Mchimbaji kortini kwa kumpa mimba mwanafunzi

Muktasari:

Mchimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Erick Peter (39) amefikishwa kwenye mahakama ya hakimu mkazi Simanjiro na kusomewa shitaka la kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya sekondari Tanzanite.

Simanjiro. Mchimbaji wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Erick Peter (39) amefikishwa kwenye mahakama ya hakimu mkazi Simanjiro na kusomewa shitaka la kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya sekondari Tanzanite.

Peter amesomewa shitaka hilo na mwendesha mashitaka Mosses Hamilton mbele ya hakimu mkuu wa mahakama hiyo Charles Uiso.

Mwendesha mashtaka huyo amesema katika kesi hiyo namba 102 ya mwaka 2022 kuwa mstakiwa huyo ametenda kosa hilo kwa kumpa mimba mwanafunzi huyo wa kidato cha nne katika tarehe isiyotajwa kwenye mwezi Mei 2022.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo Erick alikana kutenda kosa hilo la kumpa mimba mwanafunzi huyo alipoulizwa mahakamani hapo na hakimu Uiso.

Mshtakiwa huyo aliachiwa kwa dhamana mara baada ya kudhaminiwa na watu wawili ya sh2 milioni kila mmoja.

Hakimu Uiso ameahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 4, 2022 itakapotajwa tena mahakamani hapo, kwani upelelezi wa kesi hiyo bado ujakamilika.

Upande wa upelelezi unapaswa kukamilisha vielelezo ikiwemo taarifa ya daktari na shuleni ili mshtakiwa asomewe maelezo ya awali mahakamani hapo.