Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

 Wananchi watahadharishwa na mamba wakati wa mafuriko

Muktasari:

  • Kutokana na ongezeko la maji yanayoletwa na mvua zinazoendelea kunyesha nchini, wananchi wameaswa kuwa makini na mamba

Morogoro. Wakati mvua zikiendelea kunyesha na kusababisha mafurika katika maeneo mbalimbali nchini, tahadhari imetolewa kwa wananchi kujiepusha na mamba wanaoishi majini.

Mikoa ambayo imeathirika na mvua kubwa zilizonyesha na kusababisha mafuriko ni Pwani, Morogoro, Arusha, Mbeya na Mwanza huku baadhi ya wananchi wakipoteza makazi na mali zao.

Akizungumza na Mwananchi jana Aprili 12, 2024 Ofisa Mhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa), Gilbert Magafu amesema kipindi hiki cha mafuriko wanyama kama mamba na viboko wanahama wakifuata maji.

"Mamba ni mnyama jamii ya mjusi ambaye maisha yake kwa asilimia kubwa yanakuwa kwenye maji lakini wakati mwingine utamkuta nchi kavu na anapokuwa nchi kavu huwa anaota jua na wakati mwingine huwa kwenye mawindo.

“Mamba ana uwezo wa kuogelea umbali wa kilometa 32 kwa saa moja, hivyo huyu mnyama kipindi hiki cha mvua nyingi watafika kwenye makazi ya binadamu kwa kusombwa au kusafiri na maji, hivyo tahadhari zinapaswa kuongezeka.

"Tabia za mamba ni kwamba huwinda kwa kushtukiza ndiyo maana watu wengi wanaliwa na sasa kwa kuwa maeneo mengi kama Ifakara, Rufiji yamekuwa na mafuriko mara kwa mara wananchi wa maeneo hayo wanapaswa kuchukua tahadhari ili wasiliwe na mnyama huyu,” amesema Magafu.

Amesema mnyama huyo anaweza kukaa kwenye maji kwa zaidi ya saa moja bila kutoka kupumua na ana uwezo wa kuona akiwa ndani ya maji.

“Sasa kwa kuwa maeneo mengi hapa nchini kuna maji yametuama wananchi wanapaswa kuacha kufanya shughuli zao pale hasa zile za kufua nguo, kuvua samaki, kuchota maji ili mamba asiweze kuleta madhara,” amesema Magafu.

Joseph Deus,  mkazi wa Kijiji cha Mlali wilayani Mvomero amesema elimu iliyotolewa na wahifadhi ni sahihi kwa kuwa kwenye kijiji chao wakati huu wa maji mengi wameshawahi kutokewa na mamba

"Kulikuwa na mamba aliyekuwa anahatarisha maisha ya watu,  lakini tulitoa taarifa kwa mkuu wetu wa wilaya akatuma timu yake na yule mamba aliuawa,” amesema Deus.

Tuliambiwa yule mamba ameletwa na mafuriko na alikuwa na urefu wa zaidi ya futi sita, hivyo wananchi wanaoishi maeneo ambayo maji ni mengi ambayo yamekuja wakati huu wa mafuriko wawe makini."

Aprili 8, 2024 Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli alithibitisha kuuawa kwa mamba aliyekuwa akiwasumbua wananchi wa Kata ya Mlali.

"Kulikuwa na mamba aliyeonekana huku Mlali, akitishia maisha ya watu, hivyo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ikafika kwa haraka na kumuua yule mamba, lakini kwa taarifa zilizopo ni kwamba kuna zaidi ya mamba wanne ambao wamekuja tena," amesema Nguli.