TANNA yamtetea nesi aliyerekodiwa akibishana

Muktasari:

Chama cha Taifa cha Wauguzi Tanzania (TANNA) kimetoa taarifa ya video iliyosambaa mitandaoni ikionyesha malumbano kati ya muuguzi na mteknolojia wa maabara katika Zahanati ya Ishilimuya wilayani Uyui Mkoa wa Tabora, kikisema hakukuwa na vitendanishi vilivyoisha muda wake kama ilivyodaiwa.

Dar es Salaam. Takribani wiki moja tangu kusambaa kwa video ya watumishi wawili wa afya wakibishana juu ya matumizi ya vipimo vilivyosadikika kuisha muda wake, Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) kimesema kimebaini kuwepo kwa mgogoro wa muda mrefu baina ya watumishi hao.

Kufuatia video hiyo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema  watafanya uchunguzi.

Kama hiyo haitoshi, Halmashauri ya Wilaya Uyui ilitangaza kuwasimamisha kazi muuguzi huyo aliyetajwa kwa jina la Rose Shirima na mteknolojia wa maabara aliyetajwa kwa jina la James Chuchu waliokuwa wakifanya kazi katika zahanati ya Ishilimuya Kata ya Bukumbi, ili kupisha uchunguzi.

Taarifa iliyotolewa na TANNA leo Januari 12 imesema kabla ya kuanza kurekodiwa kwa video hiyo, kulikuwepo na lugha za matusi zinazodaiwa kutolewa na James Chuchu kwa Rose Shirima hali iliyofanya muuguzi huyo naye kumjibu kwa lugha isiyo na staha bila ya kufahamu kuwa anarekodiwa.

Video hiyo ilimwonyesha Rose Shirima akishinikiza matumizi ya vipimo vya malaria vilivyoelezwa kuisha muda wake, huku Chuchu akipinga kitendo hicho.

“Hakuna vitendanishi vyovyote vilivyoisha muda wake ambavyo vilikuwa vinatumika katika kituo hicho kama ilivyokuwa inaelezwa na mtekinolojia wa maabara, isipokuwa vitendanishi vilivyopo vinakaribia kuisha muda wake yaani bado vina miezi 3 mbele.

“Hivyo alichokuwa anasimamia muuguzi kilikuwa sahihi kwa kufuata utaratibu wa mfumo wa udhibiti bidhaa lakini pia alikuwa akisimamia maamuzi ya kikao chao cha ndani,” imesema taarifa ya TANNA.

Kupitia taarifa hiyo, TANNA imelaani tukio la kurekodiwa kwa mtumishi huyo kwa kile kilichodai ndani yake kuna chembechembe za udhalilishaji wa utu na unyanyasaji wa kijinsia.

“Tunatumia fursa hii kuwakumbusha watumishi wa Afya na pia kuanzisha na kuimarisha kamati za maadili kuanzia ngazi ya kituo.

“Hii itasaidia kutatua matatizo ya kitaaluma katika ngazi ya kituo na kwa wakati, ili kuzuia matukio yanayoweza kutoa taharuki katika jamii lakini pia kulinda heshima ya taaluma zetu,” imebainishwa kwenye taarifa hiyo.

TANNA imesema, kinaungana na Serikali kusisitiza watumishi kufanya kazi kwa uadilifu na weledi kwa kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma na taaluma husika katika kutekeleza majukumu ya kila siku.

TANNA pia imeishauri Serikali kuongeza ajira za kada ya Afya ili kumpunguzia muuguzi kazi zisizomuhusu.

“Mara nyingi wauguzi wamekuwa wakifanya kazi nyingi hata zisizo za taaluma yao ili mradi kuhakikisha wananchi wanapata huduma wanayoitarajia, lakini hali hiyo kwa namna moja ama nyingine inaathiri utendaji wao katika shughuli za uuguzi na ukunga kwa ufanis.”

Pia imeishauri Serikali na taasisi binafsi za afya kuajiri kampuni au watu wataoshughulika na usafi wa vituo hospitali ili muuguzi anapoingia kazini akili yake iwe kwa mgonjwa pekee.