Mtoto wa miaka sita aliyeuawa kwa kubakwa azikwa

Ibada ya mazishi ya mwanafunzi, Leonila Maleto.

Muktasari:

  • Vilio, simanzi na majonzi vimetawala katika mazikoi ya mwanafunzi, Leonila Maleto (6), aliyeuawa kikatili kwa kubakwa na kulawitiwa na kisha mwili wake kutupwa kwenye korongo.

Moshi. Vilio, simanzi na majonzi vimetawala katika maziko ya mwanafunzi, Leonila Maleto (6), aliyeuawa kikatili kwa kubakwa na kulawitiwa na kisha mwili wake kutupwa kwenye korongo.

Mwanafunzi huyo ambaye alikuwa akisoma Shule ya Msingi Wereni, iliyopo Kata ya Kibosho Magharibi, Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro amezikwa leo Juni 7 kijijini hapo huku mamia ya waombolezaji waliokuwepo katika mazishi hayo wakilaani tukio hilo la kikatili.

Tukio la kuuliwa kwa mwanafunzi huyo ambaye ni mtoto wa pekee katika familia hiyo lilitokea Mei 31, mwaka huu wakati alipokwenda 'tuition' na kutorejea nyumbani ambapo mwili wake ulikutwa kwenye korongo Juni Mosi mwaka huu.

Hata hivyo mamia ya waombolezaji waliokuwepo msibani hapo walijikuta wakitokwa na machozi wakati iliposomwa historia ya marehemu ikieleza namna mwanafunzi huyo alivyoondoka nyumbani kwenda 'tuition' na mpaka alipookotwa kwenye korongo huku mwili wake sehemu ya usoni ukiwa umetafunwa na kaa na kuharibu sehemu ya uso.

Hivyo kutokana na mwili huo kuharibiwa sehemu ya macho, jeneza lililobeba mwili wa marehemu halikufunuliwa hivyo waombolezaji waliaga kwa kuangalia picha ya mtoto huyo iliyokuwa mbele ya jeneza.

Akisoma historia ya marehemu, mmoja wa wanafamilia, Adolf Rumanyika alisema familia imepata pigo kubwa kwa kifo cha kinyama kwa mtoto huyo na kwamba aliyefanya tukio hilo ni kijana wa Kijiji hicho.

"Mei 31 mtoto wetu  alitoka nyumbani kwenye 'tuition' lakini hakufika, ilipofika saa 5:30 jioni mama yake alipomfuata 'tuition' mwalimu alimwambia hakufika siku hiyo, ndipo zilianza juhudi za kumtafuta akishirikiana na wanakijiji wote bila mafanikio na ilipofika kesho yake saa 9:00 asubuhi alikutwa akiwa amefariki,"

Akitoa salama za rambirambi kutoka Jeshi la polisi, Mrakibu wa Polisi, Asia Matauka ambaye ni Mkuu wa dawati la jinsia na watoto mkoani hapa, amesema Kata ya Kibosho imekuwa ni kinara ya matukio ya ukatili, udhalilishaji na unyanyasaji huku akisema chanzo ni viongozi waliopo katika eneo hilo.

"Tukio hili ni  gumu na sio kwenu tuu waombolezaji hata sisi Jeshi la polisi, kuna matukio yanatokea na ukamanda unaweka pembeni,  hapa kila mtu machozi yamemtoka, kitendo alichofanyiwa mtoto huyo kinaumiza, hata mimi pale dawati ninaona matukio ya kinyama, kikatili, vitendo vinavyotendeka sio vya kibinadamu na hapa Kibosho matukio haya yamezidi," amesema na kuongeza;

"Kilimanjaro tumekuwa hatuna hofu ya Mungu tena, unyama, ukatili umetutawala hofu ya Mungu juu yetu hakuna, kiukweli inahuzunisha sana, tunatakiwa kumrudia sana Mungu, jamii sasa hivi haina hofu ya Mungu tena."