Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mume asimulia jinsi Mchungaji Kantate alivyomuaga

Msaidizi wa Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Mchungaji Israel Moshi, ambaye ni mume wa Mchungaji Kantate Munis, aliyefariki ajalini, akisimulia namna alivyoagana na mkewe asubuhi kabla ya kwenda kwenye huduma. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Ajali hiyo ilitokea jana Agosti 4, 2024, Mchungaji Munis na Mzee wa Usharika, Laban Kweka (50) walifariki dunia wakati wakirejea kutoka kwenye uimbaji katika Usharika wa Gezaulole, Wilaya ya Hai.

Hai. Mungu ameficha siri kubwa katika kifo. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa Kimashuku, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Kantate Munis (42) kufariki dunia kwa ajali, saa chache baada ya kumtaka mumewe ambaye pia ni mchungaji, Israel Moshi kuvaa vazi lake la kichungaji kwenda kutoa huduma.

Mchungaji Munis pamoja na mzee wake wa Ushirika, Laban Kweka (50), walifariki dunia jana Jumapili Agosti 4, 2024 baada ya gari walilokuwa wakisafiria wakitokea kwenye uimbaji Usharika wa Gezaulole wilayani Hai, kugongwa na basi la abiria, wakati akikata kona kuingia kwenye usharika huo ambako ndiko anakoishi.

Akisimulia namna alivyoagana na mkewe asubuhi, Mchungaji Moshi amesema wakati wanajiandaa kwenda kwenye huduma, mkewe alimweleza hajapendezwa na vazi la huduma alilokuwa amevaa (kanzu), hivyo akamtaka alivue, kisha avae vazi lake la huduma.

Ameeleza jambo hilo halikuwa la kawaida kwao kutokea na kwa tafsiri yake, ni kama alikuwa akimuaga na kumkabidhi huduma yake.

"Siku ya Jumapili tumezoea kuamka saa 11 alfajiri, hivyo tuliamka mapema, lakini katika mazingira ambayo sio ya kawaida tulijikuta tunafanya utani zaidi kuliko tulivyozoea kuamka na kuwa 'serious' na kuondoka," amesimulia.

Amesema pamoja na kutaniana walibishana nani atatoka na watoto siku hiyo na mwishoni hawakufikia muafaka, lakini kwa kuwa yeye alikuwa akienda kwenye huduma mbali zaidi alilazimika kumwacha mama na watoto.

"Lakini wakati natoka akaniambia vazi langu la huduma halipendi sana,  angapendelea kuanzia sasa nitumie vazi lake la huduma ambalo lipo ofisini kwake, kwa hiyo alinizuia mpaka akahakikisha nimeondoka na vazi lake la huduma, jambo ambalo sio la kawaida, kwa tafsiri yangu ni kama vile alikuwa ananiaga au kunikabidhi huduma yake," amesema Mchungaji Moshi.

Amesema alipoondoka alikwenda moja kwa moja kanisani alikokuwa anahudumu siku ya jana katika Usharika wa Kiwalaa pamoja na viongozi wa dayosisi waliokuwepo.

"Kwenye saa 12 jioni niliambiwa kuna jambo la dharura limetokea katika familia na nilipaswa nipewe taarifa, ndipo nilipoambiwa mke wangu amepata ajali kubwa na amefariki dunia.

“Nilipewa hadithi ya kilichotokea, kwamba gari lake dogo alikokuwa anaendesha liligongwa na basi la kampuni ya Shabiby wakati anaingia barabara ya kanisani ya kuingia nyumbani ambako ndiko anakohudumu," amesema Moshi.

Amesema kwa sasa anamwomba Mwenyezi Mungu amtie nguvu na afya, ili aweze kukabiliana na wakati mgumu alionao.

"Naamini Mungu ataniwezesha kama alivyowezesha wengine, maana katika kipindi changu cha uchungaji nimeona watu wanafiwa wanaacha watoto wadogo, wake wadogo, waume wadogo, basi na mimi nitajiunga na kundi hili kadri Mungu atakavyonijalia na mimi kwa zamu yangu nipambane. Naamini Mungu atanipa kufika hapo atakapopenda nifike, ili nilee watoto wangu hawa alioniachia," amesema na kuongeza;

"Kaniachia watoto wadogo wanne, hawajaridhika sana wana maswali magumu sana juu ya mama yao kwa sababu wao walibaki wakichezacheza naye wakati nimeondoka nyumbani, lakini kwa akili zao hawakufikiri kwamba ni jambo rahisi kutokea kwamba mama yao angeliitwa mbinguni."

Akizungumzia ajali hiyo, Mkuu wa Jimbo la Hai, Dayosisi ya Kaskazini Mchungaji, Biniel Mallyo amesema kanisa limepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa mchungaji huyo pamoja na mzee wa kanisa wa usharika huo.

"Tumepokea taarifa za msiba wa mchungaji wetu kwa masikitiko makubwa, ni ajali mbaya ambayo pia ilisababisha kifo cha mzee wa kanisa wa usharika huu wa Kimashuku na kujeruhi wengine waliokuwa kwenye gari hilo," amesema.

"Tumepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa hasa ikizingatiwa bado ni mchungaji aliyekuwa anachanua katika huduma na haikutegemewa maana si jambo ambalo ungeweza kufikiria."

Aidha, amesema wanatarajia kufanya maziko Ijumaa ya Agosti 9, 2024 katika Usharika wa Kisamo, Jimbo la Kilimanjaro Kati.

"Jimbo la Hai kwa kushirikiana na Jimbo la Kilimanjaro Kati, tumekaa kuweka utaratibu mzima wa jinsi ya kulazwa kwa mwili wa mtumishi mwenzetu na kwa ratiba tumepanga atazikwa katika Usharika wa Kisamo, Jimbo la Kilimanjaro kati siku ya Ijumaa,” amesema.

Mchungaji Mallyo amemuelezea Mchungaji Munis kuwa alikuwa kiongozi mzuri, aliyejaa upendo na aliyeipenda huduma yake na kuifanya kwa uaminifu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa alisema ajali hiyo ilitokea Jumapili, Agosti 4, 2024 katika eneo la Kimashuku, Kata ya Mnadani, Wilaya ya Hai.

Ajali hiyo ilitokea wakati Mchungaji Munis alipokuwa akikatiza barabara upande wa kulia, ili kuingia kanisani kwake, ndipo alipogongana na basi la abiria.

“Dereva wa basi hilo amekamatwa kwa taratibu za kisheria kwa kosa la uzembe, kwa sababu alijaribu kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari,” amesema kamanda huyo.


Hali za majeruhi

Kwa mujibu wa Mwinjikisti wa Usharika wa Kimashuku, Omben Massawe amesema hali za majeruhi wawili ambao wanalelewa katika kituo cha kulelea watoto yatima usharikani hapo, Irene Miraji (21) na Nancy Lema (20) waliolazwa Hospitali ya Wilaya ya Hai zinaendelea vizuri.

"Hawa majeruhi wawili ambao ni watoto wetu tunawatunza kwenye kituo cha watoto yatima hapa, walipata majeraha na wanaendelea vizuri," amesema.

Mwili wa mchungaji huyo umehifadhiwa Hospitali ya KCMC na mwili wa mzee wa kanisa umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Hai ikisubiri taratibu za maziko.

Mchungaji Kante ameacha mume na watoto wanne, mmoja wa kidato cha kwanza, wawili shule ya msingi na mmoja shule ya awali.