Mwalimu mkuu, mjumbe wa kamati ya shule wahukumiwa kwa rushwa
Muktasari:
- Washtakiwa hao wawili wametiwa hatiani kwa uhujumu uchumi baada ya kutumia Sh800,000 mali ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.
Simanjiro. Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kitwai A iliyopo Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Simon Mhando na mjumbe wa kamati ya shule hiyo, Petro Orkel, wamehukumiwa kifungo cha nje cha miezi sita na kulipa Sh800,000 walizozitumia bila uhalali.
Mhando na Orkel wamehukumiwa na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Simanjiro, Charles Uisso, baada ya kesi hiyo kuendeshwa na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Faustin Mushi.
Hakimu Uisso, akisoma hukumu hiyo leo Julai 10, 2026, ameeleza kuwa washtakiwa hao wawili wametiwa hatiani kwa uhujumu uchumi kwa kumdanganya mwajiri na kujipatia Sh800,000.
Amesema washtakiwa hao walitumia nyaraka kumdanganya mwajiri, kinyume na Kifungu cha 22, na kusaidia kutenda uhalifu kinyume na Kifungu cha 30, vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, Marejeo ya 2023.
Amesema vifungu hivyo, vikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza, Kifungu cha 57(1) na 61(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, pamoja na makosa ya kughushi kinyume na Kifungu cha 333, 335(a) na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Marejeo ya 2023.
Amesema washtakiwa hao walifanya makosa hayo kwa kuandaa hati nane za malipo zilizokuwa na maelezo ya uongo, kisha mshtakiwa namba moja akawasilisha nyaraka hizo katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo.
Hakimu Uisso amesema nyaraka hizo zilimuaminisha mwajiri kuwa zimeandaliwa na kusainiwa na mwalimu pamoja na kamati ya fedha, huku zikiwa na maelezo ya uongo, hivyo kupata fedha hizo.
Ameeleza kuwa washtakiwa hao walitumia nyaraka hizo zenye maelezo ya uongo na wakaidhinishiwa fedha.
Hakimu huyo amesema washtakiwa hao wametiwa hatiani baada ya kukiri kosa na kupewa adhabu ya kulipa Sh800,000 ili zirudishwe katika shule hiyo, pamoja na kutumikia kifungo cha nje cha miezi sita.
Hata hivyo, washtakiwa hao wawili wamefanikiwa kulipa Sh800,000 walizotakiwa kulipa, na sasa wanatumikia kifungo cha nje cha miezi sita.