Mume atuhumiwa kumuua mkewe Kahama, fedha za ujenzi zatajwa chanzo
Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi.
Muktasari:
- Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia Shukuru Bizire (38) kwa tuhuma za mauaji ya mkewe, Neema John (32).
Kahama. Simanzi imetawala kwa wananchi wa mtaa wa Mwime, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga baada ya Shukuru Bizire (38) kudaiwa kumuua mkewe, Neema John (32).
Shukuru anadaiwa kumpiga na kitu kinachodhaniwa kuwa na ncha kali mkewe sehemu mbalimbali za mwili wake.
Akizungumza leo Jumapili, Julai 5, 2026 na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na linamshikilia Shukuru kwa uchunguzi zaidi na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Kamanda Magomi amesema tukio hilo limetokea Julai 3, saa 10 jioni, baada a Jeshi la Polisi kupokea taarifa Shukuru alikuwa amemfungia ndani mkewe na kuendelea kumpiga kwa muda mrefu.
"Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kwamba kuna mwanaume amemfungia ndani mke wake na anampiga kwa muda mrefu. Askari walifika katika eneo la Mtaa huo, na kumkuta Neema John akiwa ndani ya nyumba akiwa amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake.”
"Jeshi la Polisi tunakemea vikali vitendo hivi vya mauaji vinavyotokana na migogoro ya kifamilia. Hatutasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kutenda uhalifu wa namna hii.”
Tayari mwili wa Neema umeshakabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Akisimulia tukio hilo, mwenyekiti wa mtaa wa Mwime, Stella Bayugile amesema siku ya tukio Neema alikuwa kanisani na baadaye alitoka kwenda nyumbani kwake.
Amedai alipofika alikuta mpangilio wa nyumba tofauti na alivyopanga, ndipo akarudi kanisani na kueleza fedha alizokuwa akitunza ndani hazipo na mumewe hayupo, akaaga anakwenda kufuatilia zilipo fedha hizo kwani ni kwa ajili ya ujenzi.
“Akaenda nyumbani, alivyofika hakumkuta mumewe lakini akaona alivyokuwa ameweka vitu alivyokuwa ameweka vitu haviko sawa, akaangalia pesa haipo, haijulikani ni kiasi gani ila alisema ni kwa ajili ya ujenzi. Akarudi kuaga kanisani.”
“Alivyofika kule kwa mke mwenzie pia hakumkuta mumewe, majirani wakamwambia ametoka ni kama anamsindikiza mke mwenzio anasafiri, akajibanza sehemu kumsubiri. Baada ya muda mume akarudi, akachukua maji akaoge,” amedai.
Marehemu alimfuata mumewe ndani, ndipo walipoanza kuzozana na baada ya muda mfupi Stella alianza kupiga kelele za kuomba msaada, majirani walipojaribu kufungua mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani.
“Baada ya muda kimya kilitawala majirani wakajua wameshapatana, kamanda wa sungusungu walipofika wakagonga akafungua ndipo tukaona damu chini, na alikuwa ameshafariki amefunikwa shuka kitandani.
“Inavyoonekana ni kama alimpiga na kitu chenye ncha kali usoni, lakini kisogoni alikuwa ameumia sana, sasa sijui alimtoboaje kutoka usoni mpaka kisogoni, akawa amemtoboa tena mbavu zote za kulia na kushoto, waliokwenda kuosha wanasema hata utumbo ulikuwa nje.”
“Yaani sijui alimfanyaje na meno ni kama hayakuwemo, ni ukatili mkubwa sana, kina mama tumeumia sana, haielezeki, hata kumfunua watu waage haikuwezekana, yaani amepewa adhabu kubwa kuliko kosa alilofanya kama kumfuata mume ni kosa”amedai.