Museveni akumbuka maamuzi magumu ya Magufuli

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan (kushoto) na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni (kulia) wakizindua Mradi wa Kufua Umeme wa Kikagati – Murongo, Mbarara nchini Uganda

Muktasari:

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amemkumbuka Rais wa awamu ya tano wa Tanzania, Hayati John Magufuli kwa maamuzi yake magumu ambayo yamenufaisha wananchi wake na mataifa ya jirani, huku akiwataka viongozi wengine wa Afrika kumuiga kwa kutoa kipaumbele mambo yanayosaidia wananchi kuliko kuendekeza ukiritimba na siasa.

Mwanza. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amemkumbuka Rais wa awamu ya tano wa Tanzania, Hayati John Magufuli kwa maamuzi yake magumu ambayo yamenufaisha wananchi wake na mataifa ya jirani, huku akiwataka viongozi wengine wa Afrika kumuiga kwa kutoa kipaumbele mambo yanayosaidia wananchi kuliko kuendekeza ukiritimba na siasa.

Rais Museveni ameyasema hayo leo Mei 25, 2023 kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa kufua umeme wa Kikagati - Murongo unaozalisha megawati 14 katika Mto Kagera ukigharimu Dola 56 milioni za Marekani ambao umetekelezwa kwa miaka mitano  (2017 -2022).

Amesema mapendekezo ya mradi huo yaliletwa mwaka 2005 lakini yamechukua muda mrefu kupitishwa mpaka alipokuja Hayati Magufuli ambaye alitoa ruhusa mara moja na kuanza utekelezaji huku, akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha mradi huo unakamilika.

Amesema kukamilika kwa mradi huo ambao umejengwa na kampuni binafsi ya Kikagati Hydro Electric Power kwa ufadhili wa Berkeley Energy ni ishara kuwa nchi hizo zimeanza kutumia ipasavyo rasilimali za nchi zao kujiimarisha kiuchumi na kuwaletea wananchi amendeleo.

“Tangu mwaka 2005 kulikuwa na danadana ni jambo la ajabu matatizo mengi kwenye nchi za Afrika yanasababishwa na mambo kama haya na kupoteza muda kwenye mambo yasiyo ya msingi badala ya kuwaletea maendeleo wananchi wake,”

“Malumbano haya hayakuwa na maana mnakuwa kama watoto wanabishana kwenye mambo yasiyo na maana, tulianza mradi wa kuuza umeme Tanzania wakati wa Mzee Mwinyi (Ali Hassan) na Mkapa (Benjamin Mkapa) kuna tofauti gani na hapa, nafikiri wanasiasa na viongozi wa Afrika wanapaswa kuamka vinginevyo wataamshwa na mahitaji ya wananchi,” amesema na kuongeza

“Namshukuru Magufuli kwa kuharakisha kuanza kutekelezwa kwa mradi huu hakutaka kuchelewesha mambo, pia Samia ameendelea kwa kuhakikisha unakamilika sasa tumeanza kuutumia Mto Kagera katika namna ambayo ulipaswa kutumiwa,”

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema mradi huo unakwenda kuchangia kwenye maendeleo na uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili huku akiahidi kutatua baadhi ya changamoto zinazoukabili mradi huo wa kufua umeme ambao kwa Tanzania utazinufaisha Wilaya za Kyerwa, Karagwe na Misenyi mkoani Kagera.

“Najisikia furaha kuona uhusiano wetu wa muda mrefu unazidi kukua kila siku katika nyanja mbalimbali nishati inayozalishwa hapa itakuza usafirishaji, maji safi, shule bora, mazingira salama ya utoaji elimu, daraja la mawasiliano kati ya mjini na vijijini na kukuza usalama na amani katika maeneo yetu,” amesema Rais Samia