Mume ahofiwa kufa ziwani, mkewe akesha akimwita kando ya ziwa

Mume ahofiwa kufa ziwani, mkewe akesha akimwita kando ya ziwa

Muktasari:

  • Mwanaume huyo ambaye ni baba wa mtoto mmoja anahofiwa kufikwa na umauti juzi Julai 13 alfajiri baada ya mtumbwi aliyokuwemo na wenzake wawili kupinduka wakati wakitoka kutafuta kuni katika msitu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (Tafiri) Nyegezi jijini hapa

Mwanza. Mkazi wa mtaa wa Sweya kata ya Luchelele jijini Mwanza, Salehe Haruna (42) anahofiwa kufa maji kufuatia mtumbwi waliokuwa wakitumia kupinduka ndani ya ziwa Victoria.

Mwanaume huyo ambaye ni baba wa mtoto mmoja anahofiwa kufikwa na umauti juzi Julai 13 alfajiri baada ya mtumbwi aliyokuwemo na wenzake wawili kupinduka wakati wakitoka kutafuta kuni katika msitu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (Tafiri) Nyegezi jijini hapa.

Juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng'anzi kuzungumzia tukio hilo zimekwama baada ya simu yake kupokelewa na msaidizi wake aliyedai Kamanda huyo yuko kwenye kikao cha ndani na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kitengo cha Usimamizi wa Mialo (BMU) mtaa wa Sweya jijini hapa, Juma Balele amethibitisha tukio hilo kutokea, huku akisema wanaume wawili waliokuwemo katika mtumbwi huo (majina yao halisi hayakutambulika haraka) walinusurika baada ya kuokolewa na wavuvi waliokuwa wakipita katika eneo hilo.

"Marehemu ninamfahamu, nilikuwa naishi naye, siku ya tukio usiku wa kuamkia Jumatano aliamka akasema wanaenda kutafuta kuni kwenye msitu wa TAFIRI, lakini ilipofika asubuhi sikumuona badala yake nilipata taarifa ya wenzake kuokolewa na wavuvi wengine baada ya mtumbwi wao kupinduka na kuzama majini," amesema Balele.

Hata hivyo, amesema awali watu hao hawakusema iwapo walikuwa na Salehe hadi pale walipobanwa ndipo wakakiri kwamba walikuwa naye, ila amezama majini.

“Muda mfupi baada ya kutuambia hivyo walitoroka na kutokomea kusikojulikana. Ndipo alfajiri ya juzi (Jumatano) tukajikusanya hapa kuanza kumtafuta," Balele ameiambia Mwananchi Digital ilipofika katika mwalo huo.

Baba mzazi wa mwanaume huyo, Haruna Salehe ameiomba serikali kuingia kati suala hilo kwa kutoa watalaam na vifaa ikiwemo Boti kwa ajili ya kutafuta na kuopoa mwili wa mtoto wake huyo ambao haujapatikana hadi leo tangu Jumatano Julai 13, 2022 tukio la kuzama kwake lilivyoripotiwa.

Amesema mtoto wake huyo aliyezama ni wa kwanza kuzaliwa kati ya watoto watatu huku akisema alipokea taarifa ya tukio hilo Juzi Jumatano Julai 13 akiwa mkoani Geita jambo lililomlazimu kufunga safari hadi jijini Mwanza kwa ajili ya kutafuta mwili wa mwanaume huyo.

"Hadi muda huu mwili haujapatikana na hii mitumbwi ya Injini haina mafuta ya kutosha kuwafanya wazamiaji hawa wasiyo na ujuzi wa kutosha kuupata mwili huo ndiyo maana imetuwia ugumu hadi sasa hivi ni saa tano hatujaupata mwili wake. Tunaomba serikali ituletee watalaam watusaidie kuupata mwili wake," amesema Mzee Salehe

Mke akesha majini akimuita mmewe

Akizungumza na Mwananchi Digital eneo la Mwaloni, Mke wa mwanaume huyo, Heleno Misoji, amedai kutakiwa kubaki eneo hilo na kukoroga uji kwenye mafiga yasiyo na moto, huku akimwita mumewe, jambo linaloelezwa kuwa atarahisisha mumewe kupatikana.

"Nimekesha hapa leo siku ya pili nikiwa nimekaa na kuweka miguu ndani ya Ziwa. Hii ni imani yetu jamii tunayoishi pembezoni mwa Ziwa Victoria tunaamini kwa kufanya hivyo kama mwili wake umezamia hapa hautaenda mbali," amesema Misoji anayeonekana kuchoka kutokana na kupigwa na baridi kwa siku mbili mfululizo.

Hadi Mwananchi Digital inaondoka katika eneo hilo leo Saa 7 mchana mwili wa mwanaume huyo ulikuwa haujapatikana huku Misoji akiendelea kukoroga uji huo kwenye jiko lisilo na moto kufanikisha upatikanaji wa mwili wa mmewe.