Mvutano wa Ndugai, Masele ulipopotea maboya

Saa 11:13 jioni Mei 16, mwaka huu Nigeria ilimpendeza seneta wa Beyelsa Mashariki, Nigeria, Ben Murray-Bruce kuweka picha ya baiskeli za umeme kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, akasema “hii siyo Ulaya ni Rwanda.”

Bruce pia ni mfanyabiashara mkubwa. Alisema Rwanda imepiga hatua kubwa kiteknolojia kwa kuwa na baiskeli za umeme (e-bikes), mtu anaweza kuzifikia kwa kutumia App ya simu ya mkononi, anatumia na kurejesha. Kwa kufanya hivyo, Rwanda inaokoa fedha nyingi na muda.

Kwa vile Bruce ni wa chama cha upinzani cha PDP, ujumbe wake ulitafsiriwa kama shambulio kwa chama tawala cha APC cha Rais Muhammadu Buhari, kwamba inashindwa na nchi ndogo ya Rwanda.

Baadhi ya watoa maoni walimshauri Bruce kuwa uongozi ni kuonesha njia. Badala ya kuonesha picha, yeye kama mfanyabiashara anaweza kuwashirikisha wengine katika sekta binafsi ili kufanikisha mradi wa e-bikes nchini Nigeria.

Kuna ambaye alimwambia Bruce kuwa Nigeria ni tofauti na Rwanda. Akasema Rwanda njia zote za uchumi wake zimehodhiwa na Serikali chini ya Rais Paul Kagame, wakati Nigeria, hakuna mwanya kwa Serikali kufanya hivyo. Uchumi wa Nigeria ni wa sekta binafsi.

Inawezekana Bruce kusudi lake lilikuwa kuonyesha namna Afrika inavyopiga hatua kiteknolojia. Hata hivyo, maelezo yake hayakutosha, hivyo tafsiri za watu zikawa kwenye siasa. Wengine wakamuona kuwa anataka Nigeria iwe kama Rwanda kwa namna inavyoonekana ni nchi ya uamuzi wa mtu mmoja, Rais Paul Kagame.

Hapo kosa ni la nani? Mwenye kosa ni Bruce mwenyewe. Alipaswa kutambua kuwa hii ni dunia ya intaneti. Hivyo, alitakiwa kufafanua dhamira yake. Dunia ya sasa, ukisema kitu bila kueleweka vizuri, watu wa mitandaoni watatengeneza tafsiri yao. Utabaki unashangaa, mbona maana yako haikuwa inavyotafsiriwa na wengi?

Dunia ya intaneti, hasa unapokuwa kiongozi, unatakiwa ufafanue vizuri mawazo yako, vilevile utazame kipindi ambacho unajenga hoja, vinginevyo intaneti itakupeleka mahali ambako hukutaka.

Ndugai Vs Masele

Job Ndugai ni Spika wa Bunge la Tanzania. Stephen Masele ni mbunge wa Shinyanga Mjini. Masele pia ni mbunge wa Bunge la Afrika, vilevile Makamu wa kwanza wa Rais wa Bunge la Afrika.

Sifa ya kuwa mbunge katika Bunge la Afrika ni lazima uwe mbunge katika nchi yako ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

Ukiwa mbunge, ndiyo unaomba kuchaguliwa kuwa mbunge wa Bunge la Afrika. Ukipoteza ubunge kwenye nchi yako, moja kwa moja unakosa sifa za ubunge Bunge la Afrika.

Hapa ndipo kwenye mamlaka ya Ndugai. Kwamba Masele ni kiongozi wa juu kabisa Bunge la Afrika, lakini Ndugai anaweza kumfanya asiwe mbunge katika Bunge la Afrika kwa sababu ‘chaneli’ ya ubunge wake ni Bunge la Tanzania.

Ndani ya Bunge la Afrika kuna kashfa kumhusu Rais wa Bunge hilo, Roger Dang, raia wa Cameroon kutumia madaraka yake vibaya – kuhusika na rushwa ya upendeleo wa ajira na unyanyasaji wa kingono kwa watumishi.

Tuhuma dhidi ya Rais Dang (Spika) ni rasmi. Bunge la Afrika limezifanyia kazi na kamati ya uchunguzi imemtia hatiani Dang, ambaye alikuwa anajaribu kujinasua. Inadaiwa Dang baada ya kumuona Masele ni tatizo, alimshtaki kwa Ndugai.

Na Ndugai alimwita Masele nyumbani (Bunge la Tanzania) ajieleze. Awali, inadaiwa Masele alikaidi wito na akasema kwamba aliagizwa na Waziri mkuu, Kassim Majaliwa, apuuze wito wa Ndugai.

Kutokana na mvutano huo, Ndugai alitangaza kusimamisha kwa muda ubunge wa Masele kwenye Bunge la Afrika. Alimtuhumu kuwa anafanya mambo ya hovyo kugonganisha mihimili.

Baada ya kauli ya Ndugai na uamuzi wake, intaneti ilikuwa kinyume naye. Watoa maoni mitandaoni walimshambulia. Kwa mitazamo ya wengi, Masele yupo sahihi, maana tuhuma dhidi ya Dang ni nzito na anatakiwa kuwajibishwa.

Watu hawakuangalii kosa lililosemwa “kuchonganisha mihimili”, walijikita kwenye tuhuma za msingi zinazomkabili Dang.

Baada ya nivute nikuvute, Masele aliitikia wito. Kamati ya Maadili ya Bunge ilimkuta na hatia ya kugonganisha mihimili na kupendekeza aadhibiwe kwa kuzuiwa kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge. Hata hivyo Ndugai aliamua kumsamehe.

