Aliyelazimisha vifaa vilivyoisha muda kutumika matatani

Muktasari:
- Serikali imesema itatoa taarifa juu ya hatua zilizochukuliwa kuhusu video inayosambaa mtandaoni ikimuonyesha muhudumu wa Afya mkoani Tabora akiwa kwenye majibizano na mwenzake, huku akilazimisha matumizi ya dawa zilizoisha muda wake.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali inalifuatilia tukio la mhudumu wa afya mkoani Tabora aliyekuwa akilazimisha vifaa vilivyoisha muda kutumika kwa wajawazito lililoonekana kupitia video iliyosambaa mtandaoni.
Leo Januari 6, 2023 kupitia mtandao wa Twitter ilisambaa video ikimuonyesha mwanamke ambaye inasadikika ni mtaalamu wa afya, akijibizana na mwanaume ambaye hakuonekana kwenye video hiyo juu ya matumizi ya vifaa vilivyoisha muda wake.
Kulingana na maelezo yaliyoambatana kwenye video hiyo mwanaume anayesikika kupinga matumizi ya vifaa hivyo ni mtaalamu wa maabara huku anayelazimisha vitumike ni muhudumu wa afya.
Katika majibizano hayo ambayo muhudumu huyo wa afya akiwa ameketi (mwanamke) anaonekana akimtolea maneno makali mtaalamu huyo wa maabara (mwanaume) akimwambia ana kiherehere cha kutotaka vifaa hivyo vitumike.
Kupitia video hiyo iliyorekodiwa kwa usiri, majibizano yao yalikuwa kama ifuatavyo:
Mhdumu wa afya: Unampima mtu afya?
Mtaalamu wa maabara: Dawa hizi zimekwisha wakati wake.
Muhudumu wa afya: Mbona una kiherehere sana unataka ufanyakazi bora?
Mtaalamu wa maabara: Zilezile sizitumii zimeisha wakati wake.
Mhudumu wa afya: Tumeambiwa watumie wajawazito.
Mtaalamu wa maabara: Situmiii situmii.
Mhudumu wa afya: Nenda kamwambie ‘in-charge’ usiniambie mimi.
Mtaalamu wa maabara: Nishakuambia wewe kwa sababu ndio unalazimisha muhudumu wa afya, aaah mwanaume gani wewe unakuwa na shobo? Wewe ndio mtaalamu tangu taasisi imeanza nyo-nyo-nyo acha usipime wewe ndio unajua miongozo sana pita hivi!
Mtaalamu wa maabara: Kila mtu atumie taaluma yake vizuri mhudumu wa afya una utaalamu.
Kufuatia video hiyo Waziri Ummy kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema Serikali inafuatilia suala hilo.
“Timu ya Usimamizi Afya ya Mkoa (RHMT) wa Tabora na ya Halmashauri (CHMT) ya wilaya ya Uyui wanafuatia suala hili. Serikali itatoa Taarifa kwa umma juu ya hatua zilizochukuliwa,” ameandika.
Ameendelea kusema kuwa Tanzania ina vitanganishi vya kutosha vya kupima malaria (MRDT) ambavyo havijaisha muda wake vya kutosheleza miezi sita.