Mvua yakata mawasiliano ya barabara Ileje-Rungwe

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

 Mawasiliano ya Wilaya za Ileje na Rungwe yamefungwa saa 12 baada ya gema la udongo kuporomoka na kuziba barabara

Songwe. Mvua iliyonyesha kwa zaidi ya saa 10 Mkoa wa Songwe imesababisha barabara inayoungaisha wilaya za Ileje mkoani humo na Rungwe Mkoa wa Mbeya kukatika na kuleta adha kwa watumiaji.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumanne Aprili 2, 2024 eneo la tukio hilo Kata ya Luswisi wilayani Ileje, wananchi wamesema wameshindwa kusafirisha ndizi kutokana na barabara kuharibiwa na mvua iliyonyesha Aprili mosi, 2024.

Mmoja wa watumiaji wa barabara hiyo, Anna Mwashiuya amesema shughuli za uchumi zimesimama kwa muda baada ya barabara kufungwa kutokana na kumeguka kwa magema ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa kunyesha.

"Tunaiomba Serikali itusaidie kufungua barabara hii ambayo ni muhimu kiuchumi kwa kusafirisha ndizi kupeleka mkoani Mbeya kwa kuwa, ndiyo njia kuu tunayoitegemea kujiingizia kipato," amesema Mwashiuya.

Zawadi Kabuje ambaye ni katibu wa mbunge  wa Ileje Godfrey Kasekenya, amefika eneo la tukio na kutoa taarifa kwa mbunge huyo ambaye ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Songwe kufungua barabara hiyo.

Meneja wa Tanroads Songwe, Mhandisi Suleimani Bishanga amesema tayari timu ya wataalamu wamefika eneo la tukio kwa ajili ya kufungua njia hiyo ambayo imekata mawasiliano iliyosababishwa na kuporomoka kwa magema ya udogo.

Bishanga amesema barabara hiyo kila msimu wa mvua imekuwa na changamoto ya kuporomoka kwa magema, kwa sasa wamefanikiwa kupunguza kona kali zilizokuwa zinasababisha kuziba kwa barabara msimu wa mvua.