Muswada wa vyama wapingwa kila kona

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa  akizungumza wakati wa kongamano la miaka 70 ya tamko la haki zabinadam nchini lililofanyika jijini Dar es Salaaam jana.Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Baadhi wapendekeza kuanzisha vuguvugu

Dar es Salaam. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema kipo tayari kuvisaidia vyama vya siasa kisheria kupinga muswada wa marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa uliowasilishwa bungeni Novemba.

Msimamo wa LHRC umekuja ikiwa ni siku moja tangu vyama 15 vitoe tamko la kupinga marekebisho hayo.

Akizungumza katika kongamano la haki za binadamu lililofanyika jijini Dar es Salaam jana, mwanasheria wa kituo hicho, Raymond Kanegene alisema wapo tayari kutoa msaada kwa vyama hivyo watakapofuatwa.

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Kanegene alisema marekebisho hayo ni mwendelezo wa sheria mbovu zilizotungwa katika kipindi kifupi ikiwamo Sheria ya Makosa ya mtandao. “Sheria yenyewe ina vifungu 22, marekebisho yapo vifungu 32. Katiba yetu, tamko la haki za binadamu vinaendana na hiyo?” alihoji.

Wakizungumza katika kongamano hilo, baadhi ya wanasiasa akiwamo mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea alisema licha ya tushio la demokrasia, wanapaswa kupiga kelele kwa wingi.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa CUF, Ismail Jussa alisema mapambano ya demokrasia yana historia ndefu Zanzibar na kwamba, hivi sasa itajirudia.

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alishauri mkutano huo upitishe azimio la kuwa na viguvugu la demokrasia litakalohusisha makundi yote ya jamii kudai demokrasia. Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa walisema muswada huo unakiuka katiba.

Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke alisema ni ukweli usiopingika vyama vya siasa vinahitaji kufanya shughuli za kisiasa ili viendelea kuwa hai.

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (Rucu), Profesa Gaudence Mpangala alivipongeza vyama hivyo kwa hatua hiyo, ingawa wamechelewa kutoa msimamo wao kwani muswada huo ulitolewa muda mrefu.