Mwalimu jela miaka 30, viboko vinne kwa kubaka mwanafunzi
Muktasari:
- Amepatikana na hatia baada ya ushahidi kuonyesha alibaka mwanafunzi huyo kwa kumrubuni kwa Sh1,500.
Mbeya. Mahakama ya Wilaya ya Kyela Mkoa wa Mbeya, imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka 30 jela, Mwalimu wa Shule ya Msingi Ngeleka iliyopo Halmashauri ya Busokelo Wilaya ya Rungwe, Juma Mhanga (41) baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka mwanafunzi mwenye umri wa miaka 13.
Mbali na hukumu hiyo, Mhanga pia amehukumiwa kucharazwa viboko vinne na kulipa faini ya Sh500,000 kama fidia.
Akitoa hukumu hiyo Agosti 23, 2024, Hakimu Mkazi, Paul Barnabas Mabula amesema Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa ambao haujaacha shaka kuwa Mhanga alimwingilia kimwili mwanafunzi huyo anayeishi na bibi yake wilayani Kyela.
Amesema wakati wa utoaji ushahidi, shahidi muhimu ambaye ni mwanafunzi huyo alieleza Mahakama kuwa mara kadhaa mwalimu huyo ambaye ni jirani na bibi yake alikuwa akienda kuchaji simu na kuangalia mpira nyumbani kwao kutokana na nyumba aliyokuwa akiishi kutokuwa na umeme.
Alieleza alikuwa akimfanyia kitendo hicho wakati bibi yake hayupo, huku akimuonya kutosema kwa mtu yeyote na kisha kumpatia Sh1,500 .
Akijitetea kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Mhanga alikana kutenda kosa hilo, huku akidai bibi wa mhanga (jina limehifadhiwa) ndiye alikuwa akimtaka kimapenzi baada ya kumkatalia ndipo wakamsingizia kesi hiyo ya kubaka.
Pia alidai siku moja kabla ya tukio hilo alikuwa mgonjwa, aliumia mkono, hivyo asingeweza kutekeleza tukio la ubakaji ambalo linahitaji matumizi ya nguvu.
Kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Davice Msanga alieleza mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kati ya Novemba 20, 2023 na Machi 9, 2024 kwa kumrubuni mwanafunzi huyo kwa kumpa Sh1,500.
Wakili Msanga aliiomba Mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria, ili iwe fundisho kwa mtumishi huyo wa Serikali aliyepaswa kuwa kioo cha jamii, mlezi wa watoto.
Mwendesha mashtaka huyo ambaye pia Mkuu wa Mashtaka Wilaya ya Kyela , amewataka wazazi na walezi kuwa makini kuwatunza watoto dhidi ya vitendo vya ukatili, ubakaji, ulawiti na unyanyasaji wa kijinsia.