Mvua yasomba madaraja Morogoro

Mvua yasomba madaraja Morogoro

Muktasari:

  • Mvua kubwa iliyonyesha kata ya Lukobe manispaa ya Morogoro usiku wa kuamkia jana Februari 22, 2021 imeharibu miundombinu ya barabara na madaraja na kusababisha baadhi ya watu kuvushwa kwa kubebwa.

Morogoro. Mvua kubwa iliyonyesha kata ya Lukobe manispaa ya Morogoro usiku wa kuamkia jana Februari 22, 2021 imeharibu miundombinu ya barabara na madaraja na kusababisha baadhi ya watu kuvushwa kwa kubebwa.

Waliokumbwa  na kadhia hiyo ni  wakazi wa mtaa ya Azimio, Kambitano,  Golonya,  Uluguruni na Mzambarauni.

Mmoja wa wakazi hao, Shani Mohamed amesema mara kwa mara barabara na madaraja katika kata hiyo yamekuwa yakisombwa na maji na maeneo mengine kutopitika.

Aliiomba  wakala wa barabara mijini na vijijini (Tarura) kuweka madaraja ya kudumu ili maeneo hayo yapitike wakati wote.

"Kuna baadhi ya wazazi wameogopa kuwapeleka watoto wao shule wakihofia maeneo hayo hatari maana mvua ikinyesha hayapitiki na kuhatarisha usalama wa watoto," amesema Shani.

Diwani wa Lukobe,  Selestine Mbilinyi amesema changamoto hiyo wameiwasilisha Tarura na katika vikao mbalimbali vya Mkoa.

"Niliwahi kuwaambia baadhi ya viongozi kwamba haya maeneo ni hatari na tusisubiri watu wafe ndio tuchukue hatua nawahakikishia wananchi wangu hii changamoto nitaitatua," amesema Mbilinyi.

Meneja wa Tarura manispaa ya Morogoro, Leopold Runji amesema tayari matengenezo ya dharura yameanza katika maeneo yaliyoharibika, akibainisha kuwa bajeti ya mwaka 2021/22 imeainisha maeneo yote korofi yaliyopo katika kata hiyo.