Wahudumu wa afya waliobishania vipimo wasimamishwa kazi

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Watumishi wawili wa afya walioonekana kwenye video mitandaoni wakibishana kuhusu matumizi ya vifaa vya kupimia Malaria (MRDT) vilivyoisha muda wake wa matumizi wilayani Uyuni Mkoa wa Tabora, wamesimamishwa kazi.

Dar es Salaam. Serikali imewasimamisha kazi watumishi wawili wa afya katika zahanati ya Ishihimulwa iliyopo halmashauri ya Uyui mkoani Tabora baada ya kukutwa na makosa katika kipande cha video kilichowaonyesha wakibishana kuhusu kutoa huduma kwa wagonjwa.

Januari 6, 2023, watumishi hao,Rose Shirima ambaye ni muuguzi mkunga na James Chuchu ambaye ni mteknolojia wa maabara, walionekana kwenye video hiyo wakibishana kuhusu matumizi ya vifaa vya kupimia Malaria (MRDT) vilivyoisha muda wake wa matumizi.

Kutokana na tukio hilo, Serikali kwa maana ya Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – Tamisemi na halmashauri ya Uyui, ilianzisha uchunguzi wa tukio na kuwakuta watumishi hao na makosa ya kinidhamu kazini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 25, 2023, Serikali imewasimamisha kazi watumishi hao kwa makosa tofauti kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2022.

“Mkurugenzi wa halmashauri ya Uyui amewasimamisha kazi Rose Shirima aliyekutwa na tuhuma ya matumizi ya lugha isiyo na staha mahali pa kazi na James Chuchu aliyekutwa na tuhuma ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na kuleta taharuki katika jamii,” inaeleza taarifa hiyo.

Sambamba na hilo, taarifa hiyo inaeleza kwamba Shirima na Chuchu wamefikishwa kwenye mabaraza yao ya kitaaluma kujibu tuhuma walizokutwa nazo.

Katika uchunguzi huo, taarifa hiyo ya pamoja kati ya Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais, Tamisemi inaeleza kwamba wamebaini kuna uhusiano usioridhisha baina ya watumishi, matumizi ya lugha isiyo na staha, usimamizi wa kituo usioridhisha na watumishi wengine wanne wamekutwa na tuhuma za kujibu.

“Mkurugenzi wa halmashauri ya Uyui atachukua hatua za kinidhamu na za kiutumishi  kwa watumishi wengine wawili ambao ni Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ishihimulwa na mratibu wa Huduma za Maabara halmashauri ya Uyui kwa sababu nao walikutwa na tuhuma za kujibu,” inaeleza taarifa,

Vilevile, taarifa hiyo inaeleza kwamba hakuna mgonjwa aliyepimwa Malaria kwa kutumia vitendanishi vilivyokwisha muda wake wa matumizi licha ya uwepo wa vitendanishi vilivyokwisha muda wake wa matumizi tangu Agosti 2022.

Taarifa hiyo inabainisha kwamba kituo hicho kina vitendanishi ambavyo vitaisha muda wake ifikapo Aprili na Desemba 2023.