Mtwara yapanda miti milioni nne, bajeti yatajwa finyu

Mtwara. Mkoa wa Mtwara umefanikiwa kupanda miti milioni nne kati ya milioni 13.5 ya lengo iliyojiwekea ili kutimiza azma ya serikali ya kupanda miti milioni 1.5 kwa kila Halmashauri nchini kwa mwaka.

Kaimu Katibu Tawala Msaidizi, Nadhifa Zunda amebainisha hayo leo Jumatano Mei 24, 2023 katika kikao kazi cha wataalamu wa misitu mkoani hapa kuwa idadi hiyo ni hadi kufikia mwezi Mei mwaka huu.

"Kiuhalisia kiwango ni kidogo sana kupitia kikao hiki tuweke mikakati ya wazi kabisa ili kufikia na kupitiliza lengo, lazima tuwe wabunifu," amesema Zunda.

Katika jitihada za kupambana na mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na shughuli za kibinadamu serikali ilielekeza kila Halmashauri nchini kupanda miti milioni 1.5 kwa mwaka.

Mwaka uliopita 2022 mkoa huo ulifanikiwa kupanda miti 1.9 milioni.

Ofisa misitu mkoani hapo, Ronald Panga amesema kuwa changamoto kubwa ni kukosekana kwa vitalu vya miche ya miti katika Halmashauri na sasa wameanza mkakati wa kuvianzisha katika taasisi mbali mbali zikiwemo shule.

Mkuu wa kitengo cha Maliasili na Uhifadhi Wilaya ya Tandahimba, Emmanuel John amesema kuwa wamekuwa wakitegemea fedha za Halmashauri kwa ajili ya uhifadhi jambo ambalo linawakwamisha.

"Tumefanya jitihada kadhaa za kutunza mazingira kwa kupambana na changamoto zilizopo lakini ukigusia kuhusu bajeti ya kupanda miti kidogo inakua jambo gumu," amesema Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, Richard Kali.

Mhifadhi kutoka Halmashauri ya Mji wa Nanyamba, Shija Mashambaskari amesema ufinyu wa bajeti ni kikwazo kwa haraka kinahitajika kiasi cha Sh3.75 bilioni ili kuweza kupanda miti milioni 1.5.

Kamanda wa Wakala wa huduma za misitu, TFS Kanda ya kusini, Manyisye Mpokigwa amewataka wataalamu wa uhifadhi za misitu na mazingira mkoani Mtwara kushirikiana ili kutatua changamoto za uhifadhi ili kuifanya Mtwara kuwa ya kijani.