Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwamba Ziwa Victoria wasimamisha ujenzi Bandari ya Bukoba

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Dk John Simbamchawene ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya uhamasishaji biashara akiwa na wajumbe wake pamoja na viongozi wa kiserikali katika ukaguzi wa ujuenzi wa mradi huo.

Muktasari:

  • Ujenzi wa Bandari ya Bukoba uliofikia asilimia 63 unakabiliwa na changamoto ya mwamba uliopo chini ya maji wenye ukubwa wa mita 300

Bukoba. Imeelezwa kuwa, mradi wa ukarabati na upanuzi wa Bandari ya Bukoba umesimama kutokana na  kukumbwa na changamoto ya mwamba uliobainika chini ya maji katika Ziwa victoria.

Mkandarasi wa mradi huo, mhandisi Mnanka Maginga amesema hayo leo Jumanne Julai 16, 2024 wakati akitoa taarifa za ujenzi wa  mradi huo kwa wajumbe wa kamati ya kitaifa ya uhamasishaji biashara.

Maginga ameutaja mwamba huo kuwa ni Granite Rocks wenye ukubwa wa mita 300 chini ya maji.

"Ujenzi huu umefikia asilimia 63 tunakabiliwa na changamoto ya mwamba uliopo chini ya maji wenye ukubwa wa mita 300 unaohitaji upasuaji wa kina, mkandarasi amekwishapatikana tunasubiri kibali kwa ajili ya kusaini mkataba," amesema Maginga.

Mradi huo unaotekelezwa kwa miezi 20 unatarajiwa kukamilika Septemba 9, 2024  huku ukijumuisha ujenzi wa miundombinu mingine kama uboreshaji wa magati matatu na jengo la kupokea abiria 350 katika bandari hiyo kwa gharama ya zaidi ya Sh20 bilioni.

Kaimu Mkuu wa Mkoa Kagera, Erasto Sima akisoma taarifa ya  hali ya uchumu wa mkoa jana Jumatatu Julai 15, 2024  wakati kamati hiyo ilipotembelea vituo vya pamoja  vya  forodha mipakani kukagua na kuangalia changamoto zilizopo, amesema Kagera ina fursa nyingi za kiuchumi kutokana na kupakana na nchi nyingi.

Sima ametaja changamoto ya kusimama kwa ujenzi wa mradi wa miundombinu ya Bandari ya Bukoba kutokana na kubainika kuwepo mwamba chini ya maji, hali inayoweza kuzorotesha uchumi wa mkoa.

"Naomba katika kamati hii ya kitaifa  mtembelee huo mradi wa ujenzi  wa bandari  ili muone hali halisi, mwamba ulivyokwamisha kuendelea kwa ujenzi, hii inahatarisha mzunguko wa kibiashara kama hautakamilika kwa wakati," amesema Sima.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa Kagera, Nicholas Basimaki akizungumza na Mwananchi leo Jumanne 16, 2024 amesema ujenzi miradi ya Bandari ya Bukoba Mjini na Kemondo usipokamilika kwa wakati utakwamisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kutanua wigo wa biashara.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara ambaye ni mwenyekiti wa kamati  hiyo, Balozi Dk John Simbachawene amesema kamati hiyo tangu iundwe mwaka 2016 ni ziara yake ya kwanza katika Mkoa wa Kagera.

Dk Simbachawene amesema mkandarasi na uongozi wa mamlaka ya bandari utafute ufumbuzi wa kutatua changamoto ya upasuaji mwamba huo haraka  ili utekelezaji wa mradi uendelee.