Mume asimulia mkewe, mtoto walivyonusurika kifo

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimpa pole Levina Lutinda (kushoto) na Mwanaye Emmily Victor ambao wamenusurika katika ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea mjini Bukoba, jana. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Muktasari:

Levina Rutinda na mtoto wake, Emil Mwesigwa ni kati ya abiria 24 waliookolewa kwenye ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Bukoba Novemba 6, mwaka huu.


Dar/mikoani. Levina Rutinda na mtoto wake, Emil Mwesigwa ni kati ya abiria 24 waliookolewa kwenye ajali ya ndege ya Precision Air iliyotokea Bukoba Novemba 6, mwaka huu.

Kutokana na hali ya Levina, mwenye ujauzito wa miezi saba kuhitaji utulivu, mumewe, Victor Mwesigwa amesimulia aliyoelezwa na mkewe kuhusu walivyookolewa.

“Baada ya ajali, huku kila abiria akihangaika kujinusuru, mke wangu alijikuta akiwa amesimama wima ndani ya ndege akiwa amemshikilia mtoto mkono wa kushoto na boya la kujiokolea mkono wa kulia,” alisema Victor akinukuu maelezo ya Levina.

Alisema kutokana na abiria kugombania maboya, mtu mwingine alimpokonya mke wake boya, jambo lililomlazimisha kufikiria namna ya kujinusuru yeye na mtoto kutokana na maji kuanza kujaa ndani ya ndege.

“Anasema kwa haraka alimshikilia abiria aliyekuwa jirani yake ambaye tunafanya naye kazi hapa Kagera Sugar (kiwanda cha sukari) na (Levina) alipoona eneo la juu ambalo halijafikiwa na maji alimbeba mtoto na kumweka hapo,” alisimulia Victor na kuongeza:

“Wakati huo, anasema abiria mwingine aliyeonekana Mchina aliyekuwa katika jitihada za kujiokoa, alimwona mtoto Emil akiwa eneo alilowekwa na mama yake na akamchukua akaingia naye ndani ya mitumbwi iliyofika kuokoa abiria, kitendo ambacho Levina hakukiona.

“Mke wangu baada ya kutoka kwenye ndege na kutomuona mtoto pale alipomweka, alianza kupiga kelele za ‘mtoto wangu…mtoto wangu lakini akafanikiwa kuingia kwenye mtumbwi hadi alipofika ufukweni, ndipo akamwona mwanaye aliyeokolewa na Mchina,” alisema Victor.

Mume huyo alisema mkewe alikwenda Dar es Salaam Novemba 4 kuhani msiba wa baba mkwe wa kaka yake na alitakiwa kurejea Novemba 6 na yeye (Victor) tayari alikuwa Bukoba mjini kuwapokea.

“Niliwasiliana naye muda mfupi kabla akinijulisha wanakaribia kutua lakini ghafla alipotea hewani,” alisema.

Alisema akiwa hana hili wala lile, alipokea simu kutoka kwa baba mkwe wake, Theonest Rutinda akimjulisha kuwa kuna ajali ya ndege na kumtaka aende hospitalini kuangalia iwapo familia yake ni kati ya majeruhi waliofikishwa hapo.

“Nilipofika nilikumta mke wangu na mtoto na madaktari walinikabidhi mtoto na blanketi la kumfunika na baada ya muda mfupi alirejea katika hali ya kawaida, ikabidi nimpeleke wodini kumwondolea hofu mama yake,” alisema Victor.

Mtoto tarajiwa

“Kwa hakika mtoto wetu ajaye akizaliwa wa kiume tutampa jina la Mtume Petro aliyemudu kutembea juu ya maji kutokana na muujiza wa yeye, mama na kaka yake kunusurika ndani ya maji,” alisema Victor.

Ndoto ya ndoa yayeyuka

Ukiacha tukio la Victor na familia yake, lipo jingine ambalo limeacha majonzi kwa Winfrida Patric, aliyetarajia kufunga ndoa na Zacharia Mlacha (36) mwakani na ndoto hizo zikayeyushwa na ajali hiyo.

Wawili hao ambao wamekuwa katika mahusiano ya muda mrefu, tayari walikuwa wamepata mtoto mmoja, Alvin mwenye umri wa miaka mitano.

Jana, mwili wa Mlacha aliyekuwa mkuu wa kitengo cha mawasiliano katika Menejimenti na Maendeleo ya Afya (MDH) uliagwa nyumbani kwa wazazi wake, Riverside jijini Dar es Salaam kisha kusafirishwa kwenda Mwanga, Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika leo.

“Kama Mungu angejalia mwakani tungebariki ndoa, lakini Mungu kampenda zaidi, sisi tunapanga vyetu na Mungu hupanga kivyake,” alisema Winfrida.

Katika hatua nyingine, mwili wa Zaituni Mohamed (28) aliyefariki katika ajali hiyo wakati anakwenda kikazi Kagera ulizikwa jana nyumbani kwao eneo la Kwa Idd, Arumeru, Mkoa wa Arusha huku ulinzi ukiwa mkali.

Mazishi ya Zaituni yalitawala usiri na hakuna aliyeeleza marehemu alikuwa akifanya kazi gani na waandishi walipigwa marufuku kupiga picha, kurekodi matukio yaliyokuwa yakiendelea kwenye ibada hiyo na mara kadhaa matangazo yalitolewa kuonya.

Zaituni amezikwa kwa imani za Kikristo katika ibada ya mazishi iliyoongozwa na Mchungaji Loserian Kambei wa Kanisa la The Mountain Hebron Ministry.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Arumeru, James Mchembe aliongoza waombolezaji katika maziko hayo ambayo pia yalihudhuriwa na viongozi wa halmashauri hiyo, kamati ya ulinzi na usalama na ndugu na jamaa wa karibu wa familia.

Mama mzazi wa marehemu, Levina Aloyce alisema msiba wa mtoto wake umemuua, lakini “sina budi kukubali matokeo, Mungu ndiye kanipa na ameamua kumchukua, sina cha kuongea, ninapaswa kumshukuru yeye peke yake.”

Imeandikwa na Peter Saramba (Mwanza), Alodia Dominick (Bukoba), Emmanuel Msabaha (Dar), Janeth Mushi, Happy Lazaro na Tedy Kilanga (Arusha).