Mtoto afariki gunia likishika moto, kuunguza nyumba

Muktasari:

  • Tukio hilo limetokea Novemba 9 saa 4 usiku baada ya gunia la mkaa uliokuwa umehifadhiwa katika chumba cha watoto kushika moto.

Babati. Mtoto mmoja amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa baada ya mkaa waliokuwa wameuhifadhi kushika moto na kuunguza nyumba walimokuwa wamelala.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Novemba 11, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, ACP George Katabazi amesema kuwa tukio hilo limetokea Novemba 9, 2023 saa nne usiku katika eneo la Magugu iliyoko wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Amemtaja aliyefariki kuwa ni Saidi Mohamed (16) ambaye mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti hospital ya Magugu na aliyejeruhiwa kuwa ni Hamza Mohammed (9) anaendelea na matibabu katika hospital hiyo hiyo.

"Hilo tukio limetokea Novemba 9 saa 4 usiku, ambapo wahusika walikuwa wamelala ndipo gunia la mkaa uliokuwa umehifadhiwa karibu na mlango wa chumba chao kupigwa na upepo na kuanza kushika moto taratibu kabla ya kupokea pazia na nyumba nzima,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, baba mzazi wa watoto hao Mohammed Hamad amesema kuwa siku ya tukio, alitoka jioni kwenye biashara zake na kukuta mkewe amenunua mkaa na kuuhifadhi katika chumba ambacho wanalala wanae kabla ya usiku kusababisha adha hiyo ya kuteketeza mtoto na vitu vya ndani.

“Baada ya kutoka mihangaiko yangu ya biashara nikaingia ndani kula na baada ya hapo watoto wakaaga kwenda kulala katika nyumba yao ya chumba kimoja iliyoko pembeni ya nyumba yetu na mke wangu, lakini saa mbili baadaye nikahisi harufu na moshi na kutoka ndio nikakutana na haya,” amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Magugu, Deogratius Petro amesema kuwa majira ya usiku walisikia kelele za moto na kufika walishirikiana kuvunja mlango ambao ulijaa moshi na kukuta mtoto mdogo Hamza akiwa amelala chini ameishiwa nguvu kwa kelele na moshi ndio wakafanikiwa kumuokoa.

"Baada ya kutazama vizuri ndio tukaona miguu ikiwa uvunguni na baada ya kumvuta ni kaka mtu Saidi akiwa ameungua vibaya na godoro hadi kupoteza muonekano wake ndipo tukawafikisha katika hospital yetu ya Magugu," amesema.

Deogratius alitumia nafasi hiyo kuwahasa wananchi wake kuhifadhi mikaa mbali na wanapolala kwani yamekuwa yakisababisha madhara makubwa katika eneo lake.