Muuza maji aliwa na mamba ziwani

Baadhi ya vijana katika kijiji cha Busisi Kata ya Busisi wilayani Sengerema mkoani Mwanza wakitafuta mwili wa kijana aliyefahamika kwa jina moja la Charles aliyepotelea kwenye maji katika Ziwa Victoria baada ya kubebwa na mamba.

Muktasari:

  • Muuza maji huyo alikwenda kuteka maji ziwani kwa ajili ya kwenda kuuza kijijini kutokana na kuwapo kwa shida ya maji, hivyo kuitumia changamoto hiyo kama fursa ya kujipatia riziki.

Mwanza. Muuza maji na mkazi wa Kijiji cha Busisi Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza aliyefahamika kwa jina moja la Charles, anadaiwa katoweka ziwani baada ya kupitiwa na mamba alipokuwa akichota maji Ziwa Victoria.

Tukio hilo limetokea jana Aprili 17, 2024 saa 1:30 usiku akiwa anachoya maji ziwani katika eneo hilo lililopo karibu na mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi kwa ajili ya kuuza.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mwanza, Kamila Laban amesema amemwagiza Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Sengerema kufuatilia tukio hilo.

“Hivi tunavyozungumza  Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Sengerema ametoka ofisini kwenda kuzifuatilia hizo taarifa kwa sababu inawezekana hao watu waliopata hiyo tatizo hawajatoa taarifa mahali popote," amesema Kamila.

Wakizungumza leo Aprili 18, 2024, mashuhuda wa tukio hilo waliokuwa wakimtafuta kijana huyo pembezoni mwa ziwa hilo, wamesema alikwenda ziwani kuchota maji kwa lengo la kuuza ndipo alipopitiwa na mamba mkubwa aliye ibuka ghafla.

"Sehemu hii maji ni kero kubwa sana kwa hiyo vijana huwa wanatoka huko juu wanakuja kuchota na kwenda kuuza. Sasa kwa kuwa eneo hili lina uchafu kumekuwa mamba wengi, ndipo kijana huyo alipokuja ameliwa  lakini yote hayo sababu ni shida ya maji,” amesema Mayama Mukizi na kuongeza:

"Kijana huyo mpaka sasa hajapatikana ndio maana tupo hapa wengi tunamtafuta," amesema.

Akiunga mkono hoja hiyo, Relo Peter mkazi wa eneo hilo amesema tangu ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi uanze kumekuwa na ongezeko la mamba wanaohatarisha usalama wa wakazi wa eneo hilo wanaotegemea ziwa kwa maji ya kutumia kila siku.

Naye Joyce Silvester amesema wakazi wa eneo hilo hupata maji ya bomba mara moja kwa wiki au hata mbili hali inayopelekea kwenda kuchota ya  ziwani.

Mwenyekiti Kijiji cha Busisi, Patriki Musa amesema matukio ya namna hiyo yamekuwa yakijirudia, huku juhudi za mamlaka kushughulikia tatizo hilo zikisuasua.

"Hili tukio sio la kwanza, watu wamekuwa wakikamatwa na mamba sana. Tumeshatoa malalamiko kuhusiana na hawa mamba kwa ajili ya kuja kufanyiwa utafiti ili angalau wauwawe.”

“Walikuja viongozi na bunduki lakini ikaonekana waliyokuja nayo haikuwa na uwezo wa kuua mamba, hivyo wakaondoka wakitoa ahadi ya kurudi, lakini hawajarudi tena,” amesema.

Akizungumzia changamoto ya ukosefu wa maji katika eneo hilo, Musa amesema ni kero kubwa.

"Kuna utaratibu uliowekwa wa usukumaji wa maji kutoka ziwani, sasa umeme unapoisha maji hayapandi na utaratibu wa kupata fedha ya kununua umeme ni mrefu.”

"Chanzo chetu cha maji ni kidogo hili tumeshaliongea sana kwenye mamlaka husika wakasema watalifanyia kazi, tunalo tenki la maji ambalo halikidhi mahitaji ya Busisi nzima. Tunaomba mradi wa maji uboreshwe kwa sababu Busisi inazidi kukua ili tuweze kupata maji kwa wingi zaidi," amesema Musa.