Mwalimu mkuu adaiwa kumbaka, kulawiti mwanafunzi Bunda
Muktasari:
- Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limesema vitendo vya ubakaji na ulawiti vilifanyika siku moja kabla ya mwanafunzi kunyweshwa sumu ili kupoteza ushahidi
Bunda. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Masaunga wilayani Bunda, Vicent Nkunguu (39) kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti mwanafunzi wa darasa la sita shuleni hapo kisha kumnywesha sumu.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Machi 13, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Salum Morcase amesema vitendo vya ubakaji na ulawiti vilifanyika siku moja kabla ya kunyweshwa sumu siku iliyofuata lengo likiwa ni kupoteza ushahidi.
Kamanda Morcase amesema mwanafunzi huyo (16) alibakwa Machi 8, 2024 usiku akiwa amelala nyumbani kwa mtuhumiwa huyo Kijiji cha Kisorya alipokuwa amekwenda kwa ajili ya kuwapikia watoto wa mtuhumiwa baada ya kuombwa na mke wa mwalimu huyo aliyesafiri kwenda kwenye maombi katika Kijiji cha Igundu.
"Akiwa amelala na watoto chumbani, mwalimu huyo alikwenda kwenye chumba cha watoto na kumwambia mwanafunzi huyo kuwa, amekosa usingizi na kwenda naye kwenye chumba chake ambako alimbaka na kumlawiti," amesema .
Kamanda Morcase amesema baada ya kumaliza haja zake alimruhusu kurudi chumbani kwa watoto na siku iliyofuata mtoto huyo aliitwa na mama yake kwenda kufukuza ndege kwenye shamba lao la mpunga.
Amesema baada ya kutoka shambani mtoto huyo alirudi nyumbani kwa mwalimu na baada ya muda aliamua kuondoka akihofia kubakwa na kulawitiwa tena.
"Mwalimu alipoona mtoto anaondoka alimzuia lakini mtoto akasisitiza lazima aondoke ndipo alipomshika kwa nguvu na kwenda naye nyuma ya nyumba kwenye banda la kuku na kumywesha sumu lengo likiwa ni mtoto huyo afe ili asije akasema kuhusu kitendo alichokifanya," amesema.
Kamanda Morcase amesema baada ya kumywesha sumu mtoto huyo alianza kutembea hadi kwa kaka yake akaeleza namna alivyobakwa kisha kupoteza fahamu na kupelekwa hospitalini.
Amesema uchunguzi juu ya tukio hilo unaendelea.
Mama wa mtoto huyo (jina linahifadhiwa), amesema hali ya mtoto wake imeanza kuimarika na kwamba hivi sasa ameanza kujitambua.
"Jana jioni aliweza kutoa maelezo, alisema alibakwa usiku wa Machi 8, 2024 na kunyweshwa sumu Machi 9, 2024 baada ya kurudi nyumbani kwa mwalimu muda mfupi akitokea shambani kufukuza ndege.
"Ni kweli nilimuita aje kufukuza ndege na alikuja shambani saa saba mchana lakini saa tisa alasiri akarudi kwa mwalimu tofauti na sisi tulivyodhani kuwa matukio yote ya ubakaji na ulawiti pamoja na sumu yalifanyika siku moja," amesema.
Kamanda Morcase amesema baada ya kunyweshwa sumu mtoto huyo alitembea kwa kujikongoja hadi kwa kaka yake na alipata msaada wa kupelekwa polisi kisha hospitali.
"Alikuwa anatembea huku anaanguka lakini alifanikiwa kufika kwenye saa 4 usiku akiwa amechoka Mungu ni mwema walifanikiwa kumfikisha hospitali akiwa hai," amesema Kamanda Morcase.