Mwalimu auawa kinyama, mtoto wake ajeruhiwa

Marehemu Rafaela Msemwa, mwalimu wa shule ya msingi anayedaiwa kuuawa

Dar/Ludewa. Ni mauaji ya kinyama! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya mwalimu wa Shule ya Msingi Nyakatundu iliyopo Rufiji mkoani Pwani, Rafaela Msemwa kuuawa kwa kukatwa mapanga na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia Agosti 6, mwaka huu.

Pamoja na kutekeleza unyama huo, watu hao pia walimjeruhi mtoto wake mwenye umri wa miaka minne, aliyejulikana kwa jina la Bravian Mwamwenda na kumsababishia jeraha kubwa usoni na kwa sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mpaka sasa Bravian ameendelea kupokea matibabu kutoka kwa wataalamu bingwa na tayari wamemfanyia upasuaji wa jicho na wanasubiri kumfanyia vipimo vingine kuangalia iwapo jicho hilo litaweza kuona tena.

Hayo yalisemwa jana na baba mdogo wa marehemu, Nolasko Msemwa alipozungumza na Mwananchi akiwa nyumbani kwao wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe kuhusiana na mauaji hayo.

Alisema mwili wa Rafaela ulisafirishwa jana kutoka Rufiji kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya taratibu nyingine za maziko.

“Taratibu za mazishi mpaka nilivyo uliza mchana huu (jana) mwili wa marehemu utaondoka Rufiji kuelekea Dar es Salaam na kesho (leo) mchana utasafirishwa kuelekea Mbeya, Tukuyu atakakoenda kuzikwa na sisi tutaondoka kesho (leo) saa nne asubuhi kuelekea Tukuyu,” alisema Msemwa.

Taarifa za msiba

Awali alisema taarifa za msiba walizipata kupitia kwa baba wa marehemu, Aranus Msemwa ambaye alipigiwa simu na mwalimu aliyekuwa akifanya kazi na mwanaye.

“Ilikuwa Jumapili saa saba mchana, kaka yangu Aranus Msemwa alipigiwa simu na mwalimu mmoja kutoka huko Rufiji akiuliza kama yeye ndiye baba yake na Rafaela.

“Akamjibu ndiyo, akamuuliza kama ana taarifa yoyote kuhusu mwanaye akamjibu hana, akamwambia yeye ni mwalimu na anataka kumtaarifu kuwa mtoto wake amevamiwa na watu wasio julikana na amefariki,” alisema Msemwa.

Alisema baada ya kaka yake kupokea taarifa hizo alirejea nyumbani na kuwapigia simu kuwaeleza juu ya taarifa ya kuvamiwa kwa mtoto wao na kuuawa.

Alisema baada ya kuwasiliana na mume wa marehemu, siku hiyo aliwajibu kuwa naye amepata taarifa.

“Alituambia yuko njiani anaelekea Rufiji, lakini yeye aliambiwa kuwa mke wake ni mgonjwa sana, hawakumwambia kuwa amefariki,” alisema Msemwa.

Kuhusu hali ya mtoto alisema, ameshafanyiwa upasuaji wa jicho na anaendelea vizuri.

“Mtoto alifanyiwa upasuaji wa jicho jana (juzi) Muhimbili, mpaka asubuhi ya leo (jana) nilivyomuuliza baba yake alisema anaendelea vizuri na madaktari wamesema zipite siku chache ili waone uwezo wa jicho hilo kuona, jicho lilipasuka na wameshalifanyia upasuaji, ulikuwa ni uvimbe na damu iliganda mahali fulani wameshaitoa,” alisema Msemwa.

Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Rufiji, Protas Mutayoba alikiri kutokea kwa tukio hilo na alisema tayari uchunguzi umeanza ili kuwabaini waliohusika na mauaji hayo. “Tukio limetokea usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili Agosti 6, huyu mama ni mwalimu wa Shule ya Nyakatundu, aliuawa na watu ambao hawajulikani na wakamuumiza mtoto wake mdogo wa miaka minne, kwa hiyo tunaendelea kufuatilia kuona namna ya kuwapata hawa waliotenda kosa hilo,” alisema kamanda huyo.

Kwa mujibu wa RPC, Mwalimu Rafaela alikuwa anaishi peke yake na mtoto wake kwenye nyumba ya shule na ni mgeni eneo hilo ametokea Tarime, mkoani Mara.

“Kwa mujibu wa Ofisa Elimu wa Wilaya ya Rufiji, tangu amehamia shuleni hapo hajafikisha miezi mitatu,” alisema Kamanda Mutayoba.

Akizungumzia namna walivyobaini mauaji hayo, Kamanda Mutayoba alisema ni baada ya mwalimu mwenzake kufika nyumbani hapo akimfuata waende kanisani kama ilivyokuwa miadi yao ya siku ya Jumamosi jioni.

“Kuna mwalimu ambaye ni jirani yake, ndiye aliyegundua mauaji hayo. Jioni waliagana kwamba atampitia waende wote kanisani, ilipofika asubuhi akawa anamtafuta ili waende, sasa akawa hapatikani kwenye simu, ikabidi aende nyumbani kwake ndiyo akakutana na hali ile,” alisema kamanda huyo.

Alisema kwa upande wa Jeshi la Polisi tayari wameanza msako; “kazi yetu ni lazima tufanikishe kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliotenda uovu huu, kama ni mmoja au wengi tupo kazini, tunafanya upelelezi wetu na tutawatia mbaroni tu.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Michael Gwimile alisema Rafaela alikuwa mtumishi wa halmashauri divisheni ya elimu ya awali na msingi.

“Halmashauri na menejimenti imepokea kwa masikitiko taarifa za kifo chake na inatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki,” alisema Gwimile.

Msiba wa mwalimu huyo uko nyumbani kwa shemeji yake maeneo ya Ubungo Makoka, jijini Dar es Salaam.

Mwananchi lilifika kwenye msiba na kushuhudia ndugu, jamaa na marafiki wakiwa wamekusanyika wakiendelea na maombolezo.

Hata hivyo, ndugu waliokuwepo hapo hawakuwa tayari kuzungumza kuhusiana na msiba huo.