Mvua yasababisha watu 400 kukosa makazi Ifakara

Kikosi Cha zimamoto na uokoaji wilaya ya Kilombero wakiokoa wananchi wa maeneo mbalimbali ya mji wa Ifakara Kwa kutumia boti baada ya mvua kubwa kunyesha kwa zaidi ya saa 72 na kusababisha mafuriko katika maeneo hayo. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Katika mafuriko hayo wananchi zaidi ya 50 waokolewa na wengine 400 wahifadhiwa Shule ya Msingi Ifakara ambapo pia kituo cha afya Mbasa hakifikiki baada ya barabara ya kuelekea kituoni hapo kukatika.

Morogoro. Mvua kubwa iliyonyesha mfululizo kwa zaidi ya saa 72 katika mji wa Ifakara wilayani Kilombero imesababisha mafuriko ambapo  watu zaidi 400 wamekosa makazi baada ya nyumba zao kujaa maji na nyingine kubomoka.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 5, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Danstan Kyobya amesema mafuriko hayo yamesababishwa na kujaa kwa Mto Lumemo ambao unamwaga maji yake kwenye makazi ya watu na katikati ya mji.

“Mvua hii kubwa ilianza juzi na haijakatika na mchana wa leo ndio imeongezeka hadi kusababisha Mto Lumemo uliopo jirani na mji wa Ifakara kumwaga maji kwenye makazi ya watu na maeneo ya katikati ya mji na kuathiri nyumba na biashara ambapo maji yameingia kwenye baadhi ya maduka na kuharibu bidhaa,” amesema Kyobya.

Mkuu huyo wa wilaya amesema yapo majengo ya umma ambayo nayo yamezingirwa na maji ikiwemo Shule ya Sekondari Kashungu na kituo cha afya cha Mbasa ambapo pamoja na kujaa maji, pia hakufikiki kutokana na barabara inayokwenda kwenye kituo hicho kukatika.

Ameeleza jitihada za Serikali baada ya kutokea kwa mafuriko hayo, mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya, amesema hatua ya awali ilikuwa ni kuwaokoa wananchi ambao walioathiriwa  na maji kwenye nyumba zao na hatua ya pili ni kuwatafutia mahala pa kuwahifadhi.

“Watu hao 400 tayari tumeshawapeleka katika Shule ya Msingi Ifakara ambako watakuwepo hapo na watapewa chakula huku Serikali tukiendelea na uokoaji, kwa kuwa mvua bado inanyesha na hatujui maji yatapungua baada ya muda gani,” amesema Kyobya.

Kwa upande wake, Ofisa afya wa halmashauri ya mji wa Ifakara ambaye pia ni mratibu wa maafa, Jafari Ngogomela amesema mafuriko hayo hayajawahi kutokea tangu mvua zilipoanza kunyesha wilayani humo, hivyo kamati ya maafa imekuwa na wakati mgumu kuwaokoa wananchi.

Amesema  kazi ya uokoaji imeanza asubuhi wakati mvua ilipoongezeka na hadi kufikia saa 10 jioni walifanikiwa kuwaokoa watu 50, ambao walikuwa kwenye hatari ya kufa maji baada ya nyumba zao kujaa maji na nyingine kuanguka.

“Pamoja na kubomoka kwa nyumba lakini pia vyoo vingi vimebomoka na kusababisha kinyesi kuzagaa kwenye maeneo mbalimbali, hivyo tumewaelekeza wananchi namna ya kutunza mazingira na kuwataka waache kujisaidia ovyo badala yake watafute maeneo yenye vyoo ili wajisaidie,” amesema Ngogomela.

Akieleza namna uokoaji ulivyoendeshwa, Kamanda za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kilombero, Haji Madulika amesema wanaokoa kwa kutumia boti iliyotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori nchini (Tawa) kwa kushirikiana vijana wa skauti na kazi hiyo inaendelea hadi maji yatakapopungua.