Mvua yaleta maafa Kigoma, nyumba 60 zazingirwa maji
Muktasari:
- Waathirika waiomba Serikali iwasaidie mahala pa kuishi, sasa waomba hifadhi kwa ndugu na majirani.
Kigoma. Nyumba 60 za makazi ya watu na barabara ya Katubuka kwenda Uwanja wa Ndege katika Kata ya Katubuka, Manispaa ya Kigoma Ujiji zimezingirwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Pia mvua hiyo imeathiri maduka na biashara katika eneo hilo, zikiwamo bucha.
Wakizungumzia madhara waliyopata leo Februari 5, 2024 baadhi ya wananchi wamesema maji yameingia ndani ya nyumba zao, hivyo wamepoteza kila kitu kilichokuwamo, kulazimika kwenda kuishi kwa ndugu na majirani.
Mary Wilson, amesema hakuweza kuokoa kitu chochote, hivyo imemlazimu kuondoka na familia yake kwenda kwa ndugu kuishi kwa muda akiangalia utaratibu mwingine.
“Tunaomba Serikali itusaidie pa kuishi kwa sasa, tumehamia kwa majirani na ndugu na hatuwezi kukaa huko siku zote, tunajiweka kwa muda baadaye tutafute pa kuenda,” amesema.
Samson Kechegwa, amesema changamoto ya maji kujaa imesababishwa na miundombinu mibovu ya barabara, madaraja na mifereji ya maji kutokana na eneo hilo kuwa uwanda wa chini ambako maji yanaelekea.
Ameziomba mamlaka husika kufika eneo hilo, ili kurekebisha mifereji kuruhusu maji kutoka.
"Nimejenga hapa mwaka 2010 kwa kutumia pesa za pensheni baada ya kustaafu, sijawahi kuona maji mengi kiasi hiki, ni kweli mvua ni nyingi lakini miondombinu si rafiki. Barabara ipo chini, hivyo ni muhimu waje kuangalia upya na kuweka mifereji ambayo itaelekeza maji kwenda ziwani na si kwenye makazi ya watu,” amesema Kechegwe.
Mfanyabiashara wa bucha ya nyama, Harrison Kinoni amesema eneo hilo limetengwa rasmi kwa ajili ya kuuza nyama ya nguruwe, maji yameingia na kusababisha biashara kuwa ngumu.
Amesema kwa sasa wamehamia kwa muda upande wa pili wa barabara.
“Biashara imekuwa ngumu kwa siku hizi tangu maji yaingie kwenye maeneo yetu ya biashara, kwani barabara inayotokea mjini kufika eneo hili imejaa maji na madereva wa bajaji wamepandisha nauli kutoka Sh500 hadi Sh1,000 kwa sababu wanazunguka njia nyingine ambayo ni ndefu,” amesema mfanyabiashara, Joel Matatizo.
Diwani wa Katubuka, Moshi Mayengo amesema mara ya mwisho eneo hilo kuwa na maji mengi ilikuwa mwaka 1989-1990.
Amesema Serikali ya mkoa ipo kimya na hakuna hatua zilizochukuliwa kuondoa maji katika eneo hilo, licha ya kuwasiliana na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura).
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kali amesema kutokana na athari zilizowapata wananchi ameomba majirani kuwahifadhi wakati Serikali ikifanya tathmini, ili kuchukua hatua za namna ya kuwasaidia waathirika.
Kali amesema ni muhimu wananchi kuchukua tahadhari, ili kuepuka madhara makubwa yanayoweza kutokea, akiwataka wanaoishi bondeni au kwenye mikondo ya maji kuondoka na kutafuta mahali salama pa kuishi.
Meneja wa Tarura Wilaya ya Kigoma, Elias Mtapima amesema changamoto ya kujaa maji kwa barabara inaanzia kwa kujaa bwawa la Katubuka na maeneo yake.
Amesema kwa asili bwawa hilo linapokea maji kutoka maeneo mbalimbali ya Mji wa Kigoma.
Mtapima amesema eneo hilo linaonekana ni la chini na maji yote ya mji yanateremka kuelekea huko.
Amesema hakuna ujenzi wa barabara ambao umesababisha maji kuhamia upande mwingine.
Amesema eneo la bonde limeendelea kupungua kina kwa sababu linajaa mchanga na tope, hivyo kina kinaendelea kupungua na kusababisha maji yanapoongezeka kidogo eneo la barabara nalo hujaa maji na kushindwa kupitika.
Amesema kutengeneza barabara peke yake hakutatui tatizo, wamefanya juhudi za kuwasiliana na ngazi nyingine za ofisi ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na Serikali Kuu kuangalia kama kuna uwezekano wa kuanza kufanyia marekebisho eneo la bonde la Katubuka.
“Marekebisho hayo ikiwa ni pamoja na kuodoa tope na kutafanya paweze kupokea maji yanayotoka katika milima ya mji wa Kigoma. Kwa sasa Tarura tunafanya usanifu mpya wa kuongeza tuta la barabara, ili maji yasiweze kuathiri barabara,” amesema Mtapima.