Wahudumu wa afya waliobishania vipimo wasimamishwa kazi

Muktasari:
- Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mkoa wa Tabora, imewasimamisha kazi watumishi wake wawili katika sekta ya afya kufuatia video iliyosambaa mitandaoni ikiwaonyesha wakibishana kuhusu matumizi ya vitendanishi vilivyokwisha muda wa matumizi.
Tabora. Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Uyui, Dk Kija Maige ametangaza kuwasimamisha kazi watumishi Rose Shirima (muuguzi) na James Chuchu (mtalaamu wa maabara) kufuatia video iliyosambaa mitandaoni ikiwaonyesha wakibishana kuhusu matumizi ya vitendanishi vilivyokwisha muda wa matumizi.
Mkurugenzi huyo amesema wamelazimika kuwasimamisha wahudumu hao ili kupisha uchunguzi kufanyika kwa mujibu wa kanuni 37 ya Kanuni za Utumishi wa Umma ya Mwaka 2003.
Kupitia taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo, Dk Maige amesema msingi wa mabishano hayo ni uamuzi wa mtalaamu huyo wa maabara kukataa kutumia kipimo cha malaria kwa kina mama wajawazito kwa madai kilikuwa kimekwisha muda wake.
Wakati huo huo Chama cha Wanasayansi wa Maabara kimeeleza kusikitishwa na video iliyowaonyesha wahudumu wa afya wakizozana kuhusu matumizi ya vipimo vya malaria vilivyokwisha muda wake, Halmashauri ya Wilaya ya Uyui imewasimamsiha kazi watumishi hao.
Video hiyo iliyoanza kusambaa mitandaoni Januari 6, 2023 imemwonyesha muuguzi wa kike akilazimisha kutumika kwa vipimo hivyo, huku mwanaume anayetajwa kuwa mtaalamu wa maabara akipinga matumizi hayo.
Akizungumza na waandishi habari leo Jumamosi Januari 7, Makamu wa Rais wa chama cha Wanasayansi wa Maabara Tanzania, Joseph Gimbuya amesema kuwa mtaalamu wa maabara alikuwa sahihi kukataa kutumika vitendanishi ambavyo vimetumika muda wake, lakini kulikuwa na ukosefu wa maadili.
Gimbuya ambaye pia ni mtumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Uyui, ameitaja zahanati lilipotokea tukio hilo kuwa ni Ishihimulwa, kata ya Bukumbi.
"Sisi tunalaani kitendo cha kutaka kulazimisha matumizi ya vitendanishi vilivyoisha muda wake kwani sio sahihi," amesema.
Amesema baada ya kukiona kipande hicho, walishangazwa kwani hawakulitarajia kutokea na kubaki wamesikitishwa.
"Tukio hili tulikutana nalo kwenye mitandao ya kijamii kama ninyi na tukishtuka sana kwani sio tukio la kawaida," amesema.
Amesema mara baada ya kuliona tukio hilo jana, walikaa kikao na wanakusudia kuishauri Serikali namna nzuri ya kulifanya jambo hilo lieleweke kwa umma wa Watanzania.
Amebainisha kwamba maabara ni sehemu sahihi kwa matibabu ya mgonjwa kwa kupata majibu sahihi na kujua kiini cha ugonjwa na wala hawafurahii kusikia kulazimisha matumizi yasiyofaa kwa mujibu wa utaratibu na sekta ya Tiba.
Amesema Tanzania ina vitendanishi vya kutosha vya kupima malaria (MRDT) ambavyo havijaisha muda wake vinavyotosheleza mahitaji ya miezi sita.