Muuguzi aliyebishana na mtaalamu wa maabara atiwa hatiani

Muuguzi Rose Shirima katika picha iliyotokana na kipande cha video walichokuwa wakibishana  Januari 6, 2023 Halmashauri ya Uyui, Tabora.

Muktasari:

  • Muuguzi Rose Shirima aliyeonekana kwenye kipande cha video kwenye mitandao ya kijamii akibishana na mtaalamu wa maabara, aamuliwa kuwa chini ya uangalizi maalum kwa mwaka mmoja.

Dodoma. Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC) limemtia hatiani Rose Shirima aliyeonekana kwenye video katika mitandao ya kijamii akibishana na mtaalamu wa maabara kuhusu vipimo, kuwa atakuwa chini ya uangalizi wa muuguzi mkuu wa Wilaya ya Uyui, Tabora kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Rose ambaye ni muuguzi mkunga wa Zahanati ya Ishihimulwa, atatakiwa kuwa chini ya uangalizi huo bila kutenda kosa la kinidhamu huku ripoti ya utendaji kazi ikitakiwa kupelekwa kwa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania (TNMC).

Adhabu hiyo ilitolewa jana na Baraza hilo lilipomuita Rose na kumsomea shtaka lake la kushindwa kusimamia viwango vya maadili ya kitaaluma kwa kutamka maneno yasiyo na staha kwa mtaalamu wa maabara na kuiaibisha taaaluma ya uuguzi na kuzua taharuki kwa jamii.

Baada ya kusomewa shataka hilo mbele ya Baraza Rose alikiri kutamka maneno hayo na kuomba msamaha kwa kuahidi kuwa na mahusiano mazuri na wafanyakazi wenzake.

“Nimekubali kuwa nilitumia lugha isiyofaa na naomba mnisamehe viongozi wangu naahidi sitorudia tena na nitakuwa na mahusiano mazuri na wafanyakazi wenzangu,” amesema Rose alipopewa nafasi ya kujitetea.

Hata hivyo Baraza lilimtia hatiani Rose na kumpa adhabu ya kufanya kazi chini ya uangalizi maalum wa muuguzi mkuu wa wilaya ya Uyui, mkoani Tabora.

“Licha ya kuomba msamaha, Baraza limekukuta na hatia ya matumizi mabaya ya lugha ambayo hukupaswa kutamka kwa mtumishi mwenzako, kuanzia sasa utakuwa chini ya uangalizi maalum wa Muuguzi mkuu wa Wilaya ya Uyui, na ripoti za maendeleo yako zitaletwa kwetu.

Hata hivyo kama hujaridhika na maamuzi haya una haki ya kukata rufaa kwa Waziri wa Afya ndani ya miezi mitatu”amesema Profesa Lilian Mselle mwenyekiti wa Baraza hilo.

Januari 6, 2023, watumishi hao, Rose Shirima na James Chuchu ambaye ni mteknolojia wa maabara, walionekana kwenye video wakibishana kuhusu matumizi ya vifaa vya kupimia Malaria (MRDT) vilivyoisha muda wake wa matumizi.

Kutokana na tukio hilo, Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – Tamisemi na Halmashauri ya Uyui, ilianzisha uchunguzi wa tukio na kuwakuta watumishi hao kuwa na makosa ya kinidhamu kazini na baadaye kuwasimamisha kazi.