Mwanafunzi wa darasa la kwanza aliwa na mamba Sengerema

Mwanafunzi wa darasa la kwanza aliwa na mamba Sengerema

Muktasari:

  • Wananchi  wa Kata ya Maisome wameiomba Serikali kuwachimbia visima ili kuwaepusha na matukio ya kuliwa na mamba yanayogharimu maisha ya watu.

Buchosa. Janeti Mganga (8) aliyekuwa anasoma darasa la kwanza shule ya msingi Busikimbili iliyoko kata ya Maisome, Halmashauri ya Buchosa, wilayani Sengerema mkoani Mwanza  ameuawa na mamba wakati akioga kwenye Ziwa Victoria huku baadhi ya viungo vya mwili wake vikiwa vimenyofolewa na kutafunwa na mamba huyo.
 
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema,  Emmanuel Kipole,  amesema  mwanafunzi huyo alikutwa na tukio hilo wakati alipokua akioga na wanafunzi wenzake katika Ziwa Victoria.

Kipole amewasihi  wazazi wasiwaruhusu  watoto wao kwenda kuogelea ziwani badala yake wateke  maji na kwenda majumbani.


"Nitumie nafasi hii kuwaomba wananchi wajiepushe kuogea ziwani, na wasiwaruhusu watoto wao kwenda kuogea au kuchezea ziwani," alionya Kipole.

 Naye Diwani wa Kata ya Maisome, Dauson Miyaga amechukizwa na visa vya mamba kuendelea kugharimu maisha ya watu na kuzitaka mamlaka husika kuchukuwa hatua juu ya mamba hao.


" Nimelalamika mara kwa mara kwa mamlaka husika lakini hazichukui hatua zozote naomba zitusaidie," amesema Miyaga.


Wakati Ofisa mtendaji  Kijiji cha Busikimbi,  Salimu Magayi amesema wamesikitishwa na kifo hicho na kueleza huenda mwanafunzi huyo pengine angekuwa kiongozi katika siku za usoni.
 Amewaomba wananchi wawe wavumilivu kwani wao wapo kwa ajili ya kusaidia wananchi ikiwemo kutatua kero zilizopo katika jamii.  

Wakati Mwalimu Mkuu  wa Shule ya Msingi Busikimbi, Kosmas  Makoye alithibitisha  tukio la   mwanafunzi kuliwa na mamba.
 "Tumelipokea kwa mshituko mkubwa ila tunaomba serikali yetu itujengee visima vya maji ili kupunguza mlundikano wa watu kwenda kuogea ziwani," amesema Makoye.   

Wiribeti Mangapera, ambaye ni mkazi  wa Kata ya Maisome ameeleza kuwa visa vya mamba kula watu vimekuwa vikiongezeka kila siku na hivi karibuni walimpoteza Raulensia Igayo, ambaye ni  mkazi wa kijiji cha Kisaba ambacho ni kijiji jirani na Busikimbi.