida kwa mujibu wa katiba yake. Kikao hicho kitatanguliwa na kile cha Sekretarieti kilichoketi jana.
CCM yamjibu
Alipotafutwa kuhusu madai ya Balozi Karume, Katibu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Amina Mnacho alisema tayari ameshahojiwa na vikao halali vya chama hicho.
“Kuhojiwa ni kuhojiwa tu, yeye anajua kwamba ameshahojiwa na vikao halali vya chama, hivyo mtu anaweza kuongea tu anavyojisikia,” alisema Amina.
Kuhusu madai ya kada huyo kutopewa barua ya kufukuzwa uanachama alisema: “Taratibu anazijua, kama anaona imechelewa anaweza kufuata....lakini basi atapata barua yake.”
Kuhusu uamuzi wa kumfukuza uanachama kada huyo kutolewa saa 7:00 usiku, Amina alisema kikao kilianza mapema, lakini kwa kuwa kilikuwa na ajenda nyingi, uamuzi ulifanyika baada ya kikao.
Alivyotimuliwa
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa huo, Ali Timamu Haji, alisema uamuzi huo umefikiwa kwa mujibu wa katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022 ibara ya 89 inayoeleza kazi za Halmashauri Kuu ya Mkoa inayoelekeza kuangalia mienendo ya wanachama na viongozi wa CCM wa ngazi ya mkoa na kulazimika kutoa taarifa kwa vikao vinavyohusika ngazi za juu.
Pia ibara ndogo ya 14 kifungu kidogo cha 14 kinaelekeza kumuachisha au kumfukuza uanachama mwanachama yeyote atakayethibitika kwamba tabia na mwenendo wake, vinamuondolea sifa za uanachama wake na mwanachama anayeachishwa au kufukuzwa uanachama, anaweza kukata rufaa kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
"Tumepokea mapendekezo kutoka vikao mbalimbali vya chini na tumevipitia, na sisi kama chama Mkoa kwa mujibu wa katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022 ibara ya 89 (4), Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa inatupa nguvu hiyo.”
Balozi Karume anamiliki kadi ya uanachama wa CCM ya kielektroniki yenye namba C000/2809/993/1 iliyotolewa Machi 17, 2022 pamoja na kadi ya zamani yenye namba CM/078856 iliyotolewa Februari 4, 2019.
Maoni tofauti kufukuzwa kwake
Akizungumza na Mwananchi, mchambuzi wa masuala ya siasa Zanzibar, Ali Makame amesema alitarajia CCM kuchukua uamuzi huo dhidi ya Balozi Karume.
Alisema kada huyo ni mzoefu na masuala ya chama lakini, kwa makusudi ameamua kukosoa chama na viongozi wenzake kwa kutumia utaratibu usiokubalika.
“Balozi Karume ni kiongozi, ila ameamua kukosoa chama na viongozi wenzake hadharani, badala ya kutumia utaratibu wa vikao vya chama. Hapa hakuwa sahihi,” alisema Makame.
Naye mwanasheria, Awadhi Said alisema licha ya Katiba za Muungano na Katiba ya Zanzibar kutoa uhuru wa maoni kwa wananchi, baadhi ya vyama vya siasa vinawadhibiti wanachama wake kutoa maoni wasiyoyapenda.
“Sikatai kwamba vyama ni taasisi, lakini shida inakuja mtu anapotoa maoni yake, viongozi wanamwajibisha kama vile ndio wako juu ya haki za wananchi,” alisema.
Kwa upande wake, Profesa Mohammed Bakari kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliunga mkono hoja hiyo huku akisisitiza athari za kufukuzwa kwake zitategemeana na msukumo wa kundi lililo nyuma yake.
“Kama yuko peke yake hakuna athari za kisiasa, lakini sitegemei kama ataingia upinzani. Pengine kundi litakalokuwa nyuma yake linaweza kuleta madhara ndani ya chama hicho.”
Historia ya Ali Karume
Balozi Mstaafu Ali Abeid Karume alizaliwa Mei 24, 1950 ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Mzee Abeid Amani Karume. Pia pia ni ndugu wa Rais mstaafu wa awamu ya sita wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
Mwaka 2005 na mwaka 2010 alijitosa katika kugombea uteuzi wa chama chake ili apeperushe bendera ya CCM kwa upande wa Muungano wa Tanzania, lakini bahati haikuwa yake.
Akiwa na miaka 28 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri, Wizara ya Biashara na Viwanda katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kazi aliyoishikilia kwa miaka sita (1972 – 1978) alipoomba likizo na kwenda kujiendeleza zaidi kimasomo nchini Marekani.
Alianza kufanya kazi za kibalozi mwaka 1989 alipokuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.
Pia, amewahi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kisha akapelekwa kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi za Ubelgiji, Uholanzi, Luxembourg na Umoja wa Ulaya.