Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Trump asifu majadiliano Doha, Iran ikishikilia meli nyingine Hormuz

Rais wa Marekani, Donald Trump. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Mazungumzo ya upatanishi Doha yamefanyika Jumatano Julai 1, 2026, huku Rais Donald Trump akiyataja kuwa yenye mafanikio, lakini mvutano unabaki mkubwa baada ya Iran kushikilia meli nyingine katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

Dar es Salaam. Sintofahamu ya kidiplomasia inaendelea Mashariki ya Kati huku mazungumzo ya upatanishi ya mjini Doha, Qatar, yakigubikwa na kauli zinazokinzana kutoka Marekani, Iran na Qatar.

Mvutano pia unashuhudiwa baada ya Iran kushikilia meli nyingine katika Mlango wa Bahari wa Hormuz katikati ya mazungumzo yanayodaiwa kuendelea huko Doha.

Rais wa Marekani, Donald Trump, amenukuliwa na DW akisema mazungumzo kati ya wajumbe wa Marekani na Iran yanaendelea vizuri licha ya Tehran na Doha kusisitiza hakuna mazungumzo ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili.

Akizungumza akiwa ndani ya ndege yake mpya aliyopewa zawadi na Qatar mjini North Dakota, jana Jumatano Julai 1, 2026, Trump amedaiwa kusifu mazungumzo hayo akisema yanakwenda vema.

 "Kwa kadiri mambo yalivyo hadi sasa, mchakato wa kuiondolea Iran uwezo wa kuwa na silaha za nyuklia unaendelea vema wamekuwa na vikao vizuri, na tutaona. Tuliwapiga kwelikweli, lakini tunakwenda nao vizuri," amesema.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Doha, wajumbe wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner, wamekutana na Emir Hamad Al-Thani kujadili masuala ya Iran na Lebanon kwa wakati mmoja.

Awali, mazungumzo ya ngazi ya wataalamu yalitarajiwa kufanyika Jumanne, lakini mpango huo ukabadilika na wajumbe wa Iran wakaendelea kukutana na wapatanishi wa Qatar na Pakistan badala ya kukutana ana kwa ana na ujumbe wa Marekani.

Iran imesisitiza ujumbe wake ulifika Doha kwa ajili ya mazungumzo kupitia wapatanishi pekee na si kukutana moja kwa moja na ujumbe wa Marekani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmael Baqaei, amethibitisha kuwasili kwa ujumbe unaoongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Kazem Gharibabadi.

Kwa upande wake, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Majid Al Ansari, amekanusha madai ya kuwepo mazungumzo ya moja kwa moja.

"Wawakilishi wa Marekani wapo hapa sio kwa mazungumzo yao na wa Iran. Bali kukutana na wapatanishi na maofisa wa Qatar. Mazungumzo yanajumuisha suala la Iran na pia suala la Lebanon," amenukuliwa akisema.

Miongoni mwa hoja zinazojadiliwa ni makubaliano ya awali ya kupunguza mvutano wa Mashariki ya Kati, mpango wa kuzuia Iran kuwa na silaha za nyuklia, pamoja na kusitishwa kwa mashambulizi na ukaliaji wa Israel kusini mwa Lebanon.

Wakati juhudi hizo zikiendelea, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameagiza jeshi lake kuharibu miundombinu yote ya kundi la Hezbullah kusini mwa Lebanon.

"Hii ndiyo amri yangu: Musibakishe chochote, na fanyeni hivyo," amesema alipozungumza baada ya kutembelea vikosi vya jeshi lake Julai 30.

Pia, amesisitiza jeshi la Israel halitaondoka katika maeneo lililoyateka nchini Lebanon hadi Hezbullah litakaponyang'anywa silaha, msimamo ambao Iran imekuwa ikiutaja kuwa kikwazo kikubwa katika mazungumzo ya upatanishi.


Iran yadaka meli Hormuz

Wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea, televisheni ya taifa ya Iran imetangaza Jumatano Julai 1, 2026, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi limeishikilia meli nyingine ya mizigo iliyokuwa ikijaribu kupita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz bila kufuata masharti yaliyowekwa na Tehran.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, meli hiyo imelazimishwa kutia nanga baada ya kupita katika eneo ambalo halikuidhinishwa na jeshi la Iran.

"Jeshi la Iran limekuwa likiwaonya mara kwa mara manahodha, wamiliki wa meli na maofisa wa kampuni za meli kote ulimwenguni kwamba njia yoyote isiyokuwa ile iliyoidhinishwa kwenye Ghuba ya Uajemi itamalizikia kwenye hasara isiyolipika," imeonya taarifa ya jeshi.

Iran pia imekumbusha kuwa wiki iliyopita ilizishambulia meli mbili zilizojaribu kuvuka Hormuz bila idhini yake, ikiwemo iliyokuwa imebeba mafuta ghafi kutoka Qatar, hatua inayoendelea kuongeza hofu kuhusu usalama wa njia hiyo muhimu inayopitisha zaidi ya asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia duniani.

 Taarifa kutoka Iran zinaeleza  mazungumzo ya Doha yamesimama kupisha shughuli za mazishi ya Kiongoza mkuu wa Taifa hilo aliyeuawa kwenye shambulizi, Ayatollah Alli Khamenei.

Kwa mujibu wa ratiba rasmi, sala za mazishi na shughuli za kuaga mwili wa Khamenei zitafanyika kati ya Julai 4 na 8 katika miji ya Tehran, Qom na Mashhad. Hafla za kutoa pole pia zitafanyika katika miji ya Baghdad, Kazmin, Karbala na Najaf nchini Iraq.

Inakumbukwa kuwa Ali Khamenei aliuawa katika mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yaliyolenga makazi na ofisi yake, maarufu kama nyumba ya uongozi, lakini hadi sasa bado hajazikwa.