Pamoja na kutoa msamaha, mitandaoni Ndugai ameshahukumiwa kuwa anamtetea Dang, mwenye tuhuma. Akawa anamdhibiti Masele, anayepigania misingi.

Silioni kosa la Ndugai kumwita Masele alieleze Bunge la Tanzania kinachoendelea katika Bunge la Afrika. Nauona utovu wa nidhamu wa Masele kusema aliambiwa na Waziri mkuu akaidi wito wa Spika Ndugai. Matamshi hayo ni uchonganishi kwa Serikali na Bunge.

Pamoja na hivyo, Ndugai alipaswa kukumbuka yeye ni kiongozi katika ulimwengu wa intaneti. Angekumbuka hilo, angekuwa na angalizo kuhusu matamshi yake na uamuzi wake wa jumla kuhusu Masele.

Angejiuliza, je, tuhuma zipi ni nzito? Masele kukaidi wito au Dang kufanya unyanyasaji wa kingono na rushwa? Ukaidi wa Masele umeibukia wapi? Kabla, baada au katikati ya tuhuma za Dang? Majibu ni kuwa tuhuma za Dang ni nzito zaidi. Ukaidi wa Masele ulitokea katikati ya tuhuma za Dang.

Ndugai kwa kutambua yeye ni kiongozi katika ulimwengu wa intaneti, alipaswa kufahamu kwamba uamuzi wake kuhusu Masele ungesababisha sababu ya msingi izungumzwe. Na kwa sababu hiyo, alitakiwa kufahamu kwamba mitandao ingemhukumu kwa kumtetea Dang na kumdhibiti Masele.

Kuna swali; katika ulimwengu huu wa teknolojia ya habari na mawasiliano, ilishindikana vipi Ndugai kumpigia simu kuzungumza na Masele mpaka amwite nyumbani aache shughuli muhimu za Bunge la Afrika ikiwemo tuhuma za Dang?

Dunia ya intaneti yenye Skype, ilishindikana kufanya mkutano (Skype Meeting) kuondoa utata? Mwisho, Ndugai angeweza kulitatua suala la Masele kimyakimya, badala ya kupaza sauti. Kwa kuwa alizungumza, intaneti ikashtuka, ikatafuta sababu, ikaibuka na tafsiri kwamba Ndugai anamtetea Dang.

Busara za uongozi katika ulimwengu wa intaneti, zinataka ukumbuke kuwa kila unachofanya na unachosema, watu mitandaoni watapokea wanavyojua wao na watatafsiri kwa namna yao. Tafsiri yao itakuhukumu na itakukwaza. Hivyo, lazima uwe makini sana.

Kauli ya Masele

Ninaomba kutumia fursa hii kukuomba radhi wewe (Spika) binafsi na familia yako kwa usumbufu wowote ulioupata kupitia sakata hili. Niwaombe radhi wabunge wenzangu kwa usumbufu mlioupata. Nitumie nafasi hii pia kuwaomba radhi viongozi wangu wakuu, mwenyekiti wa chama changu Rais John Magufuli, Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) ambaye ni mwenyekiti wetu wa wabunge wa CCM kwa usumbufu wowote walioupata kutokana na jambo hili.

Pia, naomba rekodi ibaki sawa kuwa, makosa yaliyoorodheshwa katika shtaka langu, ningefurahi kama hansard ya kikao ingeletwa katika Bunge hili ili wabunge na Watanzania wajue ukweli.

Ninayo barua ya mwaliko wa kuhudhuria kikao cha Bunge la PAP hii hapa. Utaratibu wa Bunge, huwa hatuji kuomba kibali, bali tunatoa ‘notification’ kwa hiyo mheshimiwa Spika nilileta notification katika ofisi ya Katibu wa Bunge. Tuhuma zinasema nimesafiri bila kibali, sisi tuko wanne, kwa nini Masele ninaadhibiwa mimi na wabunge wenzangu wasichukuliwe hatua?

Barua ambayo Spika uliniandikia ukitaka nirudi Mei 16, aliipata saa 11 jioni ikinitaka niwe nimefika Tanzania Jumanne ya Mei 17 saa 4:00 asubuhi jambo ambalo lingekuwa gumu kutokana na kubadili tiketi ya ndege na sikuwa na fedha za kulipia hoteli na Bunge kutolipa posho za kujikimu.

Barua hiyo ilitaka kutumiwa na Rais wa PAP ambaye ni raia wa Cameroon anayetaka kuning’oa kwenye wadhifa wa Makamu wa Rais wa PAP na mjumbe wa Bunge hilo.

Nilifikiria haraka na busara yake ikaniongoza kukata rufaa na ndio sababu ya kuwasiliana na mwenyekiti wa CCM na Waziri Mkuu ambaye ni mwenyekiti wa wabunge wa CCM.

“Niliwaandikia ujumbe na kuwatumia barua hii nikiomba ushauri. Barua hii ilitaka kutumika kunichinja, kukata kichwa changu nisiwe Makamu wa Rais na mjumbe wa PAP, kama ni mbunge wa Bunge hili ungefanya nini?

Spika kwa nafasi yako ungeweza kunipigia simu na kuniuliza kipi kimetokea lakini uliamua kunihukumu bila hata kamati ya maadili kunisikiliza na ninasikitika kwamba sikuchonganisha mihimili, nisingeweza kupeleka jambo hili kwa waziri au katibu wa wabunge wa CCM kwa sababu muda ulikuwa mfupi.

“Naamini umefanya ushauri wa kutosha, nimekubali makosa, kwa heshima ya Bunge langu, nakuja mbele yako kuomba radhi kwa usumbufu ulioupata, nashukuru kwa nafasi hii, Bunge na Watanzania kujua ukweli,” alisema.