Mtoto mchanga afariki dunia ajali iliyoua 14 Tabora
Muktasari:
- Ajali hiyo ilitokea Novemba 7, 2024 saa 2:20 asubuhi katika Kijiji cha Mwasengo, wilayani Nzega, ilisababisha vifo vya watu 14 huku wengine tisa wakijeruhiwa ambapo wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Nkinga.
Tabora. Siku moja baada ya gari dogo la abiria aina ya Hiace kuligonga kwa nyuma lori katika barabara ya Itobo – Bukene, majeruhi mmoja kati ya saba waliokuwa wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Nkinga iliyopo Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, amefariki dunia.
Ajali hiyo iliyotokea jana Novemba 7, 2024 saa 2:20 asubuhi katika Kijiji cha Mwasengo, wilayani humo, ilisababisha vifo vya watu 14 huku wengine tisa wakijeruhiwa na sasa wanapatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 8, 2024 kuhusu hali za majeruhi hao, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Nkinga, Dk Juma Nahonyo amesema walipokea majeruhi saba wakiwa wameumia vibaya sehemu mbalimbali za miili yao.
Dk Juma amesema majeruhi hao waliopokelewa walikuwa wameumia viungo vingi vya ndani hivyo waliingizwa chumba cha upasuaji kwa ajili ya kuokoa maisha yao.
Daktari huyo amethibitisha kutokea kwa kifo cha majeruhi mmoja ambaye ni mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi minane, hivyo kufanya idadi ya waliofariki dunia kwenye ajali hiyo kufikia 15 na majeruhi wakibaki sita hospitalini hapo.
“Miongoni mwa wale majeruhi saba, alikuwepo mtoto mmoja aliyekuwa na mwaka mmoja na miezi kumi, wakati tunampatia matibabu alifariki kutokana na majeraha aliyoyapata ya kuharibika sehemu za viungo vyake vya ndani,” amesema.
Dk Nahonyo amesema majeruhi watatu kati ya saba waliofikishwa katika hospitali hiyo wamefanyiwa upasuaji mkubwa.
“Baada ya kuwapokea majeruhi, hali zao zilikua mbaya na watatu kati yao tuliwaingiza chumba cha upasuaji kwa ajili ya kunusuru hali zao na hadi leo wanaendelea vizuri, lakini bado wapo katika chumba cha uangalizi (ICU),” amesema Dk Nahonyo.
Amesema majeruhi hao walipasuka viungo vingi vya ndani ikiwemo utumbo, kongosho na viungo vingine, jambo linalosababisha madaktari hao kuwaangalia kwa ukaribu.
Awali, Mwananchi lilizungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao kujua kama dereva amekamatwa ambapo amesema: “Tunaendelea kumtafuta dereva wa Hiace aliyekimbia baada ya ajali, tunaomba ushirikiano kwa atakayemuona atupe taarifa ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.”