Mufti Zubeir akerwa kesi za uporaji maeneo ya misikiti

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar bin Zubeir

Muktasari:

  • Kesi za uporaji maeneo ya misikiti unaofanywa na jumuiya zinazojitokeza kuwasaidia Waislamu kuboresha maeneo ya kuabudia zimejaa kwenye ofisi ya Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar bin Zubeir kiasi cha kuwa kero kwake.

Bukoba. Kesi za uporaji maeneo ya misikiti unaofanywa na jumuiya zinazojitokeza kuwasaidia Waislamu kuboresha maeneo ya kuabudia zimejaa kwenye ofisi ya Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar bin Zubeir kiasi cha kuwa kero kwake.

Sheikh Zubeir alieleza hayo juzi mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, wakati wa uzinduzi wa Msikiti wa Jamiul Istiqaama uliopo mjini hapa uliojengwa na Jumuiya ya Istiqaama.

Alisema kuna jumuiya nyingi zinazowasaidia wananchi kuendeleza misikiti, hasa iliyochoka kwa kujenga mipya, lakini nyingi huwapora wananchi umiliki wa maeneo hayo.

“Kama kuna jumuiya inastahili kusaidiwa ni Istiqaama, kwani haina tatizo na jamii ya Kiislamu na Watanzania kwa ujumla, tofauti na nyingine ambazo baada ya ujenzi hutaka zipewe hati ya kiwanja au kuweka uongozi. “Kati ya kesi nilizonazo ofisini, kesi za jumuiya kutaka kupora maeneo ya wananchi hasa wa vijijini ndizo zilizojaa ofisini kwangu,” alisema Sheikh Zubeir.

Sheikh huyo alisema Istaqaama imekuwapo nchini kwa miaka 166 tangu mwaka 1856 na imekuwa ikishirikiana na Watanzania kutekeleza miradi ya elimu na afya bila tatizo.

Pamoja na hayo, Mufti aliitumia nafasi hiyo kukemea mauaji na vitendo vya kikatili vinavyoongezeka katika jamii, akisema hali hiyo inatokana na watu kuiasi dini, hivyo akawaomba viongozi wote wa dini kushirikiana kutoa elimu na kukemea vitendo hivyo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Istiqaama Tanzania, Seif Ally Seif alisema hapa nchini wana matawi 21 pamoja na shule 14 na vituo viwili vya afya na wanatarajia kujenga kituo kingine jijini Dodoma na sekondari jijini Dar es Salaam ambako wapo wanachama wao wengi.

“Awali msikiti huu ulikuwa mdogo, hivyo tulilazimika kununua viwanja vingine vinne ili kuwaongezea eneo la kuabudia na kufanya shughuli nyingine za kiimani,” alisema Seif.

Rais Samia aliishukuru jumuiya hiyo kwa kujitoa kuisaidia jamii na kuzitaka jumuiya nyingine kujenga misikiti mizuri.

Msikiti huo una maduka na madrasa huku ukiwa na uwezo wa kuingiza wanaume 1,000 na wanawake 300 kwa wakati mmoja. Hata hivyo, Rais alionya migogoro inayotokea misikitini, akisema mara nyingi husababishwa na mapato yanayotokana na shughuli za kiuchumi zinazofanyika, mfano pango la maduka.

“Serikali inatambua mchango wa Istiqaama, hasa kwenye elimu na afya na ninawapongeza viongozi wote kwa kushirikiana vyema na Serikali. Hapa kuna madrasa saba, naomba zikabidhiwe kwa walimu wenye sifa, ili wafundishe maadili kwa vijana wetu,” alisema Rais Samia.

Pia Rais Samia alipongeza ushirikiano mwema ulipo kati ya Tanzania na Oman yalipo makao makuu ya Istiqaama na akasema ameukubali mwaliko wa mfalme wake kuitembelea nchi hiyo na atafanya hivyo hivi karibuni.

Naibu Balozi wa Oman nchini, Dk Salim Al Harbi alisema Oman imepanga kujenga msikiti mkubwa jijini Dodoma utakaokuwa na kituo cha utafiti wa utamaduni wa dini ya Kiislamu na chuo cha kuwafundisha vijana maadili ya dini.