Mvua yakata mawasiliano Rungwe, barabara yafunikwa kwa udongo

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu amethibitisha kutokea kwa maafa hayo leo Jumanne Aprili 16, 2024

Mbeya. Mvua kubwa zilizonyesha Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya zimesababisha mmonyoko wa udongo na kukata mawasiliano ya barabara inayounganisha vijiji vya Kapugi na Ilenje kwenda Ikuti, hali iliyoleta adha kwa watumiaji.

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Jaffar Haniu amethibitisha kutokea kwa maafa hayo leo Jumanne Aprili 16, 2024.

“Barabara ya Kapugi - Lyenje kwenye Kijiji cha Ikuti kupitia Mto Kiwira ndiyo imekata mawasiliano baada ya mmomonyoko wa udongo kudondokea na kuleta adha kwa wananchi kutokana na kuwa kiungo muhimu,” amesema.

Haniu amesema tayari amefika eneo la tukio na kuona madhara yaliyojitokeza na wamewasiliana na watendaji wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kuharakisha kurejesha mawasiliano.

Amesema kwa sasa wametoa elimu kwa jamii kuchukua tahadhari hususan kwa watoto kufuatia kuwepo kwa mvua nyingi zinazoleta madhara makubwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Haniu amewataka wananchi wa kata za Ikuti na Malindo kusitisha wanatumia barabara ya Tukuyu – Kapugi – Ikuti na badala yake wapite ya Kyimo – Iponjola – Ikuti kwa ajili usafirishaji wa watu na mali zao.

“Tunashukuru Mungu hakuna madhara yaliyojitokeza zaidi ya barabara na mashamba kumegwa na kujaza matope na miamba katika Mto Kiwira,” amesema.

Mkulima wa Kijiji cha Ikuti, Isabela Kalebela amesema wamepata changamoto kubwa sana namna ya kusafirisha mazao kwa kuwa hakuna gari wala bodaboda linaloweza kuvuka.

“Tuombe Serikali iharakishe kufanya jitihada za kutengeneza barabara hii tegemezi na kiungo kwa shughuli za kiuchumi huku akieleza tupitia vipindi vigumu,” amesema.

Mbali na tukio hilo, waathirika katika Kata ya Katumba Songwe wilayani Kyela wamelazimika kukimbia makazi yao kufuatia maji ya mafuriko kuendelea kuzingira tangu Aprili 3, 2024.

Akizungumza na Mwananchi leo, Mkazi wa Kijiji cha Ndwanga, Ramadhani Mwakalebela amesema hali ni mbaya, kikubwa wanaomba msaada wa chakula, maturubai na miti ili kupiga makambi ya muda mfupi katika maeneo ya milimani pembezoni ya Ziwa Nyasa.

“Kwa kweli hali ni mbaya, tunahitaji chakula, malazi. Mbunge wetu, Ally Mlaghila katusaidia chakula na Sh500,000 kwa ajili ya kuchonga mtumbwi wa kusafirisha watoto kwenda shuleni,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi mbunge wa Kyela, Ally Mlaghila amesema kimsingi hali ni mbaya kuna mahitaji makubwa ikiwamo chakula, mablanketi na magodoro.

“Uwezekano wa njaa ni mkubwa, baadhi ya vijiji mpunga, mihogo, kokoa, migomba imesombwa na kufukiwa na tope, hivyo kwa sasa wananchi wameanza kuchukua tahadhari  huku wakiwa wamepata hasara kubwa kwa mazao ya chakula na biashara waliyozalisha na kumezwa na maji ya mafuriko,” amesema Mlaghila.

Katika hatua nyingine, amesema wanasubiri busara za Serikali kwa kuwa tayari kamati ya maafa imefika kujionea na kufanya tathimini, sasa wanasubiri majibu.