Mtoto aliyedaiwa kuuawa hifadhini kwa kupigwa risasi azikwa
Mwili wa Ngatipa Parmao (17) mkazi wa kijiji cha Pangaroo anayedaiwa kuuawa na askari wanyamapori ukiingizwa kaburini.
Muktasari:
Mwili wa Ngatipa Parmao(17), mkazi wa kijiji cha Pangaroo, Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro anayedaiwa kuuawa na askari wa wanyamapori wa hifadhi ya Mkomazi, Wilaya ya Mwanga, mkoani humo Julai 6, 2022 umezikwa leo Jumatatu huku Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Abdallah Mwaipaya akisema wanawashikilia askari watatu kwa tuhuma za tukio hilo.
Mwanga. Mwili wa Ngatipa Parmao (17), mkazi wa kijiji cha Pangaroo, Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro umezikwa leo Jumatatu Julai 11, 2022 huku Jeshi la Polisi mkoani humo likiwashikilia askari wanyamapori watatu kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
Mtoto huyo ambaye ni wa jamii ya kimasai anadaiwa kupigwa risasi Julai 6, 2022 na askari hao kwa madai ya kuingiza mifugo hifadhini ambapo alikimbizwa katika hospitali ya wilaya ya Same na baada ya kuzidiwa alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya kaskazini (KCMC).
Mnamo Julai 8, 2022 alifariki dunia katika Hospitali ya KCMC alikokuwa amelazwa kwa ajili ya matibabu ambapo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu (Postmoterm ) alionekana na matundu katika mkono wake wa kulia pamoja na tumboni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na familia.
Mazishi ya mtoto huyo yamehudhiriwa na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na viongozi wa serikali wakiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo, Abdalah Mwaipaya pamoja na Mbunge wa Mwanga, Joseph Thadayo.
Vilio na simanzi vilitawala katika mazishi hayo baada ya mama mzazi wa mtoto huyo, Paulina Parmao kuzimia huku baadhi ya waombolezaji waliokuwepo wakipiga ukunga.
Akizungumza katika mazishi hayo, mkuu wa Wilaya hiyo, Mwaipaya ameiomba familia kuendelea kuwa wavumilivu wakati jambo hilo likishughulikiwa na vyombo husika ambapo amesema wanaendelea kuwashikilia waliohusika na mauaji hayo.
"Niwape pole familia na tunashukuru kwa uvumilivu ambao mmekuwa nao na sisi serikali tumekuwa pamoja na nyinyi tangu tukio hili limetokea,” amesema
Kwa upande wake, baba mzazi wa Ngatipa, Marius Parmao ameiomba serikali kuhakikisha inatenda haki kwa mauaji ya mwanaye na kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na mauaji ya mtoto wao