Mvua kubwa kunyesha mikoa minne ikiwamo Dar

Muktasari:

Leo Alhamisi Januari 16, 2020 imetoa utabiri wa hali ya hewa kuanzia kesho Ijumaa unaoonyesha mvua kubwa zinatarajia kunyesha katika mikoa minne ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Pwani inayokwenda sambamba na upepo mkali na mawimbi.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kutokea mvua kubwa kesho Ijumaa Januari 17, 2020 katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara.

Taarifa ya TMA iliyotolewa leo Alhamisi Januari 16, 2020 imesema uwezekano wa kutokea mvua hizo ni wa wastani na zinaweza kuambatana na athari.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo athari  zinazoweza kujitokeza ni makazi yaliyo maeneo ya mabondeni  kuzungukwa na maji, ucheleweshwaji wa usafiri na kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Sanjari na mvua angalizo la upepo mkali na mawimbi makubwa limetolewa pia katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Pwani ya bahari ya Hindi na ukanda wa Pwani.

Upepo huo unatarajiwa kutokea kuanzia Jumamosi ya Januari 18 hadi Januari 21, 2020 hivyo watumiaji wa vyombo vya baharini wametakiwa pia kuchukua tahadhari.