Mwalimu adaiwa kumuua mwenzake darasani Geita

Mwalimu anaefundisha KKK katika shule ya msingi Igaka Wilaya Geita Emanuel Chacha wakati wa uhai wake.

What you need to know:

  • Mwalimu wa Shule ya Msingi Igaka wilayani Geita anadaiwa kumuua mwalimu mwezake wakiwa darasani kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali chanzo kikitajwa ni kugombea madaraka na walimu wengine kumtenga hasa marehemu waliyekuwa wanafundisha naye darasa la kwanza.

Geita. Mwalimu wa Shule ya Msingi Igaka, Samwel Subi anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Geita kwa tuhuma za kumuua mwalimu mwezake Emanuel Chacha (pichani) kwa kumchoma na kisu akiwa darasani.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema limetokea Machi 15 saa 3:45 asubuhi wakati walimu hao wakiandaa mtihani kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la kwanza.

“Kata ya Isulwabutundwe mwanaume wa miaka 35 katika Shule ya Msingi Igaka aliuawa kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali kwenye chembe ya moyo na mwanaume mwingine mwenye miaka 35 ambae ni mwalimu mwenzake. Walimu wote wawili walikuwa darasani wakiandaa mtihani ndipo mtuhumiwa alitoa kisu na kumchoma mwenzake kwenye chembe cha moyo,” amesema Kamanda Jongo.

Kamanda alisema chanzo cha tukio hilo inadaiwa kuwa ni ugomvi baina ya walimu hao ambao walikuwa wanagombea uongozi kwenye kitengo cha elimu ya kujitegemea.

“Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea mwalimu amekamatwa na amekiri na sababu anadai aliona walimu wenyeji wanamchukia na wamemtenga na ndio sababu ya kutengeneza nia ya kutenda tukio hilo,” amesema.