Baba mzazi amlawiti, kumbaka mwanaye mara saba

Muktasari:

Mama mzazi alimuona mwanaye akitembea mwendo usio wa kawaida na kushuku kuwa kuna jambo haliko sawa

Moshi. Hivi unaweza kuamini baba mzazi anaweza kumbaka na kumlawiti mwanaye mwenye umri wa miaka 11?

Katika tukio lililotokea mwaka 2019, unaweza kufikiri unaota, lakini mkazi wa Mpechi wilayani Njombe, alikuwa akilala na bintiye chini katika godoro akimfanyia vitendo hivyo huku watoto wengine watatu wakilala kitandani.

Baba huyo alikuwa akilala chumba kimoja na watoto wake wanne baada ya kumfukuza mkewe aliyekuwa akilala jikoni.

Mshitakiwa huyo ambaye kwa sababu za maadili na kisheria zinazotaka mwathirika asitambuliwe kwa namna yoyote tunahifadhi jina lake, anatumikia kifungo cha maisha jela na anatakiwa kumlipa mtoto wake fidia ya Sh10 milioni.

Hii ni baada ya rufaa aliyoikata Mahakama ya Rufani kutupiliwa mbali na jopo la majaji watatu Rehema Mkuye, Dk Paul Kihwelo na Paul Ngwembe walioketi mjini Iringa Desemba 11, 2023 na hukumu yake kusomwa Jumanne ya Februari 6, 2024.

Awali, alikuwa ameshitakiwa kwa makosa manne, mawili ya kumbaka mwanaye huyo wa kumzaa na mawili ya kumlawiti; kesi hiyo ikasikilizwa na Mahakama ya Wilaya ya Njombe iliyomtia hatiani kwa makosa yote manne.

Ikamhukumu kifungo cha miaka 30 kwa kila kosa kwa makosa mawili ya kufanya mapenzi na mtoto wa kumzaa na vifungo viwili vya maisha kwa makosa mawili ya kumlawiti, Mahakama hiyo ikamwamuru pia kulipa fidia ya Sh10 milioni.

Hakuridhika, akakata rufaa Mahakama Kuu ya Tanzania iliyoketi Iringa chini ya Jaji Firmin Matogolo ambayo hata hivyo ilitupwa Desemba 7, 2020 ndipo akakata rufaa mahakama ya Rufaa ambayo nayo ikaitupa na kubariki adhabu hiyo na fidia.

Ilidaiwa na upande wa mashitaka kuwa katika siku na mwezi usiojulikana mwaka 2019 eneo la Mpechi Wilaya ya Njombe, mrufani alimbaka mtoto wake wa kumzaa na pia kumlawiti, makosa ambayo alijaribu kuyakana bila mafanikio.


Ushahidi wa mtoto ulivyommaliza

Mama mzazi wa mtoto ambaye naye tunahifadhi jina lake ili kutomtambulisha mwathirika kwenye jamii, alisema asubuhi moja alimuona mwanaye akitembea mwendo usio wa kawaida na kushuku kuwa kuna jambo ambalo haliko sawa.

Lakini alipomuuliza mtoto, alijibu alianguka kwa bahati mbaya kutoka kwenye kochi wakati akiwa usingizi, alipozidi kuchunguza, mdogo wake wa kiume (9) alimweleza mama yake kuwa dada yake huwa analala kwenye godoro chini.

Akafichua kuwa yeye na wadogo zake wengine wawili walikuwa wakilala kitandani, na aliposikia hayo, mama akaamua kutoa taarifa hizo za shaka kwa mashemeji zake, kanisani na ustawi wa jamii lakini hakubadilika.

Badala yake, baba huyo akamripoti mkewe Polisi Njombe kwenye dawati la jinsia, akimtuhumu kuwa mkewe alimpiga mtoto wao huyo.

Hali hiyo ilisababisha mkewe akamatwe na polisi lakini aliachiwa kwa dhamana.

Ushahidi wa mwathirika uliotolewa Mahakama ya Wilaya ya Njombe, unaeleza hatua kwa hatua namna alivyokuwa akilala na baba yake kwenye godoro na kumbaka na kumlawiti.

Mwathirika alisema mara zote alitakiwa asipige kelele kwa ahadi angenunuliwa zawadi.

Mwathirika huyo aliieleza Mahakama kuwa, baba yake alikuwa akimbaka na kumlawiti mara kwa mara na alifanya hivyo zaidi ya mara saba na mara zote alikuwa akifanya hayo wadogo zake watatu wakiwa wamelala kitandani na mama yao amelala jikoni.

Katika ushahidi huo, mtoto mwingine alisimulia namna alivyokuwa analala na wadogo zake kitandani wakati baba na mwathirika wakilala kwenye godoro chini katika chumba hicho hicho wakati.

Ni kutokana na ushahidi huo mzito, Mahakama ya Wilaya ya Njombe ilimtia hatiani kwa makosa manne ya ubakaji na ulawiti aliyokuwa ameshitakiwa nayo na kumhukumu kifungo cha maisha, akakata rufaa lakini ikatupwa.


Jopo la majaji

Wakiitupa rufaa, Jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania ambacho ni chombo cha juu na cha mwisho cha rufaa, lilisema Mahakama Kuu ilikuwa sahihi kubariki adhabu aliyopewa kwa kuwa mashitaka yalithibitishwa.

Jopo hilo limeuchukulia utetezi wake kama njia ya kujaribu kujinasua na adhabu hiyo na kueleza kuwa mrufani kwa maneno yake mwenyewe, alikiri kulala na mwanaye huyo wa kike chumba kimoja wakati mkewe akilala jikoni.

Majaji wakasema ushahidi mwingine wa kushtusha ulitoka kwa mwathirika na mdogo wake kwamba baba huyo alikuwa akilala na mwanaye huku mkewe akishuku jambo na hata mtoto alipopimwa alikutwa ameingiliwa.

“Tumeridhika kuwa ushahidi uliopo katika kumbukumbu za Mahakama iliyosikiliza kesi (wilaya ya Njombe) na Mahakama Kuu iliyosikiliza rufaa ya kwanza zilikuwa sahihi kubaini kuwa mshitakiwa alikuwa na hatia,” walisema majaji hao.

Majaji hao wakasema kwa hoja zilizotolewa na wakili wa Serikali, Tito Mwakalinga kwa niaba ya Jamhuri na mapitio ya ushahidi uliopo katika kumbukumbu za Mahakama, wanaona rufaa ya baba mzazi haina mashiko na wanaitupilia mbali